1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri:Josephat Charo
11 Machi 2022

Magazeti ya Ujerumani yanazungumzia kuhusu nchi za Afrika jinsi zinavyoathirika kutokana na vita vya nchini Ukraine. Kampuni ya madawa ya Marekani, Mordena inakusudia kujenga nchini Kenya kiwanda cha kutengeneza chanjo.

https://p.dw.com/p/48LGd
Zeitungen Reaktionen | Washington Sturm auf Kapitol
Picha: Sean Gallup/Getty Images

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung limeandika jinsi nchi za Afrika zinazovyoathirika pia kutokana na vita vya nchini Ukraine. Linasema ingawa ziko mbali nchi za Afrika zinahitaji fuko la nafaka la Urusi na Ukraine. Gazeti hilo limelinukuu shirika la chakula duniani WFP likisema, ikwa ngano kutoka Ukraine na Urusi haitasafirishwa nje upatikanaji wa chakula unaweza kutatizika zaidi barani Afrika.

Shirika hilo limesema migogoro ndiyo inayosababisha njaa na utapiamlo duniani na limefahamisha kuwa watu milioni 283 wamo hatarini kukumbwa na baa la njaa na wengine milioni 45 tayari wanapiga mbiu ya mgambo. Gazeti la die tageszeitung linatwambia kwamba asilimia 18 ya ngano na asilimia 40 ya mafuta ya kupikia ya aina ya alizeti yanatoka kwenye eneo ambalo sasa limo katika mgogoro. Nchi za pembe ya Afrika zilizomo katika hatari kukumbubwa na athari za vita vya nchini Ukraine ni pamoja na Sudan, Kenya, Sudan Kusini na Ethiopia.

Frankfurter Allgemeine Zeitung

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linazungumzia juu ya msimamo wa nchi za Afrika kuhusu vita vya nchini Ukraine. Linasema nchi kadhaa za Afrika hazikuliunga mkono azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa juu ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine linauliza jee kwa nini? Hata hivyo gazeti linasema wapigania ukombozi wa zamani nchini Afrika Kusini wamepaza sauti zao na kusema kwamba msimamo wa Umoja wa Kisoviet wa kuunga mkono harakati za ukombozi kusini mwa Afrika hauwezi kuhalalisha yanayotokea leo.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema nchi 35 za Afrika hazikulipigia kura azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la kupinga vita vya nchini Ukraine. Gazeti hilo linaeleza kuwa Afrika Kusini ni mwanachama wa nchi zinazoinukia kiuchumi maarufu kwa jina la BRICS jumuiya inayozileta pamoja, Afrika Kusini, India, Brazil, China na Urusi. Gazeti hilo linatilia maanani kuwa Afrika Kusini haikupiga kura kwenye baraza kuu. Linaeleza kuwa nchi hiyo inajaribu kutetea msimamo wake wa kutoegemea upande wowote na limemnukuu mwanasheria Richard Calland kutoka chuo kikuu cha Cape Town akieleza kwamba uamuzi wa kutopiga kura unatokana na kutambua uhalisia wa hali.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema nchi zingine za Afrika zilikuwa na sababu nyingine kwa nini hazikupiga kura. Pamoja na sababu hizo ni uhusiano wa kihistoria, kiitikadi, kiuchumi na biashara ya silaha.Mnamo mwaka huu nusu ya silaha ambazo ilinunua zilitoka Urusi.

Handelsblatt

Kampuni ya madawa ya Mordena inakusudia kujenga nchini Kenya kiwanda cha kutengenezea chanjo dhidi ya magonjwa makali ya nchi za joto. Hizo ni habari zilizoandikwa kwenye gazeti la Handelsblatt. Linasema kampuni hiyo ya Marekani inalenga shabaha ya kuziunga mkono nchi zenye vipato vya chini katika juhudi za kupambana na magonjwa ya kuambukiza na kwa ajili hiyo kampuni hiyo itawekeza dola milioni 500 ili kutengeneza chanjo nchini Kenya.

Gazeti la Handelsblatt linafahamisha kuwa hadi kufikia mwaka 2025 kampuni hiyo ya Marekani ya Moderna itaanzisha miradi 15 ya utafiti na uzalishaji wa chanjo dhidi ya magonjwa ya kuambukiza kama vile Kifua Kikuu, Ebola na homa ya manjano.Gazeti linasema lengo la mradi huo ni kuzipasia nchi za Afrika ujuzi na kuzifungulia uwezo wa kutengeneza dawa na chanjo.

Neues Deutschland

Gazeti la Neues Deutschland linazungumzia juu ya sakata la wakimbizi kutoka Sierra Leone linaloendelea katika mji wa Munich kusini mwa Ujerumani. Kwa muda wa miezi kadhaa wakimbizi hao wamekuwa wanapigania haki ya kupatiwa hifadhi ya ukimbizi nchini Ujerumani. Hata hivyo gazeti la Neues Deutschland linaripoti kwamba watu hao wanakaribia kufukuzwa nchini. Gazeti hilo linatufahamisha kuwa wakimbizi hao wapatao 300 wamejenga kambi mbele ya ofisi ya uhamiaji ya mji wa Munich ili kusisitiza haki zao za kibinadamu lakini bado wanaendelea kuishi na wasiwasi.

Gazeti la Neues Deutschland linaeleza kuwa wakimbizi hao wamechukua hatua hiyo baada ya kukutana na wajumbe wa serikali ya Sierra Leone waliokuja Ujerumani kuthibitisha nasaba za watu hao ili wapatiwe hati za kusafiria na hivyo waweze kurudi nyumbani Sierra Leone. Neues Deutschland linasema idara ya uhamiaji haitambui sababu ya watu hao kuomba ukimbizi nchini Ujerumani.