Ahmadinejad aidhinishwa rasmi | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 03.08.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Ahmadinejad aidhinishwa rasmi

Kiongozi wa Kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amemuidhinisha Mahmoud Ahmadinejad kuwa rais wa nchi hiyo.

default

Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad.

Kiongozi wa ngazi ya juu wa kidini nchini Iran, Ayatollah Ali Khamenei, leo amemuidhinisha rasmi Mahmoud Ahmadinejad kuwa rais wa nchi hiyo kwa kipindi kingine cha miaka minne. Baada ya kuidhinishwa, Rais Ahmadinejad ataapishwa keshokutwa Jumatano kuiongoza nchi hiyo kwa muhula wa pili.

Kituo cha televisheni ya taifa ya Iran, kimetangaza kuwa Khamenei amemuidhinisha Ahmadinejad, mwenye umri wa miaka 52, kuwa rais wa nchi hiyo ya Kiislamu katika hafla iliyofanyika kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Tehran, ambapo amesema kuwa watu wa Iran wamemchagua mtu wanayemtaka.

Hata hivyo, hafla hiyo haijahudhuriwa na marais wa zamani wa Iran, Hashemi Rafsanjani na Mohammad Khatami. Wengine ambao hawajahudhuria hafla hiyo ni waliokuwa wapinzani wa Ahmadinejad katika kinyang'anyiro cha uchaguzi, ambao ni Mir Hossein Mousavi na Mahdi Karroubi.

Matokeo ya uchaguzi wa Juni 12, mwaka huu uliompa ushindi Ahmadinejad, yaligubikwa na maandamano makubwa kutoka upande wa upinzani, yaliyosababisha vifo vya watu wapatao 30 na mamia wengine kushikiliwa. Ushindi huo ulisababisha mpasuko na viongozi wa kidini waliokuwa wakiwaunga mkono wapinzani na kushutumu jinsi serikali inavyowaangalia wapinzani waliokamatwa kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi.

Jumamosi iliyopita watu wapatao 100 walifikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashitaka ya kuchochea ghasia baada ya uchaguzi. Watu wengine 10 walipandishwa kizimbani jana Jumapili. Hata hivyo, Mousavi amesema kuwa serikali ya Iran iliwatesa waandamanaji hao katika kuwalazimisha kukiri makosa yao ya kuchochea ghasia. Hata hivyo, waandamanaji wengine zaidi ya 200 bado wanashikiliwa, hatua iliyofanya nchi za Magharibi kutoa wito wa kuachiwa huru waandamanaji hao. Viongozi wa upinzani wanamlaumu Ahmadinejad aliyefaidi mapato yaliyotokana na mafuta katika uongozi wake katika kipindi cha kwanza kwa kuharibu uchumi wa nchi hiyo, kutumia vibaya maliasili, kusababisha kupanda kwa gharama za maisha na kufanya hila katika takwimu ili kuficha madhaifu yake.

Khamenei ambaye amekuwa akimuunga mkono Ahmadinejad ametupilia mbali shutuma kuwa uchaguzi huo uligubikwa na hila, huku akizituhumu serikali za nchi za Magharibi, hasa Uingereza, kwa ghasia hizo. Uingereza kwa upande wake imekanusha madai hayo ingawa wasiwasi ulizuka baada ya Iran kuwakamata wafanyakazi tisa raia wa Iran wanaofanya kazi katika Ubalozi wa Uingereza nchini humo.

Aidha, Ahmadinejad alipata upinzani mkali kutoka kwa viongozi wa kidini wenye msimamo mkali baada ya kumteua Esfandiar Rahim Mashaie, kuwa makamu wa kwanza wa rais. Uteuzi huo ulizua gumzo kutokana na kauli ya Mashaie kwamba Iran ni rafiki wa kila mtu ikiwemo Israel. Hata hivyo, Mashaie alijiuzulu wadhifa huo. Hali ilizidi kuwa tete pale Ahmadinejad alipomfukuza kazi Waziri wa Usalama, Gholam Hossein Mohseni Ejeie, kufuatia taarifa za mzozo juu ya uteuzi wa Mashaie.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE/APE)

Mhariri: M.Abdul-Rahman

 • Tarehe 03.08.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/J2R3
 • Tarehe 03.08.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/J2R3

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com