1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
30 Julai 2021

Yaliyoandikwa na magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika wiki hii ni pamoja na kampeni ya kutoa chanjo nchini Dr Congo. Wote sasa wanakwenda Msumbiji na ghasia zilizotokea nchini Afrika Kusini hivi karibuni.

https://p.dw.com/p/3yJsn
DR Kongo Covid-19 Impfung
Picha: Olivia Acland

Süddeutsche

Gazeti la Süddeutsche limeandika juu ya kampeni ya kutoa chanjo dhidi ya Covid-19 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Linasema kampeni hiyo imesimamishwa wakati maambukizi yanaongezeka nchini humo. Gazeti la Süddeutsche linafahamisha kuwa jimbo la Kivu kaskazini ndilo hasa limekumbwa na idadi kubwa ya maambukizi. Linasema vitengo vya maiti vimejaa na kwamba watu wanaokufa wanazikwa haraka.

Gazeti hilo linaarifu kwamba watu zaidi ya 48 wameambukizwa virusi vya corona nchini Kongo na mpaka sasa waliokufa ni watu zaidi ya 1000. Süddeutsche linasema mlipuko wa volkano wa hivi karibuni katika eneo la Nyiragongo mkoani Goma pia umechangia katika kuongeza maambukizi.

Gazeti la Süddeutsche linaeleza kwamba kampeni ya kutoa chanjo imesimamishwa nchini Kongo kwa sababu chanjo za AstraZeneca zilizotolewa chini ya mpango wa Umoja wa Mataifa zimeteketezwa kutokana na  kuwapo mashaka juu ya dawa hizo. Mwanaharakati wa Kongo Passy Mubalama amesema hajariridhishwa na kampeni nzima ya chanjo nchini mwake.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung linasema wote sasa wanakwenda Msumbiji, majeshi ya Rwanda, yale ya nchi za jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika na sasa wakufunzi wa kijeshi kutoka Umoja wa Ulaya. die tageszeitung linasema mfungamano wa kimataifa dhidi ya magaidi unashamiri. Majeshi hayo yataungana na wakufunzi kutoka Ureno ambao tayari wako nchini Msumbiji siku nyingi. die tageszeitung linatilia maanani kwamba wanajeshi wa Rwanda ndiyo wanaotimiza jukumu muhimu. Linasema rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alikamilisha mipango ya kupelekwa Msumbiji kwa askari wa Rwanda wakati wa ziara yake nchi humo.

Gazeti hilo linatuhumu kwamba Ufaransa inayafadhili majeshi hayo ili kulinda maslahi yake kwenye jimbo la Cabo Delgado la kaskazini mwa Msumbiji ambako kampuni ya mafuta ya nchi hiyo, Total imewekeza katika mradi wa gesi wa thamani ya dola bilioni 24. Jimbo hilo lilishambuliwa na waasi mnamo mwezi Machi. die tageszeitung limemnukulu mataalamu wa mtandao wa ulinzi wa Afrika kusini akisema kuwa kilichoanza kama uasi wa ndani ya Msumbiji sasa kimegeuka kuwa mgogoro wa kimataifa unaozihusisha pande kadhaa.

Neue Zürcher Zeitung

Nalo gazeti la Neue Zürcher linazungumzia ghasia zilizotokea nchini Afrika Kusini hivi karibuni. Linasema vitendo vya uporaji kwenye maduka vinadhihirisha udhaifu wa polisi nchini humo. Linasema pana sababu za kihistoria kwa nini polisi walisuasua kuchukua hatua. Linakumbusha kwamba mnamo mwaka 2012 polisi waliwapiga risasi na kuwaua wafanyakazi 34 kwenye mgodi wa Marikana. Gazeti la Neue Zürcher linaeleza kwamba tangu wakati huo polisi nchini Afrika Kusini wanatakiwa wawe waangalifu sana katika matumizi ya silaha. Pia limemnukulu mchambuzi mmoja akisema kwamba wanaoajiriwa kuwa polisi ni wale wanaokitii chama tawala cha ANC. Vigezo vya polisi siyo muhimu.

Frankfurter Allgemeine

Tunakamilisha kwa makala ya gazeti la Frankfurter Allgemeine linalokumbusha historia ya siasa ya ujamaa nchini Tanzanzia. Makala hiyo imeandikwa na mtaalamu wa historia anayeuliza iwapo ubepari unaweza kuujenga usoshalisti kwa kuutumia mfano wa Tanzania. Mtaalamu huyo anasema ushirikiano na nchi za Afrika  katika kuleta maendeleo baada ya nchi hizo kuanza kujitawala ulikuwa sawa na nyanja zingine za siasa. Kwa sababu ushirikiano huo ulitegemea mashindano kati ya mataifa makubwa ya dunia ya mashariki na magharibi. Mtaalamu huyo Eric Burton anaeleza katika makala yake kwamba matokeo ya ushirikiano huo hayakuwa mazuri wakati wote.

Katika makala hiyo aliyoandika kwenye gazeti la Frankfurter Allgemeine, Burton ametumia ruwaza ya Tanzania iliyokuwa inafuata siasa ya ujamaa na kujitegemea, sera iliyojulikana kama usoshalisti wa kiafrika. Ameangalia uhusiano baina ya Tanzania na nchi mbili za Ujerumani ya magharibi na Ujerumani mashariki iliyokuwa inaitwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Ujerumani iliyofuata siasa ya usoshalisti.

Mwandishi huyo anakumbusha kwamba Tanzania ilipokea misaada kutoka kwa nchi za kisoshalisti na za kibepari za magharibi. Hata hivyo baada ya hayati rais Julius Nyerere kutangaza azimio la Arusha, Marekani, Ujerumani Magharibi na Uingereza zilisimamisha misaada ya maendeleo kwa miaka kadhaa. Ushirikiano kati ya Tanzania na nchi za magharibi na mashariki ilipitia awamu mbalimbali. Lakini Burton anasema katika makala yake kuwa matokeo yake ni kwamba Tanzania ilijenga utegemezi na ilijilundikia madeni badala ya kujitegemea.

Vyanzo:/Deutsche Zeitungen