1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Iddi Ssessanga
10 Julai 2020

Baadhi ya mambo yaliyozingatiwa kwenye makala za magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika ni pamoja na sera ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed inavyokabiliwa na upinzani mkubwa.

https://p.dw.com/p/3f69X
Dr. Abiy Ahmed
Picha: DW/S. Teshome

Neuer Zürcher

Gazeti la Neue Zürcher limeandika juu ya hali inayoendelea nchini Ethiopia. Linauliza jee juhudi za kuleta mageuzi nchini humo zilizofanywa na Waziri Mkuu Abiy Ahmed zilikuwa nguvu za soda? Gazeti hilo linasema sera ya mageuzi ya waziri mkuu huyo sasa inakabiliwa na upinzani mkubwa hasa kutoka kwa watu wa kabila lake la Oromo.

Gazeti hilo linaeleza kwamba mpaka sasa watu zaidi ya 160 wameuawa kutokana na ghasia miongoni mwao polisi kadhaa. Gazeti la Neue Zürcher linatilia maanani kwamba mara baada ya kuingia madarakani mnamo mwaka 2018 Waziri Mkuu Abiy Ahmed alianzisha mchakato wa kuleta demokrasia ambapo alizipa serikali za majimbo mamlaka makubwa zaidi. Alitoa msamaha kwa viongozi wa makabila na kuwaruhusu kurejea nchini Ethiopia. Hata hivyo gazeti linasema kurejea kwa viongozi hao kumechochea siasa za kujitenga. Kutokana na hali hiyo Abiy sasa analazimika kutawala kwa ukali.

Süddeutsche Zeitung

Gazeti la Süddetsche linauliza iwapo nchi za Afrika zinaambulia makombo tu, wakati nchi tajiri zinanunua vitendea kazi vyote vinavyohitajika kwa ajili ya kupambana na janga la maambukizi ya corona? Gazeti hilo linatoa mfano wa nchini Afrika Kusini ambapo idadi ya maabukizi inaongezeka. Süddeutsche linaeleza kwamba maalfu ya watu nchini humo walipimwa katika wiki zilizopita lakini kutokana na uhaba wa vitendea kazi majibu ya vipimo yanachukua muda wa hadi wiki mbili kutolewa. Katika muda huo wale wenye maambukizi wanaendelea kuwaambukiza wengine.

Gazeti hilo limemnukulu Profesa wa magonjwa ya kuambukiza kutoka chuo kikuu cha Stellenbosch akisema nchi za Afrika zinasimama mwisho kwenye foleni yakupata vifaa vya kupimia maambukizi ya corona. Gazeti la Süddeutsche linasema kampuni zinazotengeneza vifaa vya kupimia zinapeleka vifaa hivyo kule kunakoungua zaidi.

Gazeti hilo limemnukulu mkuu wa kituo cha kudhibiti magonjwa barani Afrika John Nkengasong akisema lingekuwa jambo la manufaa endapo kampuni husika zingelikuwa zinatengeneza vifaa vyote kwa pamoja vinavyohitajika kwa ajili ya kupambana na jangoa la corona. Hata hivyo gazeti hilo linatilia maanani kwamba bei ya vifaa hivyo ni ya juu sana kwa nchi nyingi zinazoendelea.

Neues Deutschland

Gazeti la Neues Deutschland linasema janga la corona linasababisha madhara mengine makubwa, mbali na maradhi tu. Gazeti hilo limeikariri ripoti ya shirika la misaada ya chakula "Welthungerhilfe" inayotahadharisha juu ya hatari ya kuongezeka idadi ya watu wasiopata chakula cha kutosha duniani kote. Katika ripoti yake shirika hilo linasema ukanda wa Afrika Mashariki unakabiliwa na majanga manne ambayo ni Ukame, mafuriko, nzige na maambukizi ya corona.

Shirika la misaada ya chakula "Welthungerhilfe" linasema hatua za karantini zimezidisha utapia mlo katika eneo la Afrika Mashariki, hadi Sudan Kusini. Kulingana na makadirio ya shirika hilo gazeti la Neues limekariri, watu wapatao milioni 270 wataongezeka miongoni mwa wale waliomo katika hatari ya kufa njaa, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linaarifu kwamba serikali ya Zimbabwe inatumia kisingizio cha corona ili kuwaandama wapinzani. Kwa mujibu wa gazeti hilo wabunge watatu wanawake wa chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change, MDC, walikamatwa na kuwekwa mahabusu kwa muda wiki mbili kwenye jela ya mjini Harare. Kabla ya hapo, gazeti linaseama wabunge hao walikuwa wametekwa nyara. Frankfurter Allgemeine linaeleza kuwa wanawake hao baadae walikutwa wametelekezwa barabarani wakiwa wamejeruhiwa.

Gazeti hilo limemnukulu mmoja wa wabunge hao Joana Mamombe akitoa madai ya kubakwa, kupigwa na kudhalilishwa. Kwa mujibu wa mbunge huyo, wanawake hao walisimamishwa, na polisi kwenye kituo cha ukaguzi, walipokuwa wanatoka kushiriki kwenye maandamano ya kupinga hatua za karantini.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema watu waliowateka nyara wabunge hao hawajakamatwa mpaka leo. Hata hivyo waziri wa  mambo ya ndani wa Zimbabwe Kazembe Kazembe amesema wabunge  hao walitunga hadhithi hiyo  ya kutekwa nyara na kwamba walikamtwa kwa sababu ya kukiuka taratibu za karantini.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen