1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef
27 Agosti 2021

Magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya Afrika kuhusu matukio ya kisiasa nchini Tanzania. Hissene Habre aliyekuwa rais wa Chad amekufa kutokana na maradhi ya corona na Ethiopia yatengeneza mtandao wake wa kijamii.

https://p.dw.com/p/3zYsP
Samia Suluhu, Vizepräsidentin Tansania
Picha: DW/Said Khamis

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung juu ya matukio ya kisiasa nchini Tanzania. Linasema upinzani unazimwa nchini humo. Gazeti hilo linasema hayo baada ya kiongozi wa chama cha upinzani cha Chadema, Freeman Mbowe kutiwa ndani kutokana na madai ya ugaidi. die tageszeitung linasema rais Samia Suluhu Hassan anaendelea na mkondo wa rais wa hapo awali hayati John Magufuli. Hata hivyo alipoingia madarakani baada ya kifo cha Magufuli rais Samia Suluhu Hassan alisifiwa kwa juhudi za kuondoa udikteta nchini Tanzania. Lakini sasa yeye pia ameingia katika lawama.

Gazeti linaeleza kuwa Mbowe anakabiliwa na mashtaka ya kufadhili ugaidi, na limemnukulu mkurugenzi wa shirika la Amnesty International kanda ya kusini mwa Afrika Deprose Muchena akisema kukamtwa kwa Mbowe ni njama za kuunyamazisha upinzani nchini Tanzania. Hata hivyo gazeti hilo limemnukulu rais Samia Hassan akisema kwamba Mbowe alipanga kukamatwa kwake kuonekane kana kwamba hatua hiyo inatokana na mwito wake wa kuleta mageuzi ya katiba.

Neue Zürcher Zeitung

Gazeti la Neue Zürcher limeandika juu ya dikteta Hissene Habre aliyekuwa rais wa Chad kuanzia mwaka 1982 hadi 1990. Kwa mujibu wa taarifa Habre amekufa kutokana na maradhi ya corona. Chini ya utawala wake watu  wapatao 40,000 waliuliwa. Baada ya kupinduliwa alikimbilia Senegal na huko ndiko alikofariki.

Gazeti la Neue Zürcher linasema Habre alipewa adhabu ya kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya mauaji, ubakaji na udhalimu wa utumwa. Gazeti linatilia maanani kwamba kesi ya Habre ilikuwa ya kihistoria barani Afrika. Ilikuwa kesi ya kwanza kufunguliwa dhidi ya kiongozi nje ya nchi yake.

Mwanzoni mwa kesi, Ubelgiji ilitoa amri ya kukamatwa kwa Habre. Gazeti la Neue Zürcher linaeleza kuwa Mahakama ya kimataifa ICC iliiagiza Senegal imkabidhi kwenye mahakama hiyo au imfungulie mashtaka. Mnamo mwaka 2016 hatimaye alihukumiwa nchini Senegal na kupewa adhabu ya kifungo cha maisha jela.

Süddeutsche Zeitung

Gazeti la Süddeutsche linatufahamisha kwamba Ethiopia inatengeneza mtandao wake wa kijamii. Gazeti hilo linasema Ethiopia imefanya uamuzi huo baada ya watu kutoa picha feki zikimwonyesha waziri mkuu Abiy Ahmed akiwa mtupu na amekufa. Maalfu ya watu waliziona picha hizo feki. Zilimwonyesha waziri mkuu huyo ati akipelekwa Italia kwa ajili ya matibabu na baadae nchini Ujerumani. Mara walimwonyesha akiwa ndani ya gari la wagonjwa na mara akiwa kwenye kitengo cha mahututi.

Uongo huo ulionyeshwa kwenye Facebook na Twitter. Süddeutsche linaeleza kwamba siku chache baadae waziri mkuu huyo wa Ethiopia Abiy Ahmed aliwaambia watu wake kwamba alikuwa mzima wa afya lakini wajihadhari na habari feki.

Gazeti linafahamisha kwamba kutokana na kadhaia hiyo Ethiopia imeamua kujenga mtandao wake wa kijamii utakaochukua nafasi ya Facebook, Whatsapp na Twitter. Gazeti la Süddeutsche limemnukulu mkuu wa shirika la habari na usalama la nchini Ethiopia akieleza kuwa mitandao ya kijamii imegeuka kuwa majukwaa ya kisiasa.

Mkuu huyo amekaririwa akisema kwamba hakuna anayetaka kuipiga marufuku mitandao ya kijamii nchini Ethiopia bali lengo ni kuifanya isiwe na mvuto tena. Tangu kuzuka kwa vita vya Tigray habari feki na za chuki zimekuwa zinaongezeka kwenye mitandao ya kijamii nchini Ethiopia.

Neues Deutschland

Gazeti la Neues Deutchsland limeandika habari juu ya mwogeleaji kutoka Uganda, ambaye ni mshiriki mwenye umri mdogo kuliko wote kwenye mashindano ya olimpiki ya walemavu mjini Tokyo. Neues Deutchsland limesema mwanamichezo huyo Husnah Kukundakwe mwenye umri wa miaka 14 ameshakuwa mtu maarufu nchini Uganda hata kama bado hajapata medali. Mwenyewe amesema ameshapata mafanikio kuvuka kiwango alichotarajia.

Gazeti la Neues Deutchsland linasema mbali na kufurahia michezo Husnah Kukundakwe anakusudia kuwahamasisha watu ambao ni walemavu nchini Uganda. Kukundakwe aliyezaliwa bila ya sehemu ya chini ya mkono anazungumza kana kwamba maneno yanatoka kwa mtu mzima. Gazeti linasema mtoto huyo anapendelea kukutana na watu ili kujenga urafiki. Amesema anafurahia kushiriki kwenye mashindano ya olimpiki mjini Tokyo.

Gazeti la Neues Deutschland linafahamisha kwamba Husnah alianza kuwa maarufu baada ya kushiriki kwenye mashindano ya kuogelea ya ubingwa wa dunia mjini London miaka miwili iliyopita. Lengo la dada huyo gazeti linasema ni kuanzisha wakfu ili kuwasaidia walemavu wanaotaka kushiriki kwenye michezo.

Vyanzo:/Deutsche Zeitungen