1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cuba imeahidi kufanya uchunguzi kubaini sababu ya ajali

Daniel Gakuba
19 Mei 2018

Ndege chapa Boeing 737iliyomilikwa na Mexico ilianguka karibu na Havana jana muda mfupi baada ya kuruka.

https://p.dw.com/p/2xykf
Kuba, Havanna: Flugzeugabsturz, Helfer bergen Wrackteile der Boeing 737
Picha: picture-alliance/D. Boylan

Cuba imeahidi kufanya uchunguzi kubaini sababu ya ajali ya ndege iliyouwa watu takribani 100 karibu na mji wake mkuu Havana hapo jana. Rais mpya wa nchi hiyo Miguel Diaz Canel aliitembelea sehemu ilikoanguka ndege hiyo, na kusema matukio yote yatafanyiwa uchunguzi na ripoti itatolewa.

Gazeti la serikali ya nchi hiyo la Granma limesema kuwa watu watatu walinusurika katika ajali hiyo, na kuongeza kuwa idadi kamili ya waliokufa ilikuwa 105. Aidha, gazeti hilo lilisema wahanga wengi walikuwa raia wa Cuba, lakini walikuwemo pia raia watano wa kigeni, pamoja na marubani kutoka nje ya nchi.

Ndege hiyo iliyopata ajali ilikuwa chapa Boeing 737 inayomilikiwa na Mexico. Jumla ya watu wanne, wanawake watatu na mwanamme mmoja walipatikana wakiwa hai baada ya ajali hiyo, lakini mwanamme huyo alifariki muda mfupi baadaye. Wanawake hao watatu bado wako katika hali mahtuti.