1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia yainukia kiuchumi

31 Mei 2015

Magazeti ya Ujerumani yayatilia maanani maendeleo ya uchumi nchini Ethiopia na pia yanauangalia umaarufu wa Sepp Blatter miongoni mwa Waafrika baada ya kuchaguliwa tena kuwa Rais wa FIFA

https://p.dw.com/p/1FZac
Rais wa bodi ya Shirikisho la kandanda duniani Sepp Blattter
Rais wa bodi ya Shirikisho la kandanda duniani, FIFA,Sepp BlatterPicha: Reuters/A. Wiegmann

Gazeti la "Neues Deutschland" lazungumzia changamoto zinazolikabili bara la Afrika katika sekta ya uchumi. Gazeti hilo linasema bara hilo linastawi vizuri kiuchumi lakini yapo mambo yanayoweza kusababisha matatizo.

Gazeti la "Neues Deutschland" hilo limeukariri mtaala wa Benki ya Maendeleo ya Afrika,ADB unaoonyesha kwamba Afrika bado haijautumia uwezo wake wote katika sekta kadhaa. Kwa mfano biashara baina ya nchi za Afrika na nyingine zinazoendelea inafikia thumni tu,yaani moja ya nane.


Kwa mujibu wa mtaala huo changamoto nyingine kwa bara la Afrika ni ongezeko la idadi ya watu.Mtaala huo unaonyesha kwamba Waafrika wataongezeka, takriban mara mbili katika kipindi cha miaka 15 ijayo. Hadi mwaka juzi idadi ya watu barani Afrika ilifikia Bilioni 1.1 Nafasi za ajira Milioni 370 zitahitajika kwa ajili ya vijana hadi utakapofika mwaka wa 2030. Gazeti la "Neues Deutschland limesema mabadiliko ya hali ya hewa pia ni changamoto inayoweza kuuathiri ustawi wa uchumi barani Afrika.

Ethiopia yasonga mbele kiuchumi

Gazeti la "Süddeutsche" linayatilia maanani maendeleo ya kiuchumi yaliyopatikana nchini Ethiopia. Gazeti hilo linaarifu kuwa siku ya wapendanao ,"valentine's day" ni siku muhimu nchini Ethiopia vile vile. Na siyo kwa sababu ya wapendanao wa nchi hiyo tu. Ni kwa sababu ya biashara ya maua ambayo ni muhimu kwa nchi hiyo.

Gazeti la "Süddeutsche" linasema Ethiopia leo imekuwa nchi ya nne duniani kwa uuzaji wa maua.Mnamo mwaka wa 2013 nchi hiyo ilizalisha tani Bilioni 2 za maua. Gazeti hilo linakumbusha kwamba hadi miaka ya hivi karibuni tu nchi hiyo ilikumbwa na maafa makubwa ya njaa.

Gazeti la "Süddeutsche" linaiita Ethiopia kuwa nchi inayoinukia kiuchumi barani Afrika na inafikia ustawi wa uchumi wa hadi asilimia 7. Na gazeti la "Süddeutsche" linatilia maanani kwamba ustawi huo mkubwa wa uchumi hautokani na kuuza dhahabu au mafuta nje, bali unatokana na shughuli za kilimo.

Gazeti hilo linasema ni kutokana na maendeleo ya kilimo kwamba Ethiopia sasa inashika nafasi ya saba kwa ukubwa wa uchumi kusini mwa jangwa la Sahara.

Sepp Blatter ni maarufu barani Afrika

Jarida la "Der Spiegel" wiki hii linatupeleka katika dunia ya kandanda. Limechapisha makala juu ya Rais wa shirikisho la vyama vya kandanda duniani FIFA , Sepp Blatter.Gazeti hilo linawaita Waafrika kuwa ndugu wa Blatter.

Jarida hilo linasema licha ya kuwa mtu wa utatanishi, Blatter anapendwa barani Afrika. Sababu ni kwamba analisaidia bara hilo kwa mamilioni ya fedha kwa ajili ya kuleta maendeleo. Jarida la "Der Spiegel" limemnukulu Rais wa chama cha kandanda nchini Afrika Kusini ,Danny Jordaan akieleza kwamba Sepp Blatter ndiye aliehakikisha kwamba kombe la dunia linachezwa barani Afrika.

Rais wa chama cha kandanda nchini Afrika Kusini ,Jordaan amenukuliwa na jarida la "Der Spiegel" akisema kwamba Sepp Blatter ni shujaa.Jarida hilo limemkariri Jordaan akieleza kwa nini Blatter ni ndugu wa Afrika.

Amesema kuwa hapo awali bara la Afrika lilikuwa linazingatiwa kuwa ni sehemu ya maafa tu. Lakini baada kombe la dunia kuandaliwa kwa mafanikio nchini Afrika kusini, wajihi wa Afrika umejengeka na kuwa bora.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Yusuf Saumu