Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Matukio ya Afrika | DW | 20.11.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Ujerumani

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Yaliyoandikwa kwenye magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika wiki hii ni pamoja na uhusiano baina ya bara la Afrika na Marekani baada ya Joe Biden kushinda uchaguzi, juu ya mgogoro wa nchini Ethiopia na mengineyo.

Frankfurter Allgemeine

Na tunaanza moja kwa moja na gazeti la Frankfurter Allgemeine. Gazeti hilo linazungumzia juu ya uhusiano baina ya bara la Afrika na Marekani baada ya Joe Biden kushinda uchaguzi. Linakumbusha kwamba utawala wa hapo awali wa Donald Trump haukulitilia maanani bara hilo. Frankfurter Allgemeine linasema ingawa watu hawakujitokeza barabarani kuushangilia ushindi wa Biden, kama walivyofanya, Obama aliposhinda, viashiria vimebainika.

Gazeti hilo linafahamisha kwamba soko la hisa la Johannesburg, nchini Afrika Kusini lilipanda..Gazeti linasema matumaini yapo juu ya kurejeshwa uhusiano mzuri kati ya Marekani na bara la Afrika baada ya ushindi wa Joe Biden. Hata hivyo linatahadharisha kwa kuwanukulu wataalamu wa masuala ya kiuchumi wanaosema, mabadiliko yanayotarajiwa katika uhusiano huo hayatafanyika kwa haraka.

Gazeti linasema Biden atatingwa na masuala  ya ndani ya Marekani kwanza. Hata hivyo linasema jambo muhimu katika uhusiano wa Marekani na bara la Afrika ni mkataba wa biashara huru AGOA ulioanzishwa na rais wa hapo awali Bill Clinton unaoziruhusu nchi za Afrika kuuza bidhaa kwenye soko la Marekani bila ya kutozwa ushuru. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linatumai kwamba chini ya utawala wa Joe Biden mkataba huo utaendelezwa.

Neues Deutschland

Gazeti la Neues Deutschland linazungumzia juu ya mgogoro wa nchini Ethiopia. Linasema waziri mkuu wa nchi hiyo, Abiy Ahmed hana tena muda wa kusubiri katika juhudi za kuleta maridhiano baada ya vita  kufumuka kati ya serikali kuu anayoiongoza na ya jimbo la kaskazini la Tigray. Waziri mkuu Abiy Ahmed alipeleka majeshi kulishambulia jimbo hilo baada ya kituo cha jeshi la serikali kuu kushambuliwa mnamo mwezi wa Novemba. Gazeti la Neues Deutschland linaeleza kwamba kadhia hiyo ilitokea baada ya jimbo la Tigray kufanya uchaguzi licha ya katazo la serikali kuu kutokana na hatari ya maambukizi ya virusi vya corona.

Gazeti linasema mgogoro wa kivita ulianza hapo lakini linaeleza kwamba mvutano baina ya serikali kuu ya Ethiopia na jimbo la Tigray una mizizi mirefu ya kikabila. Neues Deutschland linatilia maanani kwamba kila kabila linaweka maslahi ya watu wake mbele nchini Ethiopia. Gazeti linaeleza kwamba alipoingia madarakani mnamo mwaka 2018 waziri mkuu Abiy Ahmed alilenga shabaha ya kuondosha itikadi hiyo na badala yake kuleta umoja wa kitaifa. Baadhi ya viongozi wa jimbo la Tigray hawakubaliani na sera hiyo ya kitaifa.

Gazeti la Neues Deutschland linasema haieleweki iwapo viongozi wa jimbo la Tigray wanataka mamlaka zaidi ya ndani au nia yao ni kumhujumu waziri mkuu Abiy Ahmed? Ni maoni ya gazeti hilo kwamba viongozi wa jimbo la Tigray wanataka kumwambia waziri mkuu huyo kwamba hataweza kuileta Ethiopia pamoja.     

Neuer Zürcher:

Gazeti la Neuer Zürcher limeandika juu ya mauaji yanayofanywa na magaidi wenye itikali kali ya kiislamu nchini Burkina Faso. Linasema magaidi hao wanazishambulia taasisi zote zinazowakilisha utamaduni wa magharibi na ndiyo sababu wameshambulia shule na kuwaua walimu kadhaa. Gazeti hilo linaeleza kuwa magaidi hao wanafanya mashambulio kwenye nchi za ukanda wa Sahel. Wameshambulia nchini Burkina Faso kuonyesha msimamo wa kupinga ujiingizaji kijeshi wa Ufaransa katika nchi za Sahel. Gazeti la Neuer Zürcher linakumbusha juu ya wito uliotolewa na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wa kuimarisha mapambano dhidi ya magaidi kwenye eneo la Sahel.

Hata hivyo gazeti hilo linatilia maanani kwamba licha ya asilimia 60 ya watu nchini Burkina Faso kuwa waislamu, uwakilishi wao katika sekta ya kijamii ni mdogo. Gazeti linasema hali hiyo inatokana na enzi za ukoloni ambapo waliopata elimu ya juu walitoka kwenye shule za wamishonari. Neuer Zürcher linasema serikali imetambua ulazima wa kufanya mageuzi katika mfumo  wa elimu ili kuzingatia mahitaji ya jamii na ya vijana.     

die tageszeitung

Gazeti la die Tageszeitung linatupeleka Nairobi ambako wakaazi wa mtaa mmoja wa mabanda wanaota ndoto ya kuwa na nyumba zenye vyoo vya ndani. Gazeti hilo linatupa mchapo juu ya Lidia Mwikali mama mmoja anayeishi kwenye kitongoji cha Mathare ambaye hajawahi kuishi ndani ya nyumba yenye vyoo vya ndani. Gazeti la die tageszeitung linasema hiyo ndiyo ndoto yake. Mama huyo anaishi katika nyumba ndogo pamoja na mumewe na watoto wawili.

Die tageszeitung linatufahamisha kwamba kwa sasa mama huyo na familia yake wanatumia vyoo vya nje ambapo wanapaswa kulipa. Mwikali amesomea kazi ya ukatibu lakini kwa sasa hana ajira kutokana na janga la corona. Gazeti la die tageszeitung linasema mama huyo anahofia huenda ndoto yake ya kumiliki nyumba yenye vyoo ndani ikabakia kuwa ndoto tu. Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa mataifa zilizokaririwa na gazeti hilo, asilimia 70 ya watu milioni 50 nchini Kenya hawapati huduma ya vyoo safi. 

Vyanzo:Deutsche Zeitungen