Afrika Kusini: Semenya ni Huntha? | Michezo | DW | 11.09.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Afrika Kusini: Semenya ni Huntha?

Mkasa wa yule mwanariadha wa Afrika Kusini, Caster Semenya, aliyeweka rikodi ya dunia ya kukimbia mita 800 kwa wanawake hivi karibuni hapa Ujerumani umegeuka kuwa ni suala kubwa la uadilifu na siasa.

default

Semenya akishinda mbio za mita 800 mjini Berlin

Hata hivyo, yeye hatakuwa mwanariadha wa kwanza ambaye suala la jinsia yake, kama ni mwanamume au mwanamke, linabaki kuwa sio wazi kabisa. Juu ya mabishano kama Caster Semenye ni jike au dume, huyu hapa Othman Miraji... 

Stella Walsh wa Poland alikuwa bingwa wa michezo ya Olympic katika mbio za mita mia moja hapo mwaka 1932. Baada ya kifo chake mwaka 1980, upasuaji aliofanyiwa huko Marekani uligundua kwamba alikuwa na viungo vya uzazi wa kiume pamoja na kromosomu, yaani chengachenga za shanga  za urathi, za kiume na kike.

Mkimbiaji wa Kihindi, Santhi Soundarajan, alivuliwa medali yake ya fedha katika michezo ya riadha ya Bara la Asia mwaka 2006 baada ya kutopita mtihani wa kumtambua hasa yeye ni wa jinsia gani, kama mwanamume au mwanamke. Baadae bibi huyo aligunduliwa ana aina ya ugonjwa au hitilafu ya kimaumble inayoitwa kwa kiengereza Androgen Insensitivity Syndrome, hali yenye vinasabu vya kiume, lakini ikipingana na homoni za jinsia ya kiume, hali ambayo inaufanya mwili uonekane nje kuwa wa kike.

Kuhusu Caster Semenya wa Afrika Kusini ni tu mwenendo ulio mgumu utakaowahusisha wataalamu wa magonjwa ya kinamama, wale wa vinasaba, wa magonjwa ya ndani ya binadamu, wale wa mifereji inayozalisha homoni katika mzunguko wa damu, wanasaikolojia na mabingwa wengine, pamoja na wanasheria- hao wote ndio watakaoamuwa juu ya suala hili nyeti.

Shirika la kimataifa la  riadha duniani, IAAF, lilitaka ufanywe uchunguzi kutambua jinsia ya Caster Semenya, kama ni mwanamume au mwanamke, baada ya kisa chake kugonga vichwa vya habari katika msimu huu wa mashindano ya riadha pale alipoivunja rikodi bora kabisa duniani ya mbio za mita 800 kwa wanawake. Aliirejesha chini rikodi hiyo sekundi nane.  Uchunguzi aliofanyiwa Caster Semenya, anayeonekana kama mwanamume, uliendeshwa huko Afrika Kusini na Berlin, hapa Ujerumani.

Wanawake kwa kawaida wana kromosoni mbili za X; mwanamuem anakuwa na kromosoni za X na Y; hiyo ina maana ni wanariadha tu wenye kromosoni mbili za X ndio walio na haki ya kushiriki katika mashindano ya kike.

Hata hivyo, Shirika la michezo ya riyadha duniani, IAAF, pamoja na mashirika mengine ya spoti, hayana vipengelee kuhusu hali tafauti ambapo mwanaridha jinsia yake ina utata, kama vile alivyo Caster Semenya.

Habari kutoka Australia zilisema leo kwamba matukeo ya uchunguzi ulitoa ushahidi kwamba Semenya alikuwa ni huntha, yaani mtu mwenye mchanganyiko wa mbegu za kike na za kiume, kwamba hana mfuko wa mayai ya uzazi, lakini ana kokwa za ndani ambazo zinamfanya atoe mara tatu zaidi kiasi cha homoni za kiume kuliko zile zinazotolewa na mwanamke wa kawaida.

Afrika Kusini yaonesha ina watu zaidi walio na jinsia zinazoingiliana kuliko nchi nyingine. Jumuiya ya Afrika Kusini ya jinsia zinazoambatana inasema katika mtandao wake kwamba katika kila watu hamsini basi kuna mmoja ambaye ana viungo vya kujamiiana ambavyo madaktari wanafikiria kuwa sio vya kawaida, na kwamba inaaminiwa kwamba katika kila watu mia tano, basi kuna mtu mmoja ambaye amezaliwa na jinsia mbili.

Shirika la  michezo ya riadha duniani, IAAF, litabidi liamuwe kama Caster Semenya ananufaika zaidi kushinda wanawake wengine, na litataka kujuwa kama mwanariadha huyo wa Afrika Kusini alijuwa kabla juu ya hali yake hiyo, na kama yuko tayari kufanyiwa operesheni.

Uchunguzi wa kujulikana jinsia ya mwanariadha lilikuwa shuruti la lazima  katika michezo ya Olympic baina ya mwaka 1968 hadi 2,000, baada ya  wanariadha wa nchi kadhaa za Ulaya Mashariki walipozusha hali ya wasiwasi. Hivi sasa uchunguzi huo unafanyika tu pale kukiweko shakashaka, maafisa wa michezo hiyo wanashughulika tu na wanariadha ambao wanataka kunufaika kwa kubadilisha jinsia zao.                                            

Mwandishi: Othman Miraji Mhariri: Aboubakary Liongo