Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 10.05.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Ujerumani

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yameandika juu ya hali ya kisiasa ya nchini Afrika Kusini, mvutano wa kisiasa nchini Sudan na manufaa ya viboko katika mzunguko wa upatikanaji wa chakula miongoni mwa masuala mengine.

Süddeutsche

Makala ya gazeti la Süddeutsche inazungumzia juu ya hali ya kisiasa nchini Afrika Kusini. Gazeti hilo limemnukulu Rais Cyril Ramaphosa wa nchi hiyo alipozungumza wakati wa kampeni za uchaguzi. ramaphosa alisema  "hatutajikunyata na kusalimu amri. Tutatumia kila nyenzo zilizopo katika juhudi za kuhakikisha kwamba waliopewa dhamana ya uongozi wanawatumikia wananchi badala ya kujaza mifuko yao."  Ramaphosa ameahidi kuiong'oa mizizi ya ufisadi iliyoota ndani ya chama cha African National Congress, ANC na tangu aingie madarakani amekuwa anazungumzia juu ya kuleta mabadiliko.

Gazeti la Süddeutsche linatilia maanani kwamba baadhi ya wanasiasa wa chama cha ANC wameigeuza serikali ya Afrika Kusini kuwa sehemu ya kujichotea utajiri na wanafanya hivyo kwa kushirikiana na baadhi ya raia weupe wa nchi hiyo, na kampuni za Ulaya. Jee mapambano dhidi ya ufisadi, ambayo Rais Ramaphosa aliyaahidi yako wapi? Gazeti linasema. Jibu litapatikana baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu. Itaonekana jinsi harakati za kupambana na ufisadi zitakavyoendeshwa. Itaonekana iwapo Ramaphosa atamzima Jacob Zuma na kikundi chake ambacho bado kina usemi mkubwa ndani  ya chama cha ANC.

die tageszeitung

Gazeti la die tagezeitung linazunzumzia juu ya wasaa wa uamuzi nchini Sudan. Linauliza ni nani atakayeondoka kidedea katika mvutano baina ya wapinzani na wanajeshi? Gazeti hilo linaeleza kwamba wapinzani wamekataa kusimamisha harakati zao kwa sababu bado hawajakubaliana na wanajeshi juu ya idadi ya wawakilishi wa kila upande kwenye baraza la kipindi cha mpito. Kipengele hicho ni muhimu kwa sababu baraza hilo ndilo litakalokuwa na mamlaka makubwa juu ya baraza la mawaziri la siku za usoni. Baadhi ya wapinzani wamesema wanataka kuwa na uhakika kwamba harakati zao haziwi kazi bure.

Wapinzani wanataka kuundwa baraza la mpito la wajumbe 15 na wanane watoke katika upande wao. Lakini wanajeshi wanapinga. Wapinzani na wanajeshi pia hawajakubaliana juu ya muda wa kipindi cha mpito hadi kufanyika uchaguzi.

Die Welt

Nalo gazeti la Die Welt linazungumzia ziara ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel katika nchi za eneo la Sahel. Gazeti hilo linasema Merkel alifanya ziara hiyo kwa lengo la kujenga uhusiano wenye manufaa kwa kila upande.

Gazeti la Die Welt linaeleza kwamba mawasiliano baina ya Kansela wa Ujerumani na viongozi wa nchi za eneo la Sahel, magharibi mwa Afrika yameongezeka. Merkel anaendeleza siyo urafiki tu bali anatoa mchango madhubuti katika siasa za eneo hilo. Viongozi wa nchi tano walikutana na Merkel katika mji mkuu wa Burkina Faso, Ouagadougou.

Kansela wa Ujerumani na viongozi hao wa Afrika walijadili juu ya njia za kukabiliana na ugaidi na juu ya sera ya maendeleo itakayoleta faida kwa pande zote.  Merkel mwenyewe amesema kila upande utanufaika kwa kiwango sawa. Ameielezea sera yake ya Afrika kuwa ni mabadiliko.

Der Tagesspiegel

Gazeti la Der Tagesspiegel linatufahamisha juu ya manufaa ya viboko katika mzunguko wa upatikanaji wa chakula. Gazeti hilo linatueleza kwamba vinyesi vya wanyama hao ni muhimu kwa mfumo wa ikolojia.

Wanyama hao wanatoa mchango mkubwa katika kueneza madini ya Silicon ambayo ni muhimu kwa lishe ya majani yanayostawi chini ya maji. Kwa mujibu wa utafiti wa wanasayansi, viboko wanatoa tani 11 za vinyesi kila siku kwenye ziwa Mara katika mbuga ya Maasai Mara.

Asilimia ya vinyesi hiyvo ni madini ya Silicon ambayo ni muhimu kwa ustawi wa majani hayo yanayoitwa mwani. Majani hayo yanachangia katika mfumo wa upatikanaji wa chakula na pia yanatoa hewa safi. Pia ni muhimu katika mchakato wa kupunguza sumu ya nitrojeni. Bila ya madini ya Silicon vidubini au viumbe hai wadogowadogo wengi hawataweza kuendelea kuishi duniani.

 

Vyanzo:/Deutsche Zeitungen