Afrika katika magazeti ya Ujerumani | NRS-Import | DW | 03.08.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

NRS-Import

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Magazeti yamezungumzia zaidi ujumbe wa kulinda amani Darfur, mazungumzo ya kugawana madaraka Zimbabwe, na ulaghai wa kodi DRC.


►◄
Ni wakati mwingine ambapo nakukaribisha mpendwa msikilizaji uwe nasi katika makala ya Afrika katika magazeti ya Ujerumani . Hizi ni habari zinazohusu bara la Afrika ambazo zimeandikwa katika magazeti ya hapa Ujerumani. Mimi ni Sekione Kitojo na mwenzangu humu studioni ni ……………………….


Nasema tena karibuni….Tunaanza na gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung, ambalo lina kichwa cha habari kinachosema Matokeo ya maafa katika Darfur.SP.


Gazeti linasema kuwa Julai 8 kundi dogo la wanajeshi wa kulinda amani la Afrika katika jimbo la Darfur lilijikuta katika mashambulizi makubwa ya wapiganaji wapatao 200 kwa saa kadha wakiwa na silaha kali. Walinzi hao wa amani walikuwa wanatumaini tu kupata ama msaada wa wanajeshi zaidi ama usaidizi wa jeshi la anga. Wakati huo wanajeshi katika magari ya deraya yaliweza kuwasaidia wanajeshi hao wa kulinda amani. Kwa kuwalinda raia wanajeshi hao wa kulinda amani walikuwa wanahatarisha maisha yao na wanajeshi saba waliuwawa na 19 walijeruhiwa vibaya.Mod.


Ujumbe huo wa kulinda amani wa umoja wa mataifa na umoja wa Afrika sasa umefikisha umri wa mwaka mmoja. Julai 31, 2007 baraza la usalama la umoja wa mataifa kwa kauli moja liliidhinisha azimio lililoanzisha ujumbe huo ambao ni mkubwa wa kulinda amani katika historia ya umoja huo. Leo hii unaonekana kuwa ni ujumbe dhaifu kabisa usiokuwa na vifaa na na wenye matokeo ya maafa.SP.


Gazeti la die Tageszeitung likiandika kuhusu habari hiyo linasema , wanaharakati wa Afrika wanasema umoja wa mataifa umeshindwa Darfur. Gazeti linaendelea kuandika kuwa umoja wa mataifa umeshindwa kuwalinda raia katika jimbo lililokumbwa na vita la Darfur nchini Sudan. Mashirika karibu 50 yasiyo ya kiserikali katika Afrika yamesema kuwa majeshi ya kulinda amani ya umoja wa mataifa na umoja wa Afrika , ambayo yamewekwa kuanzia mwaka 2008 katika jimbo la Darfur yameshindwa kufanya kazi hiyo.Mod.


Die Tageszeitung likiandika habari kuhusu Zimbabwe linasema: majadiliano kwa hivi sasa yamevunjika. Siku chache baada ya matumaini makubwa ya kuanza kwa majadiliano kati ya serikali na upinzani nchini Zimbabwe tayari yamevunjika.Taarifa zinasema kuwa mkuu wa ujumbe wa majadiliano wa upande wa serikali ya rais Robert Mugabe Patrick Chinawasa , siku ya Jumatatu aliondoka katika mazungumzo hayo yanayofanyika nchini Afrika kusini na kurejea katika mji mkuu wa Zimbabwe Harare. Kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai aliondoka baadaye kutoka Harare kwenda Afrika kusini ili kujadiliana na ujumbe wake katika mazungumzo hayo. Msemaji wake George Sibotshiwe amesema mazungumzo yameahirishwa hadi Jumamosi.SP.


Zimbabwe inaogelea katika fedha: hicho ni kidokezo katika taarifa iliyoandikwa na gazeti la Die Welt, ambalo kichwa chake cha habari kinasema mageuzi ya kifedha ; kwa mfano wa Mubage.


Katika mji mkuu Harare noti ya dola milioni 10 inapeperuka mtaani, na hakuna mtu anayeiokota.

Ni kiasi gani, ama ina thamani ndogo kiasi gani, huwezi kusema kwa kuwa ni saa chache tu ukiingia mkononi inakuwa haina thamani tena. Ughali wa maisha hadi katikati ya Julai umefikia kiasi cha asilimia 2.2 milioni, lakini wataalamu wa fedha wanasema huenda ni zaidi ya asilimia milioni kumi hadi milioni 30. Noti ya dola bilioni 100, inatosha kununua nusu mkate. Wakati huo huo Wazimbabwe hawaruhusiwi kuchukua zaidi ya dola bilioni 100 kwa siku katika benki.Mod.


Gazeti linaongeza kuwa rais Robert Mugabe ambaye ameitawala nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 28 sasa anataka kutatua tatizo hilo kwa njia yake. Anasema kuwa ataondoa tarakimu 10 za sifuri katika thamani ya fedha ya nchi hiyo, ameeleza gavana wa benki kuu Gideon Gono. Dola bilioni 10 za Zimbabwe zinatakuwa na dhamani ya dola moja ya nchi hiyo. Hatua hiyo imeanza rasmi siku ya Ijumaa.


Inanukia kutoka Zimbabwe , linaandika gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung.SP.


Gazeti hilo linasema kuwa , mageuzi ya sheria ya ardhi ni suala la mradi muhimu wa mageuzi nchini Afrika kusini. Lakini miaka 14 baada ya kuanguka kwa utawala wa kibaguzi bado suala hilo halijapata mafanikio.

Hadi sasa bado kiasi cha asilimia 80 ya ardhi yenye rutba inamilikiwa na wazungu. Wakati huo huo , hawazalishi zaidi ya idadi ya wakulima wa Kiafrika wanavyozalisha. Kwa hiyo basi utawala wa Afrika kusini unataka hivi sasa kuanza kazi ya mageuzi ya sheria ya ardhi kwa nguvu zote. Wazungu hata hivyo wanapinga.Mod.


Greenpeace dhidi ya Danzer, linaandika gazeti la Süddeutsche Zeitung. Shirika la ulinzi wa mazingira la Greenpeace limelishutumu vikali kampuni la kuuza mbao la Danzer. Katika mwaka 2000 hadi 2006 limeziingizia nchi za jamhuri ya kidemokrasi ya Congo DRC na jamhuri ya Congo kiasi cha Euro milioni 7.8 katika mapato ya kodi. Danzer inaendesha utaratibu ambao unatia shaka wa kulipa kodi ambayo ni mbali na mapato yake ya faida, anasema Oliver Salge kutoka Greenpeace. Shirika hilo la ulinzi wa mazingira limeweka pamoja taarifa iliyotokana na wataalamu wa kodi ambao wanasema kuna udanganyifu katika ulipaji wake wa kodi.


SP.


Na hatimaye gazeti la Die Tageszeitung lina taarifa kuhusu kurejeshwa kwa sheria ya adhabu ya kifo nchini Liberia. Gazeti linaandika; katika nchi ambayo katika muda mfupi uliopita raia wake kadha wameuwawa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe wanahitaji sheria kali dhidi ya walioendesha mauaji. Hivyo ndivyo pengine anavyofikiria rais wa nchi hiyo pamoja na wabunge , kwa kurejesha tena sheria ya adhabu ya kifo.Mod.


Naam kwa taarifa hiyo kutoka Liberia ndio tunafikia mwisho wa makala hii ya Afrika katika magazeti ya Ujerumani kutoka Deutsche Welle mjini Bonn hadi wiki ijayo, Mimi ni Sekione Kitojo na mwenzangu ni………………. Tunasema Kwaherini.

 • Tarehe 03.08.2008
 • Mwandishi Kitojo, Sekione
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EogQ
 • Tarehe 03.08.2008
 • Mwandishi Kitojo, Sekione
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EogQ
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com