1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ajali za barabarani tishio Afrika

6 Agosti 2013

Benki ya Dunia imesema kuongezeka kwa makaazi ya mijini katika nchi za Kiafrika kunasababisha matatizo mbali mbali yakiwemo ya afya. Imeelezwa pia kuwa ajali za barabarani zinazidi kuwa nyingi.

https://p.dw.com/p/19Kx8
Ajali ya gari
Ajali ya gariPicha: picture alliance/dpa

Katika ripoti iliyotolewa na Benki ya Dunia, imeelezwa kuwa hadi kufikia mwaka 2020, idadi ya vifo vinavyosababishwa na ajali za barabarani katika nchi za Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara itaongezeka kwa asilimia 80. Nchi hizo zina idadi kubwa zaidi ya ajali za barabarani licha ya kuwa na magari machache kuliko nchi nyingine.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, inakadiriwa kwamba kwa kila wakaazi 100,000 wanauwawa 24 kila mwaka katika ajali za barabarani. Vijana na watu maskini wako kwenye hatari kubwa zaidi. Kufikia mwaka 2015, ajali za barabarani zinatarajiwa kuwa chanzo namba moja cha vifo vya watoto wenye umri kati ya miaka 5 na 15. Kwa njia hiyo, ajali zitakuwa zimesababisha vifo vingi zaidi hata ya magonjwa kama malaria au ukimwi.

Jamii zenye watu maskini ziko hatarini zaidi kwani mara nyingi huishi kando ya barabara zenye magari mengi. Watoto hulazimika kupitia njia za hatari kufika shuleni na mara wanapopata ajali wanakuwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kufa kwa sababu hawafikiwi na huduma bora za afya. Mbali na kusababisha majeraha, ulemavu na hata vifo, ajali zina athari za kiuchumi pia. Inakadiriwa kwamba ajali zimegharimu nchi za Kiafrika asilimia moja hadi tatu ya pato la taifa kila mwaka.

Watoto na watu maskini huathirika zaidi na ajali za barabarani
Watoto na watu maskini huathirika zaidi na ajali za barabaraniPicha: picture-alliance/dpa

Magonjwa yasiyoambukiza yaongezeka

Ripoti ya Benki ya Dunia ilizingatia pia kusambaa kwa magonjwa yasiyoambukizwa kama vile kisukari na saratani. Waandishi wa ripoti hiyo wameeleza kwamba magonjwa hayo yanawapata watu wengi bila ya kugundulika.

Dr. Jill Farrington, ambaye ni miongoni mwa waandishi wa ripoti hiyo, amesema kwamba baadhi ya mambo yanayoleta ajali za barabarani husababisha pia magonjwa yasiyoambukiza.

Mfano mmoja wapo ni suala la watu wengi zaidi kuhamia mijini. Watu hao kwa kawaida hawafanyi mazoezi mengi ya kimwili, jambo linaloweza kusababisha kisukari au matatizo ya moyo. Kuongezeka kwa kipato kunafanya watu wanununue vyakula vya viwandani ambavyo mara nyingi huwekwa sukari, chumvi au mafuta mengi. Wakati huo huo, kuongezeka kwa idadi ya wakaazi wa mijini kunaongeza pia idadi ya wamiliki wa magari na hivyo idadi ya ajali.

Ulevi hatari kwa uendeshaji

Unywaji wa pombe umeelezwa kuwa chanzo kingine cha ajali na magonjwa. Ingawa katika nchi za Kiafrika, watu saba kati ya kumi hawanywi pombe, wale wanaokunywa wanaelezwa kunywa kiasi kikubwa.

Ajali nyingi husababishwa na watu kuendesha wakiwa wamekunywa pombe
Ajali nyingi husababishwa na watu kuendesha wakiwa wamekunywa pombePicha: Getty Images

Hakuna taarifa za kutosha kuhusu idadi ya ajali za barabarani zilizosababishwa na ulevi. Hata hivyo, utafiti uliofanywa Nigeria kati ya mwaka 1996 na 2000 ulionyesha kuwa nusu ya ajali zilizotokea zilihusisha watu waliokuwa wamekunywa pombe.

Lakini katika miaka michache iliyopita ufahamu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza umeongezeka. Kati ya mwaka 2001 na 2008, ufadhili wa kutibu saratani, magonjwa ya moyo na kisukari katika nchi zinazoendelea uliongezeka mara sita. Mwaka 2011 Umoja wa Mataifa ulikuwa na kongamano maalum juu ya magonjwa hayo. Licha ya hayo, miradi ya kupambana na magonjwa yasiyoambukiza yanaunda asilimia tatu tu ya jumla ya misaada inayotolewa duniani kote.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/World Bank

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman