Aina mpya ya corona yagunduliwa kwa msafiri toka Tanzania | Matukio ya Afrika | DW | 01.04.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Aina mpya ya corona yagunduliwa kwa msafiri toka Tanzania

Kituo cha kudhibiti magonjwa barani Afrika CDC kimesema kimegundua aina mpya ya kirusi cha Corona kutoka kwa msafiri aliyetokea Tanzania kwenda Angola.

Kituo cha kudhibiti magonjwa barani Afrika CDC kimesema kimegundua aina mpya ya kirusi cha Corona kutoka kwa msafiri aliyetokea Tanzania kwenda Angola. Kituo hicho kimesema aina hiyo ya kirusi cha Corona kina uwezo wa kujigeuza kimaumbile hadi mara 40. 

Mkuu wa kituo cha CDC John Nkengasong amesema leo Alhamisi katika mkutano na waandishi wa habari kuwa, kugundulika kwa aina hiyo mpya ya kirusi cha Corona kutoka kwa msafiri aliyetokea Tanzania kunaibua hali ya wasiwasi.

Soma zaidi:Chanjo nyingine ya Covid-19 yaanza kutumika Kenya

Kufuatilia aina hiyo ya kirusi cha Corona huenda ikawa changamoto hasa kutokana na hatua ya serikali ya Tanzania kutotangaza hadharani takwimu zake za watu waliougua ugonjwa wa Covid-19 nchini humo.

Hayati Rais John Magufuli, alipinga juhudi zozote za kupambana na janga la Covid-19 wakati wa uhai wake. Hata hivyo, Nkengasong amesema maafisa wa CDC wanajaribu kutumia njia nyengine tofauti za kushirikiana na mrithi wa Magufuli, Rais Samia Suluhu Hassan juu ya suala hilo.

CDC yatahadharisha juu ya ugumu wa bara la Afrika kufikia lengo lake la utoaji chanjo

John N. Nkengasong Afrika Africa Centres for Disease Control

Mkuu wa mamlaka ya kudhibiti magonjwa barani Afrika John Nkengasong

Mkuu huyo wa CDC pia ametahadharisha juu ya ugumu wa bara la Afrika kufikia lengo lake la utoaji chanjo kufuatia uamuzi wa India wa kupunguza kasi ya usafirishaji wa chanjo kwenda katika mataifa mengine, 

"Hakika uamuzi huo utaathiri uwezo wetu wa kuendelea kutoa chanjo kwa watu. Shehena ya kwanza ya chanjo ilitufikia kupitia mpango wa ugavi wa chanjo wa COVAX, na chanjo nyingi zilikuwa za AstraZeneca kutoka India hasa kutoka taasisi ya matibabu ya Serum. Iwapo chanjo hizo zitachelewa kutufikia, natumai kuwa ucheleweshwaji huo sio wa makusudi au marufuku, lakini iwapo itakuwa hivyo basi itatuathiri sana."

India, iliyopewa jina la "duka la dawa duniani" ilitangaza wiki iliyopita kuwa inasimamisha usafirishaji wa chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 kufuatia ongezeko la maambukizo ya ugonjwa huo unaoshambulia zaidi mapafu nchini India, na kuwa kipau mbele chao sasa ni nyumbani.

Tazama vidio 02:23

Kenya na mapambano ya COVID-19

Idadi kubwa ya chanjo za barani Afrika zimetolewa kupitia mpango wa Covax, unaokusudia usambazaji sawa wa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 duniani kote hasa katika nchi maskini.

Nkengasong amesema mataifa ya Afrika yamepokea zaidi ya dozi milioni 29.1 za chanjo, na kuwa bara hilo limefanikiwa kuwachanja watu milioni 10.3 hasa wafanyikazi wa afya, wazee na watu walio kwenye hatari zaidi kiafya.