Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 16.08.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Baadhi ya yaliyozingatiwa kwenye magazeti ya Ujerumani kuhusu bara la Afrika ni pamoja na kupatikana kwa dawa mpya za kutibu homa ya ebola nchini Kongo pamoja na hali ya kisiasa katika nchi za Kaskazini mwa Afrika.

Gazeti la Berliner Zeitung, limeandika juu ya ugunduzi wa dawa mpya zinazotibu homa ya ebola iwapo maambukizi yatagundulika mapema. Hatimaye kuna habari njema kutoka katika eneo lililoathiriwa na homa ya Ebola nchini Kongo. Baada ya miezi kumi ya majaribio ya dawa, wanasayansi wamegundua kuwa dawa mpya za aina mbili zinafanya kazi kwa ufanisi zaidi dhidi ya virusi vya Ebola tofauti na dawa zilizotumika hapo awali. Daktari Jean-Jacques Muyembe anayehusika  na udhibiti wa ugonjwa huo amenukuliwa akisema, "Kuanzia sasa hatuhitaji tena kusema kuwa Ebola haina tiba.” Daktari huyo amesema ugunduzi huo utasaidia kuokoa maelfu ya maisha ya watu.

Gazeti hilo limeandika, licha ya mapambano dhidi ya mlipuko wa homa ya Ebola watu wamekuwamekuwa wakionesha wasiwasi kwa wizara ya afya nchini humo pamoja na watoa misada ya afya wa mashirika ya kigeni. Wote wanatuhumiwa kusababisha ugonjwa huo kwa madai kuwa wananufaika kiuchumi kutokana na kuwepo kwa homa ya ebola.

Nalo gazeti la Süddeutsche Zeitung linaandika pia habari kutoka huko huko Kongo lakini lenyewe linaangazia juu ya mgogoro wa ardhi nchini humo na mashirika ya kutoa misaada. Mvutano huo umezidi kufukuta baada ya mlinzi wa kampuni ya kijerumani DEG inayofadhiliwa na benki ya umma ya Ujerumani KFW, kutuhumiwa kumuua mwanaharakati  wa haki za binadamu. Hii ni baada ya kuwepo kwa mgogoro kati ya wazalishaji wa mafuta ya mawese na sehemu ya wakazi nchini humo. Mauaji hayo yamezidi kuchochea mzozo baina ya makundi hayo mawili wakati ambapo mazungumzo ya usuluhishi yanatakiwa kuanza, huku mtandao wa wanaharakati nchini Kongo ukifanya mawasiliano na kampuni ya DEG ili kufanya mazungumzo huru ya kusuluhisha mgogoro huo.

Wiki hii Die Tages Zeitung linaandika jinsi jimbo la Makueni nchini Kenya chini ya Gavana Kivutha Kibwana lilivyopiga hatua katika mapambano dhidi ya rushwa. Gazeti hili limeandika, huko Makueni Kusini mwa Kenya, Gavana Kivutha Kibwana anafanya siasa za kuwashirikisha zaidi wananchi. Gavana huyo anasema siri kubwa ya mafanikio yake ni rahisi sana "kuasikiliza wananchi na kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo inatekelezwa bila ya fedha ilizotengewa kupelekwa kusikohusika." Wakazi wengi wa Makueni wanafurahishwa na Gavana wao na kwamba tangu achaguliwe mwaka 2013, Kivutha mwenye umri wa miaka 65 amejiweka mbali na makundi ya kisiasa ya Kenya jambo ambalo si kawaida kwa Kenya ambapo raia hushirikishwa kwa kiasi kidogo. Fedha hupotelea mifukoni mwa wanasiasa, maafisa na wakandarasi. Gazeti hilo limeandika, ni kweli kuwa baadhi ya wakuu wa makampuni wameshtakiwa kwa rushwa, na pia baadhi ya magavana na hata waziri wa fedha, lakini hukumu hutolewa mara chache.

Kwa upande wake gazeti la Frankfuter Allgemeine limeangazia kuhusu migogoro ya kisiasa katika nchi za kiarabu Kaskazini mwa bara la Afrika. Linaanza kuifananisha miogoro hiyo na ile inayoendelea katika nchi nyingine kama vile Syria na Yemen ambapo matokeo yake ni umwagaji damu, na mgogoro mkubwa wa kibinadamu. Hata hivyo kwa nchi tatu za Kaskazini mwa Afrika yaani Sudan, Algeria naTunisia zinapigania mfumo mpya wa kisiasa. Sudan wamekubaliana kipindi cha mpito baada ya kumgoa madarakani Omar al Bashir. Hali ngumu zaidi ya kuleta mabadiliko ya kisiasa, inaonekana zaidi Sudan. Vita ya wenyewe kwa wenyewe huko Darfur kati ya Kusini na Kaskazini zimeichakaza nchi hiyo.

Kwa Algeria watawala wa zamani wanakabiliwaa na changamoto toka makundi mawili ya kijamii ambayo hayana viongozi werevu sana bali wanaoshirikiana kwa kutumia mtazamo wenye mgawanyiko- kundi la Udugu wa kiislamu na wafuasi wa mrengo wa kushoto toka katika utawala. Gazeti hili limeandika tofauti na Sudan, Algeria haijawa na maandamano yenye mauaji ya watu wengi kama Sudan. Maandamano hayakuwa ya kumwaga damu. Waandamanaji walimwondoa Rais wao bila Rais huyo kuwa uhamishoni kama Tunisia  ama kuwa jela kama ilivyokuwa Misri au kumuua kama ilivyotokea Libya.

Vyanzo:  Magazeti ya Ujerumani/ Deutsche Zeitungen