1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Josephat Charo
29 Julai 2022

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani walijishughulisha na machafuko katika Jmahuri ya Kidemokrasia ya Congo, ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov barani Afrika.

https://p.dw.com/p/4EqOZ
Demokratische Republik Kongo | Goma | Proteste gegen UN
Picha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Gazeti la Tageszeitung lilikuwa na kichwa cha habari kilichosema: Wakati wa Umoja wa Mataifa umefika mwisho. Mwandishi wa gazeti hilo Dominic Johnson aliandika kuhusu maandamano dhidi ya ujumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa masahriki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo MONUSCO.

Tangu Jumatatu raia wa mashariki mwa Congo wamekuwa wakiandamana kutaka wanajeshi wa Umoja wa Mataifa waondoke. Wanapora na kuharibu vituo vya wafanyakazi wa umoja huo, ambao una idadi kubwa kabisa ya walinda amani nchini Congo kuliko eneo lolote lengine duniani. Mhariri anasema eneo la mashariki mwa Congo linaendelea kupoteza amani huku likiwa na idadi kubwa iliyovunja rekodi ya watu wanaokabiliwa na njaa na waliolazimika kuyakimbia makazi yao.

Lavrov azuru Afrika

Gazeti la Frankfurter Allgemeine liliandika kuhusu ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov barani Afrika. Mwandishi wa gazeti hilo Christian Meier aliandika kuwa Lavrov anaota akijiona katika enzi mpya, akionja ladha ya utegemezi wa nchi nyingi kwa Urusi katika ziara yake ya Afrika. Moyo wa Urusi kwa ajili ya Afrika ni mkubwa kwa sasa.

Katika ziara yake pana Afrika Lavrov aliweka wazi jinsi ari na uvumilivu wa Urusi ulivyo na jinsi uhusiano wa kidplomasia kati ya Urusi na Uganda ulivyo wa muda mrefu, wakati alipoadhimisha miaka 60 ya uhusiano kati ya Uganda na muungano wa zamani wa Sovieti. Wakati huo huo Lavrov aliipongeza Liberia kwa maadhimisho yake ya miaka 175 ya uhusiano wake na muungano huo wa zamani.

Akiwa mjini Kampala Lavrov alisema anaunga mkono kufanyiwa mageuzi baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ili nchi zinazoendelea zipate uwakilishi zaidi. Lavrov aliitembelea Uganda akitokea Jamhuri ya Congo na baadaye kukamilisha ziara yake mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Afrika - Russlands Aussenminister Lawrow in Uganda
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergei Lavrov, kulia, na rais wa Uganda, Yoweri MuseveniPicha: AFP

Macro alitembelea bara la Afrika

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliyatembelea makoloni ya zamani barani Afrika. Ndivyo lilivyoandika gazeti la Frankfurter Allgemeine. Macron alihisi ushawishi wa progaranda ya Urusi wakati wa ziara yake hiyo iliyoanzia nchini Cameroon, na kumpeleka pia Benin na Guinea Bissau. Swali lililoulizwa na mwandishi habari wa Ufaransa ikiwa Cameroon inalaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, rais wa Cameroon Paul Biya mwenye umri wa miaka 89, alisema hakumuelewa na kushika sikio lake.

Mwandishi alichukua tena mikrofoni na akauliza swali hilo kwa sauti ya juu wakati wa mkutano na waandishi habari, rais Biya akiwa ameandamana na Macron. Kwa mara nyingine Biya alitikisa kichwa. Baadaye rais Macron ambaye alikuwa amesimama kando ya rais Biya alilirudia swali hilo.

Swali hilo linabaki kuwa kumbukumbu ya ziara ya kwanza ya Macron Afrika tangu alipochaguliwa tena mwezi Aprili mwaka huu, katika eneo la makoloni yake ya zamani ambako Ufaransa inakabiliwa na mtihani wa ushawishi mkubwa wa Urusi.

Guinea-Bissau | Besuch Emmanuel Macron, Präsident Frankreich | mit Umaro Sissoco Embalo, Präsident
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, kulia, na rais wa Guinea Bissau Umaro Sissoco EmbaloPicha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Jeshi la Ujerumani njia panda Mali

Gazeti la Neues Deutschland liliandika kuhusu jeshi la Ujerumani Bundeswehr kuwa katika njia panda nchini Mali. Migogoro kati ya Umoja wa Mataifa na serikali ya Mali imeongezeka. Ujumbe wa amani wa umoja huo nchini Mali huenda ukafika mwisho kwa sababu kutokana na vita vya Urusi nchini Ukraine, mizozo mingine inapoteza nguvu na haiangaziwi tena kama ilivyokuwa hapo kabla.

Hali nchini Mali, ambako jeshi la Ujerumani Bundeswehr lina idadi kubwa ya wanajeshi wake wanaohudumu nje ya nchi, ni tete. Lakini taarifa iliyotolewa hivi karibuni na jeshi la Mali iliuhakikishia umma wa Mali kwamba hali imedhibitiwa na wanaweza kuendelea na shughuli zao kama kawaida, hatua ambayo inajaribu kufunika halli halisi iliyopo. Makundi ya wapiganaji wa jihadi wamedhihirisha wanaweza kufanya mashambulizi makubwa kama walivyofanya katika maeneo ya Mopti na Koulikoro.

Südafrika I Cyril Ramaphos I Untersuchung zu Korruptionsvorwürfen
Rais wa Afrika Kusini, Cyril RamaphosaPicha: Rodger Bosch/AFP

Ramaphosa akabiliwa na mtihani

Gazeti la Tageszeitung liliandika kuhusu rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa akisuasua kutafuta udhibiti katika chama tawala cha African Nationa Congress, ANC. Chama hicho chenye ushawishi mkubwa kinaondoa uungwaji mkono kutoka kwa Ramaphosa. Kuongezeka kwa machafuko kunaathiri mustakhbali wa taifa na rais mwenyewe. Mhariri alisema limekuwa jambo la kawaida kwa Ramaphosa kuzomewa na kupigiwa kelele za kejeli.

Kwamba kejeli hizi zinatolewa na makomredi wenzake kunadhihirisha dhahiri shahiri kwamba Ramaphosa anapoteza udhibiti wa chama cha ANC, na hata pia wa nchi. Wikendi iliyopita chama cha ANC kilifanya mkutano wake wa kitaifa katika jimbo la KwaZulu Natal, ambako ndio ngome ya chama na ambako Ramaphosa anakabiliwa na upinzani mkali. Ramaphosa hakuungwa mkono katika jimbo hilo katika mchakato wa kumrithi rais mstaafu Jacob Zuma anayetokea jimboni humo, badala yake jimbo hilo lilimuunga mkono mke wa Zuma, Nkosazana Dlamini Zuma, ambaye hakufanikwa kumrithi mume wake.

(Inlandspresse)