1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afya ya Navalny yazidi kuimarika

Lilian Mtono
10 Septemba 2020

Afya ya mwanasiasa wa upinzani nchini Urusi Alexei Navalny inazidi kuimarika wakati akindelea kupata matibabu baada ya Ujerumani kusema alipewa sumu aina ya Novichok na sasa anaweza kuzungumza tena

https://p.dw.com/p/3iGjK
Berlin Nawalny in Charite | Spezialtrage
Picha: Getty Images/M. Hitij

Navalny alianza kuugua akiwa kwenye ndege inayofanya safari za ndani nchini Urusi mwezi uliopita. Ujerumani inasema Navanly alikuwa muhanga wa jaribio la kuuawa na inataka ufafanuzi kutoka kwa Urusi. Moscow yenyewe ilikwishasema haikupata uthibitisho wowote kwamba mwanasiasa huyo alilishwa sumu. Soma pia: Ujerumani yatishia kuiwekea vikwazo Urusi kuhusu Navalny

Gazeti la Der Spiegel limesema ulinzi wa polisi kwa mwanasiasa huyo umeimarishwa kwa matarajio kwamba anaweza kutembelewa na wageni wengi zaidi wakati afya yake ikizidi kuimarika.

Hata hivyo hakukuwa na ufafanuzi wowote wa haraka kutoka kwenye hospitali anayotibiwa Navalny.

Deutschland Berlin | Polizisten vor der Charité
Ulinzi umeimarishwa katika hospitali ya CharitePicha: Getty Images/S. Gallup

Tukio hili limeibua wasiwasi mpya wa kimahusiano kati ya Urusi na Ujerumani, katika wakati ambapo serikali za magharibi zikiamini kwamba Navalny alipewa sumu na idara za usalama za Urusi zikisaidiwa na maafisa wa ngazi za juu.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo amesema kwamba kulikuwa na uwezekano mkubwa mwanasiasa huyo alipewa sumu kwa maagizo ya maafisa waandamizi wa Urusi. Berlin inakabiliwa na miito ya kuishinikiza Urusi kujibu tuhuma hizo. Baadhi ya wanasiasa wa upinzani wametaka kusitishwa kwa ujenzi wa mradi wa bomba la gesi la Nord Stream 2, kutoka Urusi hadi Ujerumani, ingawa umefikia hatua za kukamilika.

Awali waziri mkuu wa Italia Giuseppe Conte amenukuliwa akisema rais wa Urusi Vladmir Putin amemueleza kwamba ataunda tume ya kuchunguza kisa hicho cha Navalny na alikuwa tayari kushirikiana na mamlaka za Ujerumani.

Russland Moskau Nawalny
Navalny ni mkosoaji mkubwa wa serikali ya UrusiPicha: Reuters/T. Makeyeva

Conte amesema kwenye mahojiano na gazeti la Il Foglia la Italia kwamba rais Putin amemuhakikishia katika mazungumzo ya hivi karibuni kwamba Urusi inaangazia kuondoa kiwingu cha kile kilichotokea. Hata hivyo muda mfupi uliopita ikulu ya Kremlin kupitia msemaji wake imekanusha matamshi hayo na kusema labda kulikuwa na kutoelewana baina ya viongozi hao kuhusiana na kuundwa kwa tume hiyo. Soma pia: Kisa cha Navalny kulishwa sumu chazidisha wasiwasi

Kremlin imesema hawaoni msingi wa kufungua kesi ya uhalifu juu ya madai hayo na kwamba tayari wachunguzi wa Urusi wanaangazia kisa hicho huku ikikemea matamshi ya Pompeo na kusema hayakubaliki.

Katika hatua nyingine, Ujerumani imewasilisha majibu yaliyoonyesha Navalny alipewa sumu hiyi ya Novichok kwa shirika la kudhibiti matumizi ya kemikali za sumu, OPCW, maafisa wa serikali wamesema.

Kaimu msemaji Martina Fietz amewaambia waandishi wa habari kwamba Ujerumani haioni sababu ya kupeleka uthibitisho huo moja kwa moja Urusi na kusema wanaendelea kuiomba kutoa taarifa kuhusu tukio hilo.

reuters