1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
21 Agosti 2020

Mapinduzi ya kijeshi nchini Mali ni mada mojawapo iliyoandikwa kwenye magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika wiki hii

https://p.dw.com/p/3hJOk
Mali Kati PK Putsch Anführer Ismael Wague
Picha: Getty Images/AFP/A. Risemberg

Neue Zürcher

Gazeti za Neue Zürcher limeandika juu ya hali ya nchini Mali. Gazeti hilo linasema walichokifanya wanajeshi nchini humo siyo kitendo cha kidemokrasia hata kidogo. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba hatua ya wanajeshi wa Mali kutwaa madaraka siyo jambo sahihi. Neue Zürcher linakumbusha kwamba nchi za jumuiya ya kiuchumi ya Afrika magharibi ECOWAS zinasisitiza kwamba rais Ibrahim Boubacar Keita alichaguliwa kwa njia ya kidemokrasia na linatilia maanani kwamba pana wasiwasi, huenda hali hiyo ya nchini Mali ikaendelea katika nchi za jirani. Gazeti la Neue Zürcher linasema serikali ya rais Ibrahim Boubacar imepinduliwa kutokana na makosa yake yenyewe. Hata hivyo gazeti hilo linasema ni muhimu sasa kuhakikisha kwamba walioipindua serikali wanayatekeleza yote waliyoahidi.

Süddeutsche

Gazeti la Süddeutsche limeandika juu ya José Filomeno de Sousa dos Santos mtoto wa aliyekuwa rais wa Angola José Eduardo dos Santos. Gazeti la Süddeutsche linasema imethibitishwa kwamba Filomeno dos Santos aliiba dola milioni 500 na kuziweka katika benki ya Credit Suisse nchini Uingreza. Fedha hizo zilikuwa za mfuko wa serikali.

Gazeti la Süddeutsche linakumbusha kwamba fedha hizo zilikusudiwa kwa ajiili ya siku za usoni lakini ziliingia katika mifuko ya watu binafsi. Gazeti la Süddeutsche linasema baada ya rais wa hapo awali Dos Santos yaani baba yake Filomeno kuondoka madarakani mnamo mwaka 2017 rais aliyefuatia, Joao Lourenco aliingia madarakani na kampeni ya kupambana na ufisadi.

Mahahama imemuhukumu Filomeno Dos Santos adhabu ya kifungo cha miaka mitano jela kwa kosa la ufisadi baada ya kupatikana na hatia ya kupeleka dola milioni 500 kwenye benki ya Uingereza. Fedha hizo zilitolewa kwenye benki ya Angola na kupelekwa nchi ya nje.

Der Tagespiegel

Gazeti la Der Tagespiegel linazungumzia juu ya maambukizi ya virusi vya corona barani Afrika. Gazeti hilo linasema tofauti na utabiri wa hapo awali ni waafrika wapatao milioni moja tu walioambukizwa virusi vya corona. Gazeti la Der Tagespiegel linakumbusha kwamba hapo awali mashirika ya kimataifa mengi tu yalitabiri vifo vya mamilioni ya waafrika kutokana na virusi hivyo lakini mpaka sasa katika bara hilo lenye watu wapatao bilioni 1.2 ni watu milioni moja na laki moja walioambukizwa virusi vya corona. Gazeti hilo linasema tofauti na sehemu nyingine za dunia idadi ya watu walioambuklizwa virusi vya corona barani Afrika ni ndogo sana.

Berliner Zeitung

Nalo gazeti la Berliner linazumgumzia juu ya mradi wa ujenzi wa nyumba za makao nchini Uganda. Kwa kutumia maganda ya punje za mpunga. Gazeti hilo linazungumia juu ya mjerumani mmoja, Eckardt Dauck kutoka Berlin anayeamini kwamba amegundua njia ya kuwasaidia watu nchini Uganda. Hata hivyo gazeti linamwambia Dauck kwamba njia hiyo imetumika miaka yote barani Afrika. Gazeti hilo limemwambia bwana Dauck kwamba baadhi ya waafrika wamekuwa wanajenga nyumba zao kwa kutumia chuya tangu karne nyingi zilizopita. Hata hivyo gazeti la Berliner linasema Dauck anaota ndoto nzuri juu ya kuwasaidia watu wengine.

die tageszeitung

Makala ya gazeti la die tageszeitung inazungumzia juu ya biashara ya dhahabu nchini Kongo inayozijumuisha nchi za jirani ikiwa pamoja na Uganda. Kwa mujiibu wa gazeti hilo nchi hiyo imegeuka kituo cha biashara ya dhahabu. Hata hivyo gazeti la die Tageszeitung linasema biashara hiyo inawavutia majenerali, askari na wanamgambo wa makundi mbalimbali mashariki mwa Kongo. Gazeti la die Tageszeitung linasema wakati inapasa kufahamika kwamba ndege zinazoondoka Uganda zilipaswa kuwa na mizigo ya matunda na maua, polisi waligundua hivi karibuni kwamba dhahabu ilikuwamo ndani ya mizigo.

Gazeti la die Tageszeitung linasema maafisa kwenye uwanja wa ndege walishangazwa na kile walichokiona. Die Tageszeitung linasema watu zaidi ya robo milioni wanafanya kazi ya kusafisha mchanga wa dhahabu. Wanafanya kazi hiyo kwa kutumia vifaa duni lakini gazeti hilo linasema wanaonufaika ni wengine katika ngazi mbalimbali.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen