1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz
23 Machi 2018

Gazeti la die tageszeitung limeandika juu ya mkataba wa kuanzisha biashara huru baina ya nchi za Afrika. Mkataba huo kabambe ulitiwa saini na viongozi kutoka nchi 44 za Afrika, waliokutana Kigali, mji mkuu wa Rwanda.

https://p.dw.com/p/2uqWi
Ruanda Kigali Unterzeichnung Afrikanisches Freihandelsabkommen
Picha: Getty Images/AFP/STR

die tageszeitung

Mkataba huo unaoitwa, CFTA kwa kifupi, unahusu biashara ya soko litakalowanufaisha watu bilioni 1.2  barani Afrika. Gazeti la die tageszeitung linasema mapatano yaliyofikiwa na viongozi wa bara hilo yataleta mageuzi katika sekta za huduma na bidhaa kwa asilimia 90. Hata hivyo gazeti hilo limetilia maanani mambo mawili. Kwanza Uganda na Nigeria bado zimejiweka kando na mkataba huo na pili limemnukuu mkurugenzi wa biashara wa soko la pamoja la nchi za mashariki na kusini mwa Afrika, Comesa akisema kuwa muda mrefu utahitajika ili kuweza kuyaweka mambo sawa.

Neues Deutschland

Nalo gazeti la Neues Deutschland wiki hii linatahadharisha kwamba watu milioni 80 huenda  wakalihama bara la Afrika, ikiwa hatua thabiti hazitachukuliwa ili kuzikabili athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi. Gazeti hilo limeinukuu ripoti ya Benki ya dunia.

Mchoro kuhusu mabadiliko ya Tabianchi (Index 2017 POR -DW)
Mchoro kuhusu mabadiliko ya Tabianchi

Ripoti hiyo inawatanabahisha wahusika wote na inatahadhrisha kwamba baadhi ya maeneo barani Afrika yatakumbwa vibaya zaidi, kuliko mengine, na athari hizo. Gazeti la Neues Deutschland limewanukuu wataalamu walioandika ripoti ya benki ya dunia wakisema maeneo hayo hayataweza kutumika kwa kilimo, na kwa hivyo binadamu hawataweza tena kuishi katika sehemu hizo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, huenda Waafrika wapatao milioni 80 wakalihama bara lao hadi ufikapo mwaka wa 2050. Lakini gazeti hilo linasema, licha ya tahadhari zinazotolewa pana hatari ya ajizi kufanyika na kwamba huenda watu katika maeneo husika wakasahauliwa!

die tageszeitung

Makala nyingine iliyoandikwa na gazeti  la die tageszeitung mnamo wiki hii, inahusu mgogoro wa kibinadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kwa mujibu wa gazeti hilo mgogoro huo ni mkubwa kabisa duniani na kwamba, sasa jumuiya ya kimataifa haipaswi kunyamaza kimya. Gazeti hilo linaeleza sababu za kuitaka jumuiya ya kimataifa ichukue hatua.

Mgogoro wa kibinadamu nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Mgogoro wa kibinadamu nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya KongoPicha: DW/M. El Dorado

Kwanza wananchi milioni 13.1 wa Jamhuri  ya kidemokrasia ya Kongo wanahitaji misaada. Raia wengine 670,000 wa nchi hiyo wamekimbilia katika nchi za jirani na wengine milioni 4 na nusu ni wakimbizi wa ndani huku watu milioni 7 .7 wa nchi hiyo wanateseka kwa njaa. Gazeti la die tageszeitung linasema mgogoro wa nchini Kongo umewekwa kandoni mwa ajenda ya diplomasia ya kimataifa.

Gazeti hilo pia linailaumu Ujerumani kwa kuupuuza mgogoro huo na linasema msimamo huo ni wa makosa. Gazeti linasema hatari ni kubwa ikiwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo itaripuka, basi nusu ya bara la Afrika itakumbwa na matatizo makubwa!

Der Tagesspiegel

Nalo gazeti la Der Tagesspiegel linatupasha habari juu ya Faru dume mweupe wa mwisho aliyekufa jumatatu wiki hii huko nchini Kenya. Uhai wa kiumbe huyo, aliyeitwa Sudan, ulikatizwa kutokana na matatizo ya kiafya yaliyosababishwa na umri wake uliokuwa mkubwa. Gazeti la Der Tagesspiegel linafahamisha kwamba Sudan alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa baridi yabisi, ulioathiri vibaya viungo vya mwili wake. Sudan alidungwa sindano ya huruma  ili  kumwepusha na mateso. Alikuwa amewekwa kwenye hifadhi ya OL Pejeta huko nchini Kenya ili kumlinda dhidi ya majangili. Faru Sudan alifikia umri wa miaka 45 katika uhai wake.

Faru Sudan enzi za uhai wake
Faru Sudan enzi za uhai wakePicha: picture-alliance/Photoshot/S. Ruibo

Kifo cha faru huyo kilitokea wakati ambapo mamia ya wanasayansi na wawakilishi wa serikali mbalimbali kutoka duniani kote walipokuwa wanakutana nchini Columbia, kutathmini kasi ya kutoweka kwa baadhi ya viumbe. Gazeti hilo linasema kifo cha Faru huyo aliyekuwa adimu kinatoa ujumbe wa tahadhari kwamba hiyo ndiyo hali inayoweza kutokea katika siku za usoni, yaani kutoweka kwa aina fulani ya viumbe.

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri:Josephat Charo