1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
26 Novemba 2021

Masuala na matukio yaliyozingatiwa na magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika mnamo wiki hii ni pamoja na matukio ya nchini Ethiopia. Matatizo ya kijamii yanayowasibu watu nchini Afrika Kusini na mengineyo.

https://p.dw.com/p/43Wlf
Äthiopien I Tigray-Krise
Picha: AP/picture alliance

die tageszeitung

Matukio ya nchini Ethiopia yaliyozingatiwa na gazeti la die tageszeitung. Linasema waziri mkuu wa nchi hiyo Abiy Ahmed ameondoka mjini Addis Ababa ili kwenda kusimama mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya waasi wa Tigray. Gazeti linasema msemaji wa serikali ya Ethiopia mjini Addis Ababa amethibitisha kwamba waziri mkuu Abiy Ahmed amepiga ripoti kwa makamanda wa majeshi ya serikali. Gazeti la die tageszeitung linaeleza kuwa juhudi za kidiplomasia za kuleta amani mpaka sasa zimeshindikana licha ya kufanyika kwa wiki kadhaa. Viongozi wengine kadhaa wa serikali ya Ethiopia wamefuata mfano wa waziri mkuu huyo.

Hata hivyo gazeti hilo linasema waasi wa Tigray hawajameza propaganda ya waziri mkuu huyo na badala yake  wameonyesha picha za wanajeshi wa serikali waliotekwa ili kuashiria kwamba wanazo nguvu kubwa zaidi kuliko za majeshi ya serikali kuu. Waasi wa Tigray wanadai kwamba wako umbali wa kilometa 200 kutoka mji mkuu Addis Ababa.

Gazeti la die tageszeitung linautathmini uamuzi wa waziri mkuu Abiy Ahmed wa kwenda vitani mwenyewe kuwa hataki tena mazungumzo na waasi. Linasema uamuzi huo ni pigo kubwa kwa juhudi zinazofanywa na wanadiplomasia wa Marekani na Umoja wa Afrika. Gazeti hilo limemnukulu mjumbe wa Marekani Jeffrey Feltmann akisema kwamba matukio kwenye uwanja wa mapambano yanakwenda haraka kuliko juhudi za kidiplomasia.

Süddeutsche Zeitung

Gazeti la Süddetsche wiki hii linazungumzia juu ya matatizo ya kijamii yanayowasibu watu nchini Afrika Kusini. Linasema katika kitongoji kimoja cha Soweto mama mmoja ameeleza kuwa hakumbuki ni lini kwa mara ya mwisho aliweza kuchota maji karibu ya nyumbani kwake. Mama huyo Matatiso Lebajou, ameeleza kuwa sasa anapaswa kwenda mwendo mrefu ili kuweza kupata maji. Gazeti la Süddeutsche linakumbusha ahadi zilizotolewa na viongozi juu ya kuleta maisha bora kwa waafrika nhini Afrika Kusini baada ya kuondolewa mfumo wa kibaguzi. Gazeti limemnukulu mama huyo Lebajou akisema ahadi nyingi bado hazijatimizwa. Uhaba wa maji ni mojawapo ya matatizo.

Hata hivyo gazeti hilo linatilia maaanni kwamba mamilioni ya nyumba yamejengwa kwa ajili ya waafrika, watoto wamepata fursa za elimu na tabaka la kati la watu weusi limejengwa lakini pia linazingatia ukweli kwamba mambo mengi yamekwama. Ukosefu wa ajira umeongezeka na kufikia asilimia 34. Miundo mbinu inasambaratika kwenye sehemu nyingi. Nisthati ya umeme ni ya mashaka na mamilioni ya watu miongoni mwao, Matatiso Lebajou hawapati maji kwa uhakika nchini Afrika Kusini.

Ufisadi bado umetanda Afrika Kusini

Gazeti la Süddeutsche linasema ufisadi bado umetanda chini ya serikali ya chama tawala cha ANC licha ya rais Cyril Ramaphosa kuchukua hatua kali za kupambana na ufisadi. Gazeti hilo pia linasema makampuni ya kimataifa pia yanashiriki katika wizi. Linasema kampuni hizo za kimataifa zinalenga sehemu ambapo zinaweza kuiba mamilioni ya fedha, mfano ni kampuni ya ushauri inayoitwa McKinsey.

Gazeti linasema kampuni maarufu ya Software ya Ujerumani, SAP hivi karibuni ilikuwamo katika vichwa vya habari kutokana na kuhusika na kashfa iliyosababishwa na uhaba wa maji kwenye kitongoji cha Soweto. Gazeti hilo linasema kampuni hiyo ilifikia mikataba miwili na wizara ya maji ya Afrika Kusini, ilipata malipo lakini haikutoa huduma. Süddeutsche linaeleza kwamba kampuni hiyo imesbabisha shida ya maji kwa mamilioni ya watu kama Matatiso Lebajou nchini Afrika Kusini.

Neue Zürcher Zeitung

Gazeti la Neue Zürcher linazizungumzia nchi tatu muhimu za barani Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara. Linasema nchi hizo Nigeria, Afrika Kusini na Ethiopia zinayaumba. Gazeti hilo linasema nchi hizo tatu ni muhimu kisiasa na kiuchumi barani Afrika. Kwa pamoja zinachangia nusu ya tija ya uchumi wa nchi za Kusni mwa Jangwa la Sahara. Thuluthi ya watu wa Afrika wanaishi katika nchi hizo tatu.

Nchini Nigeria peke yake, wako watu zaidi ya milioni 200. Hata hivyo gazeti la Neue Zürcher linasema nchi hizo tatu zimeingia katika matatizo mnamo miaka ya hivi karibuni na siyo tu kutokana na janga la maambukizi ya virusi vya corona. Gazeti linasema Ethiopia sasa imo katika mgogoro wa kivita na imo hatarini kumegeka. Uchumi wake pia ni taabani. Juu ya Afrika Kusini gazeti la Neue Zürcher linasema nchi hiyo pia inapitia misukosuko ya kisiasa na kiuchumi. Ufisadi bado unailemea Afrika Kusini.Tofauti kati ya masikini na matajiri inaongezeka. Hivi karibuni ghasia zilisababisha vifo vya mamia kadhaa ya watu.

Kuhusu Nigeria Neue Zürcher linasema mpaka sasa serikali ya rais Muhammadu Buhari bado haijafanikiwa kuwazima magaidi. Mara kwa mara watu na hasa watoto wa shule wanatekwa nyara. Matatizo ya kiuchumi yamerudi baada ya Nigeria kutumbukia tena katika mdororo wa uchumi. Gazeti la Neue Zürcher linasema nchi hizo tatu muhumi barani Afrika hazina matumaini ya kuibuka na nguvu mpya karibuni badala yake gazeti linaeleza Nigeria, Afrika Kusini na Ethiopia zitaziathiri nchi jirani kisiasa na kiuchumi. 

die tageszeitung

Makala nyingine ya gazeti la die tageszeitung juu ya matukio ya nchini Libya. Linazungumzia juu ya kujiuzulu kwa mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Jan Kubis wakati Libya  inajitayarisha kwa uchaguzi wa rais mwezi ujao. Gazeti ladie tageszeitung linasema uchaguzi huo unapaswa kuileta tena Libya pamoja. Gazeti linasema sababu ya mjumbe huyo kujiuzulu haijulikani lakini linaeleza kuwa uamuzi wake umefanyika wakati mbaya.

Uchaguzi wa rais umepangwa kufanyika tarehe 24 mwezi ujao nchini Libya na gazeti linatilia maanani kwamba matayarisho yote yameshakamilishwa. Licha ya matayarisho hayo gazeti la die tageszeitng linasema kujiuzulu kwa mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa Jan kubis ni hatua inayosababisha wasi wasi juu ya uchaguzi ujao.

Vyanzo:/Deutsche Zeitungen