Al-Khatib kuongoza wapinzani wa Syria | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.11.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Al-Khatib kuongoza wapinzani wa Syria

Wapinzani wa Syria wamemchagua Ahmed Moaz al-Khatib kuwa kiongozi wa muungano mpya ambao umewaunganisha wapinzani wa Rais Bashar al-Assad.

Uchaguzi huo umefanyika baada ya makundi ya upinzani yaliyogawanyika kuweka pembeni tofauti zao kutokana na makubaliano ya kuunda umoja kufuatia mazungumzo ya Qatar. Ahmed Moaz al-Khatib, aliyewahi kuwa Imamu wa Msikiti wa Umayyad Damascus, ataongoza Muungano wa Majeshi ya Mapinduzi ya Syria na Upinzani, ulioundwa baada ya Baraza la Taifa la Syria kukubali kujiunga na muungano huo mpya. Muungano huo unayajumuisha makundi yaliyopo ndani na nje ya Syria. Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuchaguliwa, Al-Khatib, mwenye umri wa miaka 52 ametoa wito wa kuwepo uhuru, haki na maelewano kwa Wasyria wote wakiwemo kutoka madhehebu ya Wasuni, Alawi, Washia na Wakristu.

Kiongozi huyo mpya alikamatwa mwaka 2011 kwa kuunga mkono vuguvugu la upinzani na kuupinga utawala wa Assad kabla ya kuondoa nchini humo miezi mitatu iliyopita. Al-Khatib anaonekana kama mpinzani huru asiyetoka kwenye kundi lolote la kisiasa na hausishwi na kundi la Udugu wa Kiislamu wala chama chochote cha Kiislamu. Aidha, kiongozi mpya wa Baraza la Taifa la Syria aliyechaguliwa hivi karibuni, George Sabra, amesema uteuzi wa Al-Khatib ni hatua muhimu dhidi ya utawala wa Assad na hatua muhimu kuelekea kupata uhuru. Hata hivyo, Sabra ameitolea wito jumuiya ya kimataifa kuwasaidia wapinzani, la sivyo hawana namna yoyote isipokuwa kujilinda wao wenyewe.

Marekani kuwaunga mkono wapinzani

Wakati huo huo, Marekani imetangaza uamuzi wake wa kuwaunga mkono wapinzani wa Syria walioungana kutokana na mazungumzo hayo ya Qatar. Msemaji msaidizi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Mark Toner amesema wako tayari kuusaidia muungano wa kitaifa katika harakati zao za kumaliza ghasia za Syria zinazosababisha umwagikaji damu na kuanzisha utawala wa amani. Toner amesema kuwa Marekani itashirikiana na Muungano wa Kitaifa wa Syria kuhakikisha msaada wao wa kibinaadamu na usiosabisha mauaji unawafikia wananchi wa Syria.

UN yazitolea wito Israeli na Syria kupunguza mvutano

Ama kwa upande mwingine Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amezitaka Israeli na Syria kupunguza mvutano kati yao kuhusu mgogoro wa eneo la milima ya Golan, huku kukiwa na onyo kwamba mgogoro wa Syria huenda ukasambaa. Msemaji wa umoja huo, Martin Nesirky amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ana wasiwasi kuwepo uwezekano wa mzozo huo kuongezeka. Israeli jana ilirusha risasi za onyo kwa Syria baada ya makombora kutoka upande wa Syria kushambulia eneo la Israeli kwenye milima ya Golan. Ndani ya Syria kwenyewe kiasi watu 121 wameuawa nchini humo Jumamosi iliyopita wakati ghasia zikiendelea. 11 wanaripotiwa kuuawa katika mji wa Deraa. Waasi wa Jeshi Huru la Syria wamedai pia kulitwaa eneo la Ras al-Ain, lililoko karibu na mpaka wa Uturuki.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo
Mhariri:Hamidou Oummilkheir

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com