1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Rashid Chilumba
13 Agosti 2021

Magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya Afrika kuhusu Sudan kuamua kumkabidhi Omar al Bashir kwa mahakama ya ICC. Uhalifu wa kingono kwenye jimbo la Tigray na pia juu ya uchaguzi mkuu wa Zambia.

https://p.dw.com/p/3ywsN
Sudan Khartum | Prozess & Urteil Omar al-Baschir, ehemaliger Präsident
Picha: picture-alliance/Anadolu Agency/M. Hajaj

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine limeandika juu ya aliyekuwa rais wa Sudan Omar al-Bashir. Gazeti linasema Sudan sasa imeamua kumkabidhi al-Bashir kwa mahakama ya kimataifa ya mjini the Hague, ICC. Waziri wa mambo ya nje wa Sudan amethibitisha habari hizo baada ya  baraza la mawaziri kupitisha uamuzi.

Gazeti linatilia maanani kwamba kiunzi kilichokuwapo hadi sasa ni kwamba Sudan siyo mwanachama wa mfumo wa sheria za Rome. Al-Bashir anatakiwa kujibu mashtaka juu ya mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu kutokana na mgogoro wa jimbo la Darfur mnamo mwaka 2003. Wakati huo wanamgambo na hasa wenye asili ya kiafrika walianzisha harakati za kupinga ukandamizaji wa utawala wa serikali ya Sudan.

Serikali ya al-Bashir ilijibu kwa kutumia ukatili mkubwa uliofanywa na wanamgambo wake wa Janjawid. Kwa mujibu wa taarifa ya Umoja wa Mataifa watu wapatao 300,000 walikufa kutokana na mgogoro huo. Al-Bashir amekanusha madai hayo. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema kesi ya rais huyo wa zamani wa Sudan imesababisha taharuki barani Afrika na kuleta mvutano kati ya Umoja wa Afrika na mahakama ya kimataifa ya mjini the Hague.

Neue Zürcher

Gazeti la Neue Zürcher limeandika juu ya uhalifu wa kingono kwenye jimbo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia. Watafiti wa shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International wamewahoji wanawake 63 waliotendewa uhalifu huo katika jimbo hilo la mgogoro. Watu hao sasa wako kwenye kambi ya wakimbizi nchini Sudan ambako maalfu ya watu wa Tigray wamekimbilia baada ya kuzuka vita.

Gazaeti la Frankfurter Allgemeine linasema wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wamebainisha kuwapo wanawake zaidi ya 500 waliolazwa hospitali kutokana na kubakwa. Linasema waliotenda uhalifu huo ni askari wa jeshi la serikali kuu ya Ethiopia na askari wa Eritrea. Gazeti hilo linafahamisha kwamba shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International linasema vitendo hivyo vinaweza kuwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu. Shirika hilo linatuhumu kwamba uhalifu huo unaendekezwa na serikali za Ehtiopia na Eritrea.

die tageszeitung

die tageszeitung linasema hakuna anayetaka kushindwa katika uchaguzi wa nchini Zambia. Kinyanganyiro hicho ni kati ya rais aliyemo madarakani Edgar Lungu na mshindani wake mkuu, kiongozi wa upinzani Hakainde Hichilema. Gazeti linasema linatilia maanani kwamba Zambia mpaka sasa imekuwa nchi tulivu lakini kutokana na migogoro katika nchi jirani, Zambia nayo inaweza kutumbukia katika vurumai baada ya uchaguzi. Linasema mpinzani wa rais Lungu bwana Hichilema anaelekea kuwa anajitayarisha kwa mvutano  baada ya uchaguzi.

Gazeti hilo linaarifu kwamba kwa mara ya kwanza jeshi la Zambia wiki iliyopita liliwasaidia polisi kuwaandama wapinzani baada ya serikali ya Zambia kutoa madai kwamba wapinzani walikuwa wanavuruga taratibu za uchaguzi. Gazeti hilo linazungumzia juu ya kadhia zinazosababisha wasi wasi juu ya usalama wa Zambia.

Gazeti hilo limenukulu taarifa zinazosema kwamba chama tawala, Patriotic Front cha rais Lungu kimeibambikia silaha na mihadarati sektretariati ya chama cha  UPND ili kukiingiza chama hicho katika matata ya kisheria. Linasema chama tawala kinajaribu kuuzuia upepo wa mabadiliko unaovua nchini Zambia

Neues Deutschland

Gazeti la Neues Deutschland linaturudisha tena nchini Eswatini ambako mfalme wa nchi hiyo Mswati wa 3 anadhibiti mamlaka yote. Vyama vya siasa vimepigwa marufuku nchini humo na wanaharakati wanaotaka mageuzi wananazimwa kwa ukatili wote. Gazaeti la Neues Deutschland linasema vyama vya upinzani vinaitwa kuwa makundi ya magaidi. Wanaharakati na wabunge wanaopigania mageuzi wanatiwa ndani.

Maandamano ya kuwania demokrasia yaliyofanyika mnamo mwezi Juni yalizimwa kwa mabavu ambapo watu zaidi ya 75 walijeruhiwa. Maandamano hayo yaliitishwa baada ya mwanafunzi mmoja kufa wakati akiwa mahabusu. Watu wa Eswatini ambayo hapo awali ilikuwa inaitwa Swaziland waliitikia wito wa wabunge watatu juu ya kupigania mageuzi katika mfumo wa utawala.

Gazeti la Neues Deutschland linasema wananchi waliokuwa na hasira walizishambulia kampuni zinazohusiana na mfalme Mswati wa 3. Gazeti hilo limezinukulu taarifa zinazosema kuwa watu wapatao 697 wameshatiwa ndani mpaka sasa nchini Eswatini. Gazeti linakumbusha kwamba tangu mwaka 1968 Eswatini imo katika mfumo ambapo mfalme anadhibiti mamlaka yote.

Vyanzo:Deutsche Zeitungen