1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz
29 Juni 2018

Wiki hii magazeti ya Ujerumani pamoja na mengine yameandika juu ya mripuko wa  gurunedi uliotokea kwenye mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na waziri mkuu mpya wa Ethiopia Abiy Ahmed.

https://p.dw.com/p/30WiJ
Äthiopien Abiy Ahmed, Premierminister
Picha: Getty Images/AFP/Y. Tadesse

die tageszeitung

Makala ya gazeti  la die tageszeitung juu ya shambulio la gurunedi lililotokea kwenye mkutano wa hadhara uliohutubiwa na waziri mkuu mpya  wa Ethiopia Abiy Ahmed. Watu wawili waliuawa kutokana na shambulio hilo na wengine zaidi  ya 150 walijeruhiwa. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba waziri mkuu Ahmed anadhamiria kuleta mageuzi muhimu nchini Ethiopia na linaeleza kwamba waziri huyo mkuu wa Ethiopia anataka kusonga mbele haraka  na mageuzi katika sera ya  ardhi.

Tangu aingie madarakani mnamo mwezi  wa Aprili waziri mkuu huyo ameweza kuziteka nyoyo za idadi kubwa ya wananchi wake. Katika muda huo mfupi waziri mkuu Ahmed amezitekeleza ahadi zake juu ya kuleta mabadiliko nchini Ethiopia. Maalfu ya wafungwa wa kisiasa wameachiwa na uhuru wa  vyombo vya habari umerejeshwa nchini humo na ameanza mazungumzo na wapinzani. Pamoja na hayo kiongozi huyo mpya wa Ethiopia ameanza kuchukua hatua za kuutatua mgogoro wa mpaka baina ya  nchi yake na nchi jirani ya Eritrea.

Neue Zürcher

Gazeti la Neue Zürcher pia limeandika juu ya shambulio la bomu lililotokea karibu na mahala alipokuwapo rais Emmerson Mnangagwa katika mji wa Bulawayo. Bomu hilo liliripuka mara tu baada  ya Mnangagwa kumaliza kuhutubia kwenye mkutano wa hadhara, lakini alinusurika. Hata hivyo watu wawili waliuawa na wengine 47 walijeruhiwa. Gazeti la Nuer Zürcher linaendelea kueleza kwamba rais Mnangagwa anaamini kwamba yeye ndiye alielengwa katika shambulio hilo lakini amesema hatavunjika moyo.Amesema hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa maadui zake kujaribu kumwangamiza. Rais Mnangagwa amedai kwamba mke wa rais wa hapo awali Grace Mugabe alijaribu kumtilia sumu kwenye ice cream.

Gazeti hilo la Neue Zürcher limemnukulu makamu wa rais wa Zimbabwe Chiwenga akisema kuwa shambulio hilo halitavuruga mpango wa kufanyika uchaguzi mkuu wa mwezi ujao. Ni maoni ya gazeti la Neue Zürcher kwamba huenda shambulio hilo likahusiana na mvutano uliopo baina ya jeshi na chama tawala cha Zanu-PF Lakini mpaka sasa hakuna yeyote aliyedai kuhusika na hujuma hiyo.

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa
Rais wa Zimbabwe Emmerson MnangagwaPicha: picture-alliance/AP Photo/T. Mukwazhi

Gazeti la Neue Zürcher wiki hii pia limeandika juu ya kuathirika kwa sarafu ya Rand nchini Afrika kusini kutokana na sera mpya za utawala wa Donald Trump. Gazeti hilo linasema furaha kubwa iliyoonekana baada ya rais Zuma kuondoka madarakani, sasa imefifia kutokana na sarafu ya Rand kupungua thamani mbele ya dola ya Marekani na linauliza jee ujio wa rais Ramaphosa ulikuwa ni nguvu ya soda?

Gazeti hilo linaeleza kwamba Rais mpya wa Afrika kusini Cyril Ramaphosa aliingia madarakani mnamo mwezi wa februari baada ya rais wa hapo awali Jocob Zuma kungátuliwa. Ujio wa Ramaphosa ulimaanisha kumalizika kwa miaka tisa ya utawala wa kifisadi, chini ya uongozi wa Jacob Zuma. Uchumi wa Afrika kusini ulianza kustawi tena na sarafu ya Rand iliongezeka thamani lakini sasa sera ya utawala wa Donald Trump inatibua mambo siyo tu nchini Afrika kusini bali pia katika nchi zote zinazoinukia kiuchumi. Sera ya benki kuu ya Marekani inaathiri kasi ya maendeleo ya nchi hizo.

Gazeti la Neue Zürcher linatilia maanani kwamba vita vya kibiashara vilivyoanzishwa na utawala  wa Trump dhidi ya China pia vinauathiri uchumi wa Afrika kusini, na nchi hiyo haina nguvu za kukabiliana na vita hivyo. Katika robo ya pili ya mwaka huu tija ya uchumi ilipungua kwa asilimia 2  mara nne ya kiwango kilichotarajiwa. Rais mpya hana cha kuonyesha kama mafanikio, baada ya siku zaidi ya mia moja tangu kuingia madarakani huku kukiwa na wasi wasi unaotokana na mpango wa kuleta mageuzi ya sera ya ardhi. Gazeti la Neue Zürcher linasema serikali ya Afrika Kusini ina mpango wa kutaifisha ardhi bila ya kulipa fidia.

Süddeutsche Zeitung

Kuhusu nchini Afrika Kusini gazeti la Süddeutsche linatupasha habari juu ya kifo cha mpiga picha maarufu  wa nchi hiyo David Goldblatt alieorodhodhesha mengi yaliyotokea wakati wa utawala wa kibaguzi. Mpiga picha huyo hakuridhika kuona maji yametuama tu alitaka kujua nini kilikuwa kinatokea chini ya maji hayo.

Mpiga picha maarufu wa Afrika Kusini David Goldblatt aaga dunia
Mpiga picha maarufu wa Afrika Kusini David Goldblatt aaga duniaPicha: AFP/Getty Images

Gazeti hilo la Süddeutsche linasema mpiga picha Goldblatt atakumbukwa kwa msemo wake maarufu kwamba jukumu lake lilikuwa kuyaenzi yale yasiyoonekana haraka machoni!. Goldblatt aliyezaliwa mnamo mwaka 1930 alishuhudia jinsi chama cha National Party kilivyoingia madarakani nchini Afrika Kusini na kutayarisha njia ya kuanzisha mfumo wa kibaguzi mnamo mwaka 1948. Msanii huyo hakutaka kupiga picha mambo ya kusisimua bali alielekeza macho yake kwenye mambo na matukio yaliyosababisha misisimuo kwa mfano uzio uliojengwa na walowezi wa kizungu mnamo mwaka 1660 kwa lengo la kujihami dhidi ya wenyeji.

Gazeti la Süddeutsche linasema hiyo haikuwa picha ya kusisimua lakini iliashiria mwanzo wa utawala wa kibaguzi nchiniAfrika Kusini. Mpiga picha huyo Goldblatt alifariki dunia jumatatu iliyopita katika mji wake wa Johannesburg akiwa na umri wa miaka 87. 

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Mohammed Khelef