Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 26.04.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Karibu tuyadurusu pamoja  yaliyoandikwa na magazeti ya Ujerumani juu ya matukio na masuala ya barani Afrika.

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine juu ya changamoto za maradhi ya Malaria nchini Msumbiji ambazo zimekuwa kubwa zaidi kutokana na maafa yaliyosababishwa na kimbunga Idai. Gazeti hilo linasema harakati za kupambana na maradhi ya malaria zimerudi nyuma nchini Msumbiji kutokana na janga liloletwa na kimbunga Idai. Hadi kufikia mwaka 2017 hatua kubwa zilikuwa zimepigwa nchini humo katika juhudi za kupambana na ugonjwa huo. Katika baadhi ya wilaya idadi ya watu waliokumbwa na malaria ilizidi kupungua na katika sehemu nyingine hakuna mikasa iliyoripotiwa.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema hali imebadilika baada ya Msumbiji kukumbwa na kimbunga hicho Idai na linaeleza zaidi Watu wakirejea kwenye makaazi yao yaliyoathiriwa na mafuriko watawakuta mbu wanawasubiri. Gazeti hilo linashauri kwamba msaada wa jumuiya ya kimataifa utahitajika kwani bara la Afrika linapoteza kiasi cha dola bilioni 12 kila mwaka kwa sababu ya watu kushindwa kwenda kazini kutokana na maradhi ya malaria.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung linatupeleka Burkina Faso ambako linasema serikali ya nchi hiyo inatatizwa na wanamgambo wanaoitwa Koglweogo. Jee hao ni watu gani? Gazeti hilo linatueleza kwamba makundi ya wanamgambo hao yalianzishwa mnamo mwaka 2015 na yamekuwa yanafanya kazi ya polisi. Wanamgambo hao wanajulikana kama walinzi wa misitu kwa sababu wanalinda sehemu ambapo mashambulio ya kigaidi yamekuwa yanatokea mara kwa mara nchini Burkina Faso na hasa kwenye jimbo la Centre Nord la kaskazini mwa nchi hiyo.

Lakini walinzi hao wamekuwa mtihani kwa sababu wanalipiza kisasi kwa watu wa kabila la Peul ambao pia wanajibu mashambulio je ni kwa sababu gani? Gazeti la die tageszeitung linasema sababu ya kuwaandama watu wa kabila hilo ni kwamba mmoja wa viongozi wa kundi la kigaidi linaloitwa JNMI, nchini Burkina Faso anatoka kwenye kabila hilo. Kundi hilo linahusishwa na mashambulio ya kigaidi yanayotokea mara kwa mara nchini Burkina Faso. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba wanamgambo hao wanaungwa mkono na baadhi ya wananchi. Waziri wa utawala wa majimbo, ameandikiwa barua ya kumtaka awatambue rasmi wanamgambo hao kwa sababu wanazuia kutokea mashambulio ya magaidi.

Die Zeit

Nalo gazeti la Die Zeit limeandika juu ya ziara ya waziri mkuu wa jimbo la Bavaria Markus Söder nchini Ethiopia. Gazeti hilo linatilia maanani juu ya ziara hiyo. Waziri mkuu wa jimbo hilo la kusini mwa Ujerumani bwana Söder amefanya ziara yake ya kwanza kabisa katika nchi za nje. Hakwenda, Marekani, Ufaransa au China bali amekwenda Ethiopia. Bwana Söder ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha Christian Social Union,CSU kilichomo katika serikali ya mseto ya Ujerumani, alifanya ziara hiyo kwa lengo la kuanzisha ukurasa mpya wa uhusiano baina ya Ujerumani na nchi za Afrika. Ni barani Afrika ambako yalichimbuka matatizo yaliyoitumbukiza Ujerumani katika mgogoro wa wakimbizi uliowazungusha vichwa wanasiasa wa Ujerumani katika miaka mitatu iliyopita.

Katika ziara yake nchini Ethiopia waziri mkuu wa jimbo la Bavaria Markus Söder alitembelea miradi ya maendeleo na kambi ya wakimbizi wanaotoka Sudan Kusini.

Gazeti hilo la Die Zeit linasema asilimia 60 ya wakimbizi hao ni watoto ambao hawajafika hata umri wa miaka 18. Waziri Mkuu wa jimbo la Bavaria bwana Söder alitoa msaada wa dola laki moja kwa ajili ya vifaa vya shule, mahitaji ya maabara na pia aligawa jezi za timu maarufu ya Bayern Munich.

Mwandishi:Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Josephat Charo