1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ajali ya ndege ya Air France

Oumilkher Hamidou2 Juni 2009

Chanzo cha ajali bado hakijulikani

https://p.dw.com/p/I1zb
Air France A330Picha: AP

Ajali ya ndege ya Air France -Airbus chapa A330 iliyokua ikitokea Rio de Janeiro nchini Brazil kuelekea Paris nchini Ufaransa,haijulikani bado hadi dakika hii imesababishwa na nini.Hata juhudi za kuchunguza wapi imeangukia ndege hiyo iliyokua na jumla ya watu 228,hazijaleta tija mpaka sasa.

Viongozi wa nchi mbili zinazohusika zaidi na ajali hiyo,Ufaransa na Brazil wanasema hakuna uwezekano hata kidogo wa kugunduliwa wahanga wahai wa ajali hiyo iliyotokea jana alfajiri.

Katika hali kama hii "hakuna chochote chengine cha kufanya isipokua kulia tuu na kuwapa moyo familia" amesema hayo rais wa Brazil Luiz Lula Da Silva akielezea mazungumzo aliyokua nayo pamoja na rais mwenzake wa Ufaransa Nicolas Sarkozy.

"Tumepeyana rambirambi.Hatujui bado nini hasa kimetokea.Tumearifiwa tuu kuhusu uwezekano wa kuvurugika mitambo ya umeme."Amesema.

Watu 228 waliokuwemo ndani ya ndege hiyo,wanatokea katika nchi 32 tofauti,wakiwemo wafaransa 73,wabrazil 58 na wajerumani 26.

Sarkozy nach Flugzeugabsturz
Rais wa Ufaransa Nicolas SarkozyPicha: AP

Rais Nicolas Sarkozy amepangiwa kukutana na familia za wahanga wa ajali hiyo hii leo.Jana rais huyo wa Ufaransa alikwenda katika uwanja wa ndege wa Charles de Gaule alikosema :

"Ni msiba huu ambao Air France haijawahi kuushuhudia.Tumekutana na familia za wahanga.Kila mmoja anaweza kutambua hisia za mama aliyepoteza mtoto wake,kijana aliyepoteza mchumba wake.........."

Usiku kucha ndege za Brazil zenye vifaa vya elektronik,mitambo ya radar na mitambo mengineyo yenye miale ya ukaguzi zimeendelea kusaka.Wataalam wanalenga uchunguzi wao katika eneo la kilomita 1100 katika fukwe za Brazil na Senegal.

Ndege mbili za kijeshi za Ufaransa zimeanza shughuli za kutafuta mahala ndege hiyo ilipoangukia tangu leo asubuhi,baada ya rubani mmoja wa kibrazil kusema "ameona taa zikimeta meta baharini katika eneo ambako ndege ya Air France pengine ndiko ilikoangukia.

Marekani pia imetuma ndege ya kijeshi ya ukaguzi na tume ya waokozi."Watatoa msaada wote unaohitajika kujua nini kimetokea" amesema hayo rais Barack Obama katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni cha Ufaransa.

"Uchunguzi utaendelea mpaka mwisho" amesema kwa upande wake waziri wa ulinzi wa Ufaransa Hervé Morin.

Chanzo cha ajali hiyo,kubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa na shirika la ndege la Ufaransa Air France na ya kwanza ya aina yake kwa ndege hiyo ya Airbus chapa A330,hakijulikani hadi dakika hii tulio nayo.

Mkurugenzi mkuu wa Air France Pierre-Henry Gourgeon amezungumzia juu ya mfululizo wa maelezo ya kiufundi yaliyonaswa kati ya saa 10 na robo za alfajiri,yakimaanisha "vifaa kadhaa viliharibika" na kusababisha "hali ya mparaganyiko isiyokua na mfano ndani ya ndege".

Afisa mwengine wa Air France anazungumzia juu ya uwezekano wa ndege hiyo kupigwa na radi.

Ndege hiyo "ina uwezo" wa kukabiliana na misuko suko ya kila aina ya hali ya hewa katika maeneo ya joto"lakini pengine kulitokea mfululizo wa mambo tofauti" anasema kwa upande wake waziri wa usafiri wa Ufaransa Jean-Louis Borloo.

Mwandishi: Oummilkheir Hamidou/AFP

Mhariri:M.Abdul-Rahman