1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef
13 Mei 2022

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yanazungumzia juu ya ukame kwenye upembe wa Afrika. Migogoro ya kivita kuanzia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hadi Msumbuji na jukumu la jeshi la Ujerumani la kulinda amani nchini Mali.

https://p.dw.com/p/4BFsz
Symbolbild Hunger
Picha: Daniel Kubirski/dpa/picture alliance

Neue Zürcher Zeitung

Makala ya gazeti la Neue Zürcher juu ya maafa ya ukame kwenye upembe wa Afrika inaelezea kiwango cha ukame kwenye sehemu hiyo hakina mfano katika muda wa miaka 40 iliyopita. Gazeti hilo linatahadharisha kwamba watu wapatao milioni 20 wamo katika hatari ya kukumbwa na baa la njaa kutokana na ukame huo.

Neue Zürcher linataarifu kwamba tayari watu wameshakufa kwenye sehemu ya Turkana ya kaskazini mwa Kenya. Watu wanapoteza mifugo yao katika eneo hilo. Gazeti hilo linasema watu waliomo katika hatari ya kufa njaa wako kwenye eneo linalozijumuisha Ethiopia, Kenya na Somalia.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung limeandika juu ya migogoro ya kivita inayoanzia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hadi Msumbuji. Linasema juhudi za kuleta suluhisho la amani zimeshindakana na badala yake mapambano yanaendelea kati ya waasi na majeshi ya serikali. die tageszeitung linatilia maanani kwamba viongozi wa waasi walikutana na wajumbe wa serikali ya Kongo mjini Nairobi katika juhudi za kuleta ufumbuzi. Gazeti linasema mazungumzo hayo hayakuleta matunda yoyote na linafahamisha kuwa wakati wa mazungumzo yalipokuwa yanafanyika mjini Nairobi mapigano yaliendelea mashariki mwa Kongo kati ya waasi wa kundi la M23 na majeshi ya serikali.

Gazeti la die tageszeitung linakumbusha kuwa Rais Tshisekedi aliahidi kuleta amani mara tu baada ya kuingia madarakani na linauliza Jee atatimiza ahadi hiyo kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwaka ujao.

Gazeti la die tageszeitung pia linatukumbusha kwamba majeshi ya Rwanda yanapambana na waasi wenye itikadi kali kwenye jimbo la Msumbiji la Cabo Delgado. Waasi hao wanajitambulisha kuwa washirika wa kundi la ADF linaloendesha harakati za kigaidi nchini Kongo. Na ndiyo sababu gazeti la die Tageszeitung linaitilia maanani ziara ya rais wa Msumbuji Filipe Nyusi aliyofanya nchini Uganda mwezi uliopita. Uganda  imekubali kuiunga mkono Msumbiji kijeshi.

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine wiki hii limeandika juu ya jukumu la jeshi la Ujerumani la kulinda amani nchini Mali. Linasema jukumu hilo limekuwa gumu kutokana na msimamo wa serikali ya Mali wa kuweka kifua mbele kutokana na kuungwa mkono na Urusi.

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Christine Lambrecht amethibitisha kwamba Ujerumani haitaendelea kushiriki katika mradi wa Umoja wa Ulaya wa kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa Mali. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linafahamisha kuwa uamuzi juu ya jukumu la wanajeshi wa Ujerumani nchini Mali utatolewa na bunge la Ujerumani mwishoni mwa mwezi huu. Umoja wa Mataifa pia utatoa uamuzi mnamo mwezi wa huu. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema maamuzi hayo yatakuwa magumu hasa baada ya Ufaransa kuamua kuyaondoa majeshi yake kutoka Mali na baada ya serikali ya Mali kuanza kushirikiana na Urusi.

Ni maoni ya gazeti hilo kwamba itakuwa vigumu kwa Mali kuwadhibiti magaidi bila ya kuungwa mkono na Umoja wa Mataifa. Pia linasema pana hatari ya magaidi hao ya kuweza kujitandaza hadi katika nchi za jirani kama Ivory Coast.

Die Welt

Gazeti la Die Welt linauzungumzia uamuzi wa Uingereza wa kuwahamisha wakimbizi walioingia nchini humo na kuwapeleka Rwanda. Linasema uamuzi huo ni wa utatanishi. Gazeti la Die Welt linaeleza kuwa kati kati ya mwezi wa Aprili waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson alitangaza uamuzi wa kuwapunguza wakimbizi nchini mwake na kuwapeleka Rwanda ambako watakaa huko wakati wakisubiri maombi yao yakishughulikiwa. Kwa upande wake Rwanda imepokea pauni milioni 120.

Hata hivyo gazeti la Die Welt linasema uamuzi huo wa Uingereza unakosolewa kutoka pande zote. Shirika  la wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR limesema kukwepa majukumu ni jambo lisilokubalika. Mashirika 160 ya misaada na haki za kiraia ya nchini Uingereza yanataka makubaliano yaliyofikiwa baina ya Uingereza na Rwanda yabatilishwe. Mashirika hayo yamesema mkataba huo ni wa aibu! 

Baadhi ya wanasiasa wamesema nchi tajiri kama Uingereza zinapaswa kutekeleza wajibu wao wa kimataifa katika kuwahudumia wakimbizi kwa namna inavyopasa. Gazeti la Die Welt linasema nchini Rwanda pia vijana wanalalamika juu ya uamuzi wa Uingereza na serikali yao. Wanasema ajira kwa wakimbizi hao  zitatoka wapi ikiwa vijana wa Rwanda wenyewe wanasaga lami baada ya kumaliza masomo.!

Vyanzo: Deutsche Zeitungen