Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 20.09.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Ujerumani

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Yaliyozingatiwa kwenye magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika ni pamoja na kuuliwa kwa kamanda wa jeshi la mgambo la waasi wa Kihutu, (FDLR) Sylvestre Mudacumura huko nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung limeandika kuwa Sylvestre Mudacumura aliuliwa siku ya Jumatano iliyopita kwenye msitu wa Nyanzale, jimbo la Kivu kaskazini katika operesheni ya kijeshi ya pamoja baina ya askari wa Rwanda na Kongo. Gazeti la die tageszeitung linasema, Sylvestre Mudacumura aliyekuwa mhalifu mkubwa wa kivita alikuwa anasakwa na mahakama ya kimataifa ya mjini The Hague (ICC). Tangu mwaka 2012.

Kuuliwa kwa mhalifu huyo wa kivita ni hatua muhimu katika harakati za kupambana na waasi ambao kwa muda wa miaka mingi wamekuwa wanatenda ukatili mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo. Gazeti la die tageszeitung linatufahamisha kwamba miongoni mwa viongozi wa kundi la waasi la FDLR wapo wale walioshiriki katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda. Waasi hao walikimbilia katika nchi jirani ya Kongo baada ya mauaji hayo ya halaiki.

Die Welt

Gazeti la Die Welt linatupeleka Sudan ambako aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Omar al- Bashir amefunguliwa mashtaka lakini gazeti hilo lina mashaka iwapo kesi hiyo ni ya dhati, na linaeleza kwamba Bashir bado ana wafuasi. Watu hao husimama kwenye ukumbi wa mahakama na kumsalimu kwa kuonyesha heshima kubwa. Wanawake pia wanamwonyesha ishara ya kumbusu na hayo yote yanaonekana kwenye televesheni. Lengo ni kusema kwamba bado anapendwa. Bashir aliyeondolewa madarakani na wanajeshi wenzake anakabiliwa na mashtaka ya ufisadi lakini mashtaka hayo hayahusu uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu alioutenda.

Gazeti la Die Welt linaeleza kwamba mahakama inaepuka kumfungulia Bashir mashtaka dhidi ya uhalifu wa kivita kwa sababu ya kuhofia kutifua vurumai na linaendelea kusema kwamba kesi inayomkabili Omar al-Bashir kwa makusudi itachukua muda mrefu mahakamani, kwa  matumaini kwamba hali itakuwa imetulia zaidi kabla ya hukumu kotolewa. Pia ni vigumu kuamini iwapo Bashir atapelekwa mjini the Hague kujibu mashtaka ya kutenda uhalifu wa kivita ambapo inadaiwa alihusika  na mauaji ya watu 300,000 katika jimbo la Darfur, magharibi mwa Sudan. Gazeti la Die Welt linasema jinsi kesi dhidi ya Bashir inavyofanyika inaonyesha namna dikteta huyo alivyoitawala Sudan. Bashir bado ana wafuasi.

Weser-Kurier

Nalo gazeti la Weser-Kurier limeandika juu ya watu wanaoishi nchini Afrika Kusini kutoka nchi nyingine za Afrika. Wengi miongoni mwao wameamua kurejea kwenye nchi zao baada ya ghasia zilizotokea hivi karibuni. Gazeti hilo la Weser-Kurier limewanukulu baadhi ya waafrika hao wakisema hawataendelea kutafuta maisha bora mahala, ambapo wanaweza kuuliwa na kwa hivyo ni bora kurudi nyumbani.

Kwa muda wa miaka zaidi ya 20 waafrika hao, wamekuwa wanaishi nchini Afrika Kusini lakini matumaini waliyokuwa nayo yamegeuka kuwa jinamizi. Wageni kutoka Msumbiji, Zimbabwe na Nigeria wamesema maji yamewafika kwenye kilemba. Hakuna njia nyingine ila kuondoka Afrika Kusini.

Gazeti  la Weser-Kurier linaeleza kuwa magenge yanayowashambulia waafrika kutoka nchi nyingine yanadai kuwa waafrika hao ni wahalifu na wanachukua nafasi za ajira za wazawa. Gazeti hilo linauliza: Jee mpango wa demokrasia wa mwaka 1994 umesambaratika nchini Afrika kusini? Linajibu swali hilo kwa kueleza kwamba tofauti na hali iliyokuwapo chini ya mfumo wa ubaguzi wa rangi, kwa jumla watu wanaishi kwa amani kwenye mitaa ya Afrika Kusini. Na hata katika sehemu ambako watu wanapeana visogo unatafutwa mwafaka ili kuweza kusonga mbele. Lakini Afrika Kusini inakabiliwa na matatizo ya kimsingi. Asilimia 55 ya watu wanahesabika kuwa masikini na asilimia 27 hawana ajira na hasa vijana. Na tangu mwaka 2008 vijana ndio wamekuwa wanawashambulia waafrika kutoka nchi nyingine.

Gazeti la Weser Kurier linatilia maanani kwamba safari hii nchi kadhaa za Afrika zimechachamaa. Nchini Nigeria, Kongo na Msumbiji watu walilipiza kisasi. Gazeti hilo linasema kama jinsi waafrika walivyokuwa wanabaguliwa chini ya utawala wa makaburu, sasa Afrika Kusini imejiweka katika hatari ya kutengwa na nchi nyingine za Afrika.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung limeandika juu ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi nchini Ubelgiji na juu ya mustakabal wa Kongo kwa jumla na  linaeleza kwamba Rais Tshisekedi alifanya ziara nchini Ubelgiji kuanzia Jumanne hadi Ijumaa wiki hii. Hapo awali aliishi nchini humo kama mkimbizi lakini sasa amerejea kwa siku chache tu kama Rais wa nchi yake ya Kongo. Ziara ya Tshisekedi ina lengo la kuujenga upya uhusiano baina ya nchi yake na nchi za Ulaya kwa jumla.

Gazeti la die Tageszeitung linakumbusha kwamba pia Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Heiko Maas alifanya ziara nchini Kongo ambako aliahidi kuyaunga mkono mageuzi yanayofanywa na serikali ya Rais Tshisekedi, die tageszeitung linatumai kwamba Tshisekedi ataielekeza nchi yake upande wa magharibi  tofauti na rais wa hapo  awali Joseph Kabila aliyeshirikiana zaidi na China katika mambo ya  kibiashara.

Gazeti la die Tageszeitung linatilia maanani kwamba Kongo ina utajiri mkubwa wa maliasilia. Na kwa ajili ya kushirikiana na Kongo nchi za magharibi ziko tayari kusahau shutuma zilizotoa juu ya matokeo ya uchaguzi wa Rais ambapo Tshisekedi alishinda.

Vyanzo:/Deutsche Zeitungen