1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Babu Abdalla
20 Agosti 2021

Magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya Afrika kuhusu Uganda kuwachukua wakimbizi 2000 wa Afghanistan. Ushindi wa Hakainde Hichilema katika uchaguzi wa rais nchini Zambia na mengineyo.

https://p.dw.com/p/3zDmy
Afghanistan I Evakuierungsflüge aus Kabul
Picha: Marc Tessensohn/Bundeswehr/dpa/picture alliance

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung ambalo limeandika juu ya Uganda kuwachukua wakimbizi 2000 kutoka Afghanistan baada ya kufikia mapatano na Marekani. Gazeti hilo linasema shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia wakimbizi UNHCR bado halijatoa taarifa ya hakika iwapo watu hao watabakia nchini Uganda au wataendelea na safari. Hata hivyo waziri wa Uganda anayeshughulikia maswala ya wakimbizi amesema waafghan hao watakaa Uganda kwa muda wa miezi mitatu kwanza.

Gazeti linauliza je Marekani imetoa kiasi gani cha fedha kwa ajili ya mahitaji ya wakimbizi hao? linasema tayari wako wakimbizi milioni 1.5 nchini Uganda. die tageszeitung linafahamisha kwamba Uganda na Marekani zinashirikiana kijeshi. Wanajeshi wa Uganda kwa miaka mingi wamekuwa wakilinda sehemu muhimu za usalama nchini Afghanistan kama waajiriwa wa kampuni binafsi za  Marekani.

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema kuchaguliwa kwa kiongozi wa upinzani Hakainde Hichilema kuwa rais kunaleta matumaini ya kufanyika mageuzi nchini Zambia na hali hiyo inajenga mazingira mazuri ya kufanyika mazungumzo na shirika la fedha la kimataifa IMF juu ya kupatiwa mkopo mpya na kuweka utaratibu mwingine wa kulipa madeni ya kimataifa. Gazeti hilo linasema Hichilema alishinda kwa kupata kura milioni 2.8 na kumshinda rais aliyekuwamo madarakani Edgar Lungu kwa kura milioni moja.

Gazeti  la Frankfurter Allgemeine limemnukulu bwana Hichilema akisema sasa ni wakati wa kuleta mabadiliko. Linasema analenga shabaha ya kurekebisha uchumi wa Zambia. Frankfurter Allgemeine linakumbusha kwamba rais Lungu aliwatia wasiwasi waekezaji vitega uchumi kutokana na mipango yake ya kutaifisha migodi na kuongeza kodi. Uchumi wa Zambia ulishuka kwa zaidi ya asilimia 3 mwaka uliopita licha ya bei nzuri za malighafi kwenye soko la dunia.

Neue Zürcher

Gazeti la Neue Zürcher limeandika juu ya habari za kutia wasiwasi katika nchi za Afrika magharibi. Linasema maradhi ya Ebola yamejitokeza tena nchini Ivory Coast kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1994. Mtu aliyekutwa na maradhi hayo ni msichana mmoja mwenye umri wa miaka 18 aliyeingia Ivory Coast kutokea Guinea. Na sasa amelazwa hospitali kwenye chumba cha pekee yake. Gazeti la Neue Zürcher linakumbusha kwamba maambukizi ya virusi vya Ebola yalizikumba Liberia na Sierra Leone kati ya miaka ya 2014 na 2016. Linakumbusha pia kwamba watu 28,000 waliambukizwa na 11,000 walikufa.

Gazeti linasema shirika la afya duniani WHO limeelezea wasi wasi juu ya taarifa hizo kwamba maradhi ya Ebola yamegundulika Abidjan mji wenye wakaazi milioni 4. Hata hivyo gazeti hilo linatilia maanani kwamba hatua kubwa zimepigwa katika kupambana na maradhi hayo. Njia za tiba zimekuwa bora zaidi na pia ziko chanjo za aina mbili.

Süddeutsche Zeitung

Gazeti la Süddeutsche linatupeleka Angola ambako binti wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Dos Santos sasa ameingia matatani. Baada ya kuwa mwanamke mwenye utajiri mkubwa kabisa barani Afrika, Isabel dos Santos ameamriwa kuyarudisha mabilioni aliyoyachuma kwa njia za udanganyifu. Gazeti la Süddeutsche linasema maporomoko ya mama huyo yalianza baada ya kufichuliwa kwa siri zake kwenye mitandao maarufu kama ule wa Luanda Leaks.

Gazeti linakumbusha kwamba Isabel dos Santos aliwahi kuuliza kwenye mkutano jee nani ni bingwa wa Afrika? akimaanisha nani anabeba taji la utajiri barani Afrika. Wakati huo alikuwa mwanamke tajiri kuliko wote wengine barani Afrika.

Utajiri wa Isabel dos Santos

Gazeti hilo linafahamisha kwamba uchunguzi uliofanywa ulibainisha kwamba mama huyo alipata utajiri kwa njia ya udanganyifu. Kabla ya uchunguzi gazeti linasema mama huyo alikuwa na utajiri wa dola zaidi ya bilioni tatu. Sasa ameamrishwa arudishe dola milioni 422 kwa kampuni ya nishati ya Ureno Galp. Gazeti linasema kiasi kingine cha fedha cha dola bilioni 1.6 kimo mashakani na uchunguzi bado unaendelea.

Gazeti la Süddeutsche linatilia maanani kwamba hatua zilizochukuliwa dhidi ya Isabel dos Santos ni miongoni mwa mafanikio makubwa ya mahakama katika nchi kadhaa kwa kuweza kuzirejesha fedha zilizoibwa kwa serikali ya Angola. Binti huyo wa rais wa zamani wa Angola alikuwa mwenyekiti wa kampuni ya mafuta na alikuwa mmiliki wa mabenki na kampuni ya bia. Gazeti la SD linasema mama huyo amekanusha madai yote yanayomkabili.Hata hivyo ni wazi kwamba umalkia wake umeanza kufikia mwisho!

Vyanzo:/Deutsche Zeitungen.