Afrika katika Magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 20.11.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Afrika katika Magazeti ya Ujerumani

Yasemavyo magazeti ya Ujerumani kuhusu Afrika

Jenerali Mohammed Hassan el-Farrow (kushoto)akishikana mikono na kamanda wa jeshi la SPLA, Taban Deng, baada ya kutiwa saini Mkataba wa kudumu wa amani juu ya Kusini mwa Sudan mjini Naivasha, Kenya

Jenerali Mohammed Hassan el-Farrow (kushoto)akishikana mikono na kamanda wa jeshi la SPLA, Taban Deng, baada ya kutiwa saini Mkataba wa kudumu wa amani juu ya Kusini mwa Sudan mjini Naivasha, Kenya

Miaka mitano baada ya kukamilika mkataba wa amani baina ya serekali kuu ya Sudan ya mjini Khartoum na Chama cha Ukombozi wa Sudan, SPLM, kilichokuwa kinapigania Sudan ya Kusini ijitenge, mwenendo wa amani unaolegalega katika nchi hiyo ilio kubwa kabisa kwa eneo barani Afrika, uko katika hatua zake za mwisho. Mwaka 2011 Wa-Sudan ya Kusini watachagua katika kura ya maoni kama wanataka kuwa na dola yao wenyewe. Uchaguzi wa bunge hapo April mwakani utakuwa hatua muhimu ya mwisho.

Lakini serekali ya mkoa wa Kusini mwa Sudan huko Juba inataka uchaguzi wa bunge wa mwakani uahirishwe. Jambo hilo limeripotiwa katika gazeti la TAGESZEITUNG la mjini Berlin, likisema ombi hilo linachunguzwa bado na serekali kuu ya Khartoum. Sudan ya Kusini ina mamlaka ya utawala wa ndani tu, maamuzi yanayohusu nchi nzima yanachukuliwa katika mji mkuu wa Khartoum. Wafanya kazi wa serekali na wabunge wametakiwa huko Kusini mwa Sudan wasaidie kuwavutia watu wajiandikishe kupiga kura kwa ajili ya uchaguzi huo. Rais wa Kusini mwa Sudan, Salva Kiir, anahitaji kila kura ili chama chake cha SPLM kiwe na uzito katika bunge la Khartoum na pia katika bunge la mkoa mjini Juba. Lakini wale Wa-Sudan ya Kusini, ambao katika vita vya kienyeji vilivodumu miaka 20, licha ya maafa waliokumbana nayo, walibakia katika upande wa vuguvugu la Salva Kiir, wanakataa, kwa mara ya kwanza, kufuata agizio hilo la watawala.

Kwa mtizamo wa watu wengi, sababu ya zoezi la uandikishaji wapigaji kura kwenda polepole mno, ni kutoonekana matunda ya mapatano ya amani huko Kusini mwa Sudan. Inadaiwa raia wanapatiwa ulinzi si wa kutosha, katika maeneo mengi sura ya dola haiko, na mahala ambapo watu wanasononeka kwa njaa au wanalazimika kukimbia kutoka kwa maharamia wenye silaha, kwa wao uchaguzi sio kipaumbele. Mnamo mwaka huu peke yake, Wasudan ya Kusini laki tatu wamekimbia na zaidi ya 2,500 wamekufa kutokana na mapigano katika mkoa huo, hasa ya kikabila na ya wizi wa mifugo. Pia kumeripotiwa mauaji ambapo wengi wa wahanga ni wanawake na watoto.

Kuna wale wanaosema kwamba baadhi ya mapigano hayo yanachochewa na serekali kuu ya Khartoum, lakini kuna wale wanaobisha na kusema kwamba serekali ya SPLM huko Juba inaitumia sababu hiyo huenda kuficha matatizo ilio nayo, kama vile madai ya kuweko rushwa serekalini na wabunge kushindwa kuyatembelea majimbo yao ya uchaguzi.

Kwa mara ya kwanza Ujerumani imetumia kitabu cha sheria za kimataifa za uhalifu. Sheria hiyo imeanza kufanya kazi tangu mwaka 2002 na adhabu zinatajwa kwa mauaji ya halaiki, uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita. Lakini hadi punde, mwendeshaji mkuu wa mashtaka wa Shirikisho la Ujerumani aliye pekee na dhamana hiyo, amekataa kuendesha upelelezi juu ya tuhuma kama hizo.

Gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG limeandika kwamba, lakini, mara mambo yamekuwa vingine sasa. Jumanne iliopita, askari kanzu wa Ujerumani walimkamata Ignace Murwanashyaka, rais wa wanamgambo wa Kihutu wa Rwanda, aliye na umri wa miaka 46, na pia katika eneo la Stuttgart wakamtia mbaroni makamo wake, mwenye umri wa miaka 48, Straton Musoni. Wote wawili wanatuhumiwa kufanya uhalifu mkubwa katika eneo la Kongo mpakani na Rwanda- kutoka Januari 2008 hadi July mwaka 2009 wameuwa mamia ya raia, kubaka, kuvamia vijiji na kuwakimbiza wakaazi wa vijiji hivyo. Mwendeshaji mkuu wa mashtaka wa Ujerumani atawasilisha mashtaka yake kwa mujibu wa sheria za kimataifa, na jambo hilo linaweza kufanyika katika mahakama ya Stuttgart, kwa vile mwishoni washukiwa hao waliishi katika Mkoa wa Baden-Württemberg. Kwa makisio ya wanasheria ni kwamba kesi hiyo itakuwa muhimu sana kwa mahakama.

Pia toleo lengine la agzeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG lilijishughulisha na kile kinachosikika huko Afrika Kusini. Ni kwamba Caster Semenya, yule msichana mwenye umri wa miaka 18, bingwa wa dunia wa mbio za mita 800, yu katika hali nzuri, na kinyume na vile watu walivofikiria kwamba atakuwa sio katika kama hiyo kutokana na kuwa katikati ya yale mabishano juu ya ujinsia wake, watu wengine wakidai kwamba huenda ni wa jinsia mbili.

Wiki hii shirikisho la michezo ya riyadha duniani, IAAF, lilitaka kutoa uamuzi juu ya kisa cha msichana huyo, kama abakie na ubingwa na nishani yake na pia aendelee kukimbia katika michuano ya wanawake. Lakini taarifa ya shirikisho la IAAF baadae ilisema uchunguzi wa kimatibabu kwa mwanariadha huyo haujakamilika. Alhamisi, lakini, wizara ya michezo ya Afrika Kusini iliharakisha kutoa taarifa kwamba Caster Semenya atabakia na zawadi yake ya ushindi ya dola 60,000, na kwamba imekubaliwa matokeo ya uchunguzi aliofanyiwa yasichapishwe. Lakini shirikisho la michezo ya riyadha duniani halijahakikisha hayo. Suali la kama Semenya ni mwanamume au mwanamke lilizusha mabishano makubwa katika ulimwengu wa riyadha, na hata waziri wa michezo wa Afrika Kusini, Makhenkesi, alitishia vita vya tatu vya dunia pindi shirikisho la IAAF litafikiria kutomruhusu tena msichana huyo kushiriki tena katika michuano ya mbio.

Na kwa hayo basi, ni mimi Othman Miraji ninayekamilisha makala haya ya Afrika katika magazeti ya Ujerumani. Hadi wakati mwengine.

mwandishi: Miraji Othman

Mhariri : Mohammed Abdulrahman

 • Tarehe 20.11.2009
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/KcCi
 • Tarehe 20.11.2009
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/KcCi