1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Gakuba, Daniel
12 Februari 2021

Yaliyozingatiwa kwenye magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika ni pamoja na hukumu ya mahakama ya ICC dhidi ya Dominic Ongwen na pia kuhusu Ngozi Okonjo Iweala anayewania wadhifa wa mkurugenzi wa shirika la biashara WTO.

https://p.dw.com/p/3pGRC
Niederlande | Prozess Dominic Ongwen | Internationaler Strafgerichtshof in Den Haag
Picha: ICC-CPI/REUTERS

 die tageszeitung 

Gazeti la die tageszeitung limeandika kuhusu mahakama ya kimataifa ya mjini the Hague, ICC ambayo imemhukumu Dominic Ongwen aliyekuwa kiongozi wa waasi wa Uganda baada ya kupatikana na hatia ya kutenda uhalifu wa kivita na dhidi ya binadamu.

Ongwen mwenye umri wa miaka 46 alipatikana na hatia ya ubakaji na mauaji ya kikatili. Gazeti la die tageszeitung linasema wakati bado alipokuwa na umri wa miaka 30 Ongwen alitenda uhalifu mara 70 kaskazini mwa Uganda mnamo mwaka 2004. Adhabu yake bado haijajulikana lakini anaweza kula kifungo cha miaka 30 jela.

Gazeti la die tageszeitung linatilia maanani kwamba hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa kundi la Lords Resistance Army kufikishwa mbele ya mahakama ya kimataifa ya mjini the Hague na kuhukumiwa. Hata hivyo gazeti hilo linaeleza kuwa Ongwen alikuwa mhalifu na mhanga wakati mmoja kwa sababu yeye pia alitekwa nyara alipokuwa mtoto na kuingizwa katika kundi hilo la LRA.

Gazeti linakumbusha kwamba baada ya kuwa kamanda wa kikosi, Ongwen, aliwaamrisha watu wake kukivamia kijiji cha Lukodi, kaskazini mwa Uganda. Wanakijiji waliswekwa ndani ya vibanda na kuchomwa moto mnamo mwaka 2004. Kundi la LRA liliendesha mapambano ya kikatili dhidi ya serikali ya Uganda kuanzia kati kati ya miaka ya 80 lakini hasa lilifanya ukaliti mkubwa kwa raia.

Handelsblatt,

Gazeti la Handelsblatt linazungumzia juu ya bibi Ngozi Okonjo Iweala, mnaigeria anayewania wadhifa wa mkurugenzi wa shirika la biashara duniani WTO. Gazeti hilo linasema mama huyo anayetarajiwa kuwa mwafrika wa kwanza na mwanamke kuiongoza WTO anasubiriwa na migogoro mingi ya biashara atakapoingia katika wadhifa huo.

Handelsblatt linasema enzi mpya zitapambazuka kwenye shirika hilo la biashara kutokana na ujio wa mama huyo ambaye pia ana uraia wa Marekani. Linasema hii ni mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa  shirika hilo mnamo mwaka 1995 kwa mwanamke kushika hatamu zake. Hata hivyo gazeti linatilia maanani kwamba mama huyo mwenye umri wa miaka 66 atakabiliwa na changamoto chungutele. Pia linatilia maanani kwamba njia ya mama huyo kuelekea kwenye wadhifa wa mkurugenzi wa shirika la WTO imefunguka baada ya rais Joe Biden kuingia madarakani nchini Marekani kwani utawala wa hapo awali wa Donald Trump ulimwekea mama huyo kigingi. Donald Trump alikuwa anampigia debe mjumbe wa Korea ya Kusini, Yoo Myung waziri wa biashara wa nchi hiyo.

Süddeutsche Zeitung    

Gazeti la Süddeutsche linazungumzia juu ya mgogoro kati ya Ethiopia, Misri na Sudan kuhusu bwawa kubwa la umeme kwenye mto Nile. Gazeti hilo limemnukulu waziri wa maji wa Sudan Yasir Abbas akisema kwamba mambo hayawezi kuendelea hivyo daima. Mazungumzo juu ya mradi huo kabambe wa Ethiopia yamekuwa yanafanyika kwa takriban mwongo mmoja na mpaka sasa hakuna hatua iliyopigwa.

Gazeti la Süddeutsche linaeleza kwamba mazungumzo hayo yanahusu njia ya kugawana maji kwa manufaa ya nchi zote. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba mgogoro huo umesababisha vitisho kutoka kila upande. Linasema hivi karibuni Misri ilitishia kulipiga mabomu bwawa hilo wakati Ethiopia imetishia kuendelea kulijaza maji bwana hilo bila ya makubaliano.

Mzizi wa fitina

Gazeti la Süddeutsche linaeleza kuwa mzizi wa fitina unahusu kiasi cha maji ambacho Ethiopia itaruhusu kupanda juu hadi Misri. Linasema matumaini ya kufikiwa mapatano yamezidi kudidimia kwa sababu Sudan nayo imeubadilisha msimamo wake baada ya kuwa nchi pekee ya kuaminika kwenye mazungumzo hayo. Hapo awali Sudan ilitaka ujumbe wa Umoja wa Afrika ushiriki kwenye mazungumzo lakini sasa imeubadilisha msimamo huo na kusababisha mazungumzo yakwame.

Mradi mkubwa wa bwana la Ethiopia ulipaswa kukamilika mnamo mwaka 2017 lakini haikuwezekana kutokana na matatizo ya kiufundi na ufisadi. Hata hivyo Ethiopia imetangaza kwamba itaanza awamu ya pili ya kujaza maji kwenye bwawa hio bila ya kujali maslahi ya jirani zake.

die tageszeitung,

Makala nyingine ya gazeti la die tageszeitung inazungumzia juu ya hali ya maambukizi ya virusi vya corona nchini Afrika Kusini baada ya kubainika kwamba chanjo ya AstraZeneca haina ufanisi uliotarajiwa. Kulingana na uchunguzi wa hivi karibuni chanjo ya AstraZeneca inafikia ufanisi wa asilimia 22 tu!

Gazeti la die tageszeitung linaeleza kuwa Serikali ya Afrika Kusini ilikuwa na matarajio makubwa juu ya chanjo hiyo na kuwa mfano barani Afrika kote lakini mpango wa kutoa chanjo hizo sasa umesimamishwa. Watu zaidi ya 46,000 wameshakufa nchini Afrika Kusini kutokana na maambukizi ya virusi vya corona. Gazeti la die tageszetung linaarifu kwamba baadhi ya makanisa yamewataka waumini wao waamini zaidi sala na maombi badala ya dawa za kikemia.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen