Afrika kusini yatangaza janga la kipindupindu mpakani mwake na Zimbabwe. | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.12.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Afrika kusini yatangaza janga la kipindupindu mpakani mwake na Zimbabwe.

Afrika kusini imetangaza janga la kipindupindi katika mpaka wake na Zimbabwe kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ambao mpaka sasa umeshaua watu karibu 800.

default

Wanawake na Watoto wakichota maji kutoka katika chemchem, kufuatia kukatwa kwa maji mjini Harare, hali inayochangia mlipuko wa kipindupindu, kutokana na shida ya maji inayosababsha watu kunywa maji yasiyo salama.


Tangazo hilo limekuja kufuatia idadi kubwa ya Wazimbabwe wanaovuka mpaka kuingia Afrika kusini kwa ajili ya kutafuta matibabu ya ugonjwa huo wa kipindupindu.

Ugonjwa huo umeelezwa kusambaa katika eneo la mpaka kuliko na shughuli nyingi.

Kuanguka kwa uchumi wa Zimbabwe pamoja na mfumo mzima wa afya kumefanya wagonjwa wa ugonjwa huo kujiuguza wenyewe na wengine kujaribu kukimbilia Afrika kusini kusaka huduma.

Msemaji wa serikali katika jimbo la Limpopo, Mogale Nchabeleng amefahamisha kuwa wilaya ya Vhembe ikiwemo eneo la Musina, imetangazwa kuwa eneo la janga hilo, kufuatia mkutano wa dharura mapema wiki hii na kusema kuwa juhudi zaidi zinahitajika kushugulikia tatizo hilo.

Amesema Wazimbabwe wanaingia nchini humo kukimbia majanga ya kiutu yaliyoikumba nchi yao, ambapo wengine tayari wameshaathiriwa na ugonjwa huo wa kipindupindu na kwamba inabidi wawatibie

Musina ni njia kuu wapitayo wahamiaji haramu wa Zimbabwe wanaoingia nchini Afrika kusini, ambao wanakimbia majanga ya kiutu yaliyokumba nchi yao.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa mpaka sasa watu 775 wamekufa kutokana na ugonjwa huo wa kipinduipindu na kwamba zaidi ya elfu 15 wanaaminika kuambukizwa ugonjwa huo.

Jana Waziri wa Afya wa Afrika kusini Barbara Hogan alitembelea jimbo hilo lililoathiriwa na ugonjwa huo kutathmini hali ilivyo.

Afrika kusini tayari imesema kwamba haina mipango ya kuweka karantini kwa Wazimbabwe wanaovuka mpaka kuingia Musina au miji mingine iliyoko mpakani.

Serikali ya Zimbabwe yenyewe inasema ugonjwa huo kwa sasa unadhibitiwa.

Rais Mugabe ametangaza leo kwa njia ya televisheni kwamba kwa sasa hakuna tena kipindupindu baada ya madaktari wa nchi hiyo kwa ushirikiano na wa Shirika la Afya Duniani kuweza kuudhibiti mlipuko huo.

Mlipuko wa Ugonjwa huo, ambao unaenda sambamba na kuanguka kwa uchumi wa nchi hiyo kumezusha miito kutoka katika mashirika ya kimataifa inayojishughulisha na misaada ya kiutu pamoja na wito unaotolewa na viongozi wa nchi za magharibi na baadhi ya nchi za Kiafrika kumtaka Rais wa nchi hiyo Robert Mugabe ajiuzulu.

Katika mtazamo mwengine kuhusiana na mzozo huo wa Zimbabwe, baadhi ya wachunguzi wa siasa za kigeni wanasema maamuzi tofauti yanayotolewa katika kutatua janga hilo la Zimbabwe, kunaweuza kusababisha kusahaulika kwa msimamo mmoja wa Umoja wa Mataifa, kama anavyoelezea Mbunge wa chama cha Mrengo wa Shoto ''Die Linke'' katika bunge la Ujerumani Norman Paech kwamba kila nchi au kila umoja wa nchi, utaachiliwa kujiamulia wapi ambapo kuna majanga ya kiutu na wapi nchi hiyo au jumuia hiyo ya nchi ziendeshe operesheni zao, hapo hati ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Mataifa wenyewe unaweza kusahaulika.

Ameongeza kusema kuwa hapo haki ya mwenye nguvu ndio itakayofanya kazi.

Zimbabwe imekuwa ikilaumu mataifa wapinzani wake kutumia janga hilo la kipindupindu kutaka kumuondoa madarakani Rais Mugabe.
 • Tarehe 11.12.2008
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GDbn
 • Tarehe 11.12.2008
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GDbn
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com