Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 15.09.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Ujerumani

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Gazeti la die tageszeitung linasema Rais Yoweri Museveni wa Uganda amepewa ruhusa ya kuzeekea madarakani. Frankfurter Allgemeine limeandika India na Japan kujenga uhusiano zaidi na Afrika ili kuipa China changamoto.

Makala ya die tageszeitung juu ya uamuzi wa bunge la Uganda wa kukubali kuibadilisha katiba ili kumwezesha rais Museveni kuendelea kuzeekea madarakani. Kwa mujibu wa katiba ya Uganda umri wa juu kabisa wa kugombea urais ni miaka 75 lakini kutokana na mabadiliko yaliyofannywa na bunge kipengele hicho kitaondolewa. Gazeti hilo la die tageszeitung linasema lengo la mabadiliko hayo ni kumuwezesha rais Museveni aliyemo madarakani kugombea tena katika uchaguzi ujao utakaofanyika mwaka 2021 nchini Uganda. die tageszeitung linatufahamaisha kwamba wabunge wa chama cha rais Museveni cha National Resistance Movement (NRM) waliunga mkono hoja ya kubadilisha katiba kwa manufaa ya kiongozi huyo ambaye sasa ana umri wa miaka 71. Chama cha NRM kina viti 293 katika bunge la Uganda lenye jumla ya viti 426.

Gazeti la Süddeutsche Zeitung limeandika kuhusu Kenya na kwa mara nyingine linazungumzia juu ya hisia za watu kwenye vitongoji vya walala hoi baada ya mahakamna ya juu ya nchini humo kuyabatilisha matokeo ya uchaguzi wa rais na kuamaua ufanyike upya. Gazeti la Süddeutshce Zeitung linaeleza kuwa watu wanaoishi kwenye mitaa ya mabanda wanaweka matumaini juu ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga ambaye wanamuona kuwa ni mkombozi wao. Gazeti limemnukulu kijana mmoja anayeishi kwenye kitongoji cha Kibera, Kevin Otieno akisema kuwa Odinga ni mkombozi. Kevin Otieno anayetokea jimbo moja na Raila Odinga ameliambia gazeti la Süddeutsche Zeitung kwamba mambo yake ni mazuri kwa sababu Raila alimpa kiwanja cha kujengea banda lake ambapo anaishi pamoja na mkewe na watoto wawili.  Otieno ameliambia gazeti la Süddeutsche Zeitung kwamba atampigia kura Raila Odinga kwenye uchaguzi wa marudio. Lakini kijana mwingine Stephen Nzusa alinukuliwa na gazeti hilo akiwaambia wakazi wa kitongoji cha Kibera kwamba wasimsubiri mwokozi.

Gazeti hilo la Süddeutsche Zeitung limeeleza kwamba Nzusa alizaliwa hapo hapo Kibera ambayo ni ngome mojawapo kuu ya Raila Odinga kwa miaka zaidi ya 30. Baada ya kuhitimu masomo yake ya sheria Stephen Nzusa amekuwa balozi wa amani katika kitongoji hicho na anatumia muda wake mwingi barabarani kuwaambia watu kwamba wanasiasa sio sawa na wafalme wenye utajiri wa kugawa ruzuku kwa raia.Gazeti hilo limemnukulu balozi huyo wa amani akiwafahamisha wakazi wa Kibera kuwa nyumba zinazoitwa mradi wa wanasiasa zimejengwa kutokana na fedha zilizotolewa na benki ya dunia na sio wanasiasa hao.

Na gazeti la Frankfurter Allgemeine katika Makala yake wiki hii linazungumzia juu ya mashindano ya kuligombea bara la Afrika. Gazeti hilo linasema India na Japan pia zinataka kujikita barani Afrika na hivyo kuipa China changamoto. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema hakuna hata siku moja inayopita barani Asia bila ya watu kuzungumzia jinsi China inavyojiingiza katika nchi za bara la Afrika. Katika ziara yake nchini India waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe na mwenyeji wake Narendra Modi walizungumzia sio tu juu ya shughuli za China barani Asia bali pia wanataka kuwapo mpango wa pamoja wa ustawi wa uchumi baina ya Asia na Afrika. Gazeti la Frankfurter Allgemeine linaelezea kwamba Japan imeshawekeza dola bilioni 32 katika miundombinu barani Afrika. Vile vile gazeti hilo linakumbusha kwamba kwenye mkutano wa kilele baina ya India na nchi za Afrika wa mwaka 2015 waziri mkuu wa India Narendra Modi alizihakikishia nchi za Afrika mkopo wa jumla ya dola bilioni 10.

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:  Mohammed Abdul-Rahman     

 

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com