Afrika yagawanyika kuhusu utawala wa mwaka mmoja wa Trump | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.01.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Afrika yagawanyika kuhusu utawala wa mwaka mmoja wa Trump

Januari 20 mwaka huu Rais wa Marekani, Donald Trump atafikisha mwaka mmoja tangu alipoingia madarakani. Katika mwaka wake wa kwanza, Trump hajapata marafiki wengi Afrika.

Watu wa bara hilo wana ghadhabu kutokana na matamshi yake ya hivi karibuni kuhusu wahamiaji, lakini sio kila mmoja anamfikiria vibaya.

Katika mitaa ya mataifa mengi ya Afrika, Trump amekuwa gumzo. Inaelezwa kuwa matumizi yake ya neno la kashfa ''mataifa yaliyovunda'' wakati akiwazungumzia wahamiaji kutoka Haiti na mataifa kadhaa ya Afrika, yamewakasirisha wengi katika bara hilo. Matamshi hayo yamehalalisha mtazamo wa muda mrefu kuhusu kiongozi huyo wa Marekani, kama mbaguzi wa rangi.

Hasira dhidi ya Trump tayari ilianza mwanzoni kabisa wa mwaka wake wa kwanza madarakani, kwa mfano Januari 2017 alivyosaini amri iliyowazuia raia wa mataifa kadhaa ya Kiislamu kuingia Marekani, huku Somalia na Sudan zikiwa miongoni mwa nchi hizo. Nchi nyingi za Afrika zilionyesha ghadhabu yao dhidi ya Trump kupitia majukwaa ya mitandao ya kijamii.

Amri ambayo Trump alisaini kuwapiga marufuku raia wa baadhi ya nchi za Kiislamu mfano Sudan ilisababisha baadhi ya nchi kuwa na hasira na utawala wake

Amri ambayo Trump alisaini kuwapiga marufuku raia wa baadhi ya nchi za Kiislamu mfano Sudan ilisababisha baadhi ya nchi kuwa na hasira na utawala wake

Ingawa Bispo Inocencio Jm Jm kijana kutoka Angola anaandika katika ukurasa wake wa Facebook kwamba Trump ni kiongozi mbaya kuwahi kutokea katika historia ya Marekani, Iberth Garcia pia kutoka Angola yeye ana mtazamo tofauti kabisa. Anasema hadi sasa, Trump amejionyesha kuwa msema kweli na kwamba amewaumbua marais wabaya wa Afrika.

Marafiki wa Trump barani Afrika

Kuna watu ambao bado wanamuunga mkono Trump. Ismail Togolani kutoka Tanzania anaamini kuwa Trump ameifanya Marekani kuwa bora tena na kwamba dunia inamuhitaji mtu kama Trump kwa sasa, vinginevyo hapatokuwa na heshima. Lakini pamoja na pongezi hizo, maoni mengi kuhusu Trump yanaonekana kuwa mabaya. Sekou Samake kutoka Mali, anasema hawawezi kumtegemea Trump kwani hatabiriki.

Naye Barack Mganga kutoka Kenya pia anaonyesha kukatishwa tamaa na utawala wa Trump. Anasema hajaona chochote kikubwa ambacho amekifanya kwa Marekani, zaidi ya kuanzisha maadui wa nchi yake.

Chama tawala nchini Afrika Kusini, African National Congress, ANC kimeyaelezea matamshi ya Trump kama mabaya sana. Serikali ya Botswana imemuita Trump ''mbaguzi wa rangi'' na ''asiyewajibika''. Nchi kadhaa za Afrika ziliwaita mabalozi wa Marekani katika nchi zao kutokana na matamshi hayo. Msemaji wa Umoja wa Afrika, Ebba Kalondo amesema umoja huo umeshtushwa na matamshi hayo, kutokana na hali halisi kwamba Waafrika wengi waliingia Marekani kama watumwa.

Nchi kadhaa za Afrika ziliwaita mabalozi wa Marekani katika nchi zao kutokana na matamshi machafu ya Trump kuhusu Afrika

Nchi kadhaa za Afrika ziliwaita mabalozi wa Marekani katika nchi zao kutokana na matamshi machafu ya Trump kuhusu Afrika

Mwandishi habari kutoka Zimbabwe, Savious Kwinika anasema waandishi wengi wa Afrika kutoka katika bara lote wamekasirika sana na Trump. Kulingana na Kwinika, kiongozi huyo mwenye utata hathamini uhusiano wake na Afrika kama viongozi waliomtangulia walivyofanya.

Kwinika ameiambia DW kila anachokifanya Trump kinasababisha mtafaruku duniani, lakini kwa barani Afrika kwa sasa kunachemka kutokana na matamshi yake ya hivi karibuni. Kwinika anasema hakuna tena heshima dhidi ya Waafrika walionyonywa nchini Marekani wakati walipoiendeleza nchi hiyo miaka mingi iliyopita. Anasema kwamba uhusiano uliopo kati ya Afrika na Trump ni ule wa ''bwana na mtumwa.''

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DW http://bit.ly/2DeVRAz
Mhariri: Saumu Yusuf

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com