Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Matukio ya Afrika | DW | 05.02.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Ujerumani

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Yaliyozingatiwa katika magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika wiki hii ni pamoja na hofu ya kuzuka baa la njaa nchini Ethiopia. Afrika Kusini yapokea shehena ya kwanza ya chanjo za COVID-19.

Neue Zürcher

Gazeti la Neue Zürcher juu ya hali ya jimbo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia. Gazeti hilo linasema kuna hatari ya jimbo hilo kukumbwa na baa la njaa. Neue Zürcher linasema hali imekuwa mbaya kiasi kwamba janga lililotokea mnamo miaka ya 80 huenda likarejea tena nchini Ethiopia. Watu zaidi ya milioni moja walikufa njaa wakati huo. Gazeti hilo linasema ni vigumu kujua kwa uhakika yale yanayotokea kwenye jimbo la Tigray lakini imethibitika kuwa thuluthi moja ya watu wa jimbo hilo wamegeuka kuwa wakimbizi wa ndani. Watigray wapatao 60,000 wamekimbilia katika nchi jirani ya Sudan na maalfu wengine wameuliwa.

Mwakilishi wa serikali kuu ya Ethiopia kwenye jimbo la Tigray amesema ikiwa misaada ya lazima haitafika  kwa haraka, maalfu ya watu watakufa njaa katika jimbo hilo. Gazeti la Neue Zürcher limemnukulu kamishna wa wakimbizi wa Umoja wa Mataifa Filippo Grandi akisema kwamba hali ni ya kutisha kwenye jimbo la Tigray.

Süddeutsche

Gazeti la Süddeutsche limeandika juu ya wasaa wa faraja nchini Afrika Kusini. Rais Cyril Ramaphosa, makamu wake pamoja na waziri wa afya mapema wiki hii wamepokea shehena ya chanjo za COVID-19. Hata hivyo gazeti hilo linasema mzigo huo wa vichupa laki tano vya chanjo ni kidogo mno. Hiyo ni shehena ya kwanza ya dawa hizo kusini mwa janga la Sahara.

Süddeutsche linaarifu kwamba walioko mstari wa mbele katika harakati za kupambana na janga la corona ndiyo watakaopewa kipaumbele katika kupatiwa chanjo. Gazeti linasema Afrika Kusini imeagiza kiasi hicho kidogo kutokana na uhaba wa fedha. Afrika kusini imesimama njia panda kwa kuwa nchi hiyo inazingatiwa kuwa inajiweza kifedha, na kwa hivyo haistahiki kupatiwa chanjo bure lakini katika upande mwingine haina fedha za kutosha kulinganisha na nchi za Ulaya au Marekani ili kuweza kuagiza kiasi kikubwa cha chanjo.

Maalfu ya watu nchini Afrika Kusini walifanyiwa majaribio ili kubainisha ufanisi wa dawa hizo. Hata hivyo gazeti limemnkulu rais Ramaphosa akilalamika kwamba nchi tajiri zimejimbilikizia chanjo hizo mara nne zaidi ya mahitaji yao. Gazeti la Südedeutsche linatilia maanani kwamba Afrika Kusini inanunua dawa hizo kwa bei kubwa zaidi.

Neue Zürcher

Habari nyingine zilizoandikwa kwenye gazeti la Neue Zürcher ni juu ya watoto nchini Kenya ambao wamerejea shuleni baada ya kukaaa nyumbani kwa muda wa miezi tisa katika juhudi za kuepuka maambukizi ya virusi vya corona. Gazeti la Neue Zürcher limeikariri wizara ya elimu nchini Kenya ikieleza kwamba yapo manufaa makubwa kwa watoto kurejea masomoni na kwamba katika nchi inayoendelea kama Kenya kwenda shule kunaleta faida zaidi ya masomo kwa sababu watoto pia hupata chakula.

Gazeti la Neue Zürcher linasema Kulingana na uchunguzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la watoto na elimu, kufungwa kwa shule kulimaanisha pia kuongezeka kwa umasikini, utapiamlo na maradhi miongoni mwa watoto. Linasema walimu nchini Kenya wamefurahi kuwaona watoto wakirejea shuleni.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung linaingalia hukumu iliyotolewa dhidi ya kampuni ya Royal Dutch Shell kwa  sababu mbili, kwanza ni onyo kwa makampuni makubwa duniani yanayojihusisha na shughuli  zinazoharibu mazingira duniani kote na pili gazeti hilo limeelezea masikitiko kwamba imechukua muda mrefu kuitoa hukumu hiyo kwani baadhi ya waathiriwa hawapo hai.

Baada ya kesi kufanyika kwa muda wa miaka 13, Mahakama ya mjini the Hague ya nchini Uholanzi imeiamuru kampuni hiyo kuwalipa fidia wakulima wa Nigeria kutokana na mazingira yao kuathirika na shughuli ua uchimbaji wa mafuta kwenye eneo la Niger Delta. die tageszeitung limemnukulu wakili wa Nigeria Eric Dooh akisema uamuzi uliotolewa dhidi ya kampuni ya uholanzi ya Royal Dutch Shell umeleta matumaini kwa watu wa jimbo la Nigeria la Niger Delta kwa sababu kampuni hiyo imeamriwa kuyasafisha mazingira yaliyochafua ardhi ya wakulima wa jimbo hilo.

Gazeti la die tageszeitung limemunukulu mkurugenzi wa shirika la ulinzi wa mazingira bwana Donald Pols akisema kuwa hukumu hiyo imeonyesha kuwa watu wanaodhulumiwa kutokana na mazingira yao kuharibiwa au kutokana na ardhi zao kuporwa wanaweza kuwa na matumaini ya kupigania haki zao na kushinda.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen

 

 

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com