1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani.

Abdu Said Mtullya12 Desemba 2014

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yameandika juu ya kufutwa kesi ya Kenyatta na juu ya uwezekano wa Oscar Pistorius kupewa adhabu kali zaidi .Mwendesha mashtaka ataka Pistorius ahukumiwe kwa mauaji ya kudhamiria

https://p.dw.com/p/1E3GC
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya
Rais Uhuru Kenyatta wa KenyaPicha: Reuters/T. Mukoya

Wiki hii gazeti la "die tageszeitung"limemnukuu Kamishna wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa akizilaumu vikali nchi za Umoja wa Ulaya kwa tabia ya utepetevu juu ya maafa yanayowafika wakimbizi.

Kenyatta afutiwa kesi

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limeandika juu ya uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa inayopambana na uhalifu ICC ya mjini The Hague wa kumfutia mashtaka Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya. Gazeti hilo linasema Mahakama ya ICC haikuwa na ushahidi. Lakini gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limemnukuu mwendesha mashtaka mkuu Fatou Bensouda akilalamika juu ya ukosefu wa ushirikiano baina ya Kenya na Mahakama ya mjini The Hague.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limemnukuu Bensouda akisema kuwa ushahidi haukupatikana dhidi ya Rais Kenyatta kutokana na ukosefu wa ushirikiano .Rais Kenyatta alikuwa anakabiliwa na tuhuma za kuhusika na machafuko yaliyotokea mwanzoni mwa mwaka wa 2008 baada ya kufanyika uchaguzi mkuu wa Kenya.

Ghasia hizo zilisababisha vifo vya watu zaidi ya 1000. Lakini Rais Kenyatta alizikanusha tuhuma hizo. Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limefahamisha kwamba kesi ya makamu wa Kenyatta William Ruto ambae pia anatuhumiwa kuhusika na ghasia hizo itaendelea.

Ulaya yalaumiwa kwa utepetevu

Kamishna wa Umoja wa Mataifa anaeshughulikia masuala ya haki za binadamu Seid Raad al Hussein amezilaumu nchi za Ulaya kwa utepetevu wao juu ya maaafa yanayowakumba wakimbizi. Gazeti la "die tageszeitung " limemnukuu kamishna huyo akiyatoa malalamiko hayo.

Gazeti hilo limemnukuu Kamishna Seid Raad al -Hussein akisema ,kutokana na maafa makubwa yanayowafika binadamu, msimamo wa kutojali, miongoni mwa nchi za Ulaya ni jambo la kushtusha sana. Gazeti la "tageszeitung" linafahamisha katika taarifa yake kwamba,tokea mwanzoni mwa mwaka huu wakimbizi zaidi ya laki mbili wameenda Ulaya, ikiwa pamoja na kutoka Afrika. Lakini wengine zaidi ya 3,000 walikufa baharini. Idadi kubwa waliekelea Italia na Malta ,miongoni mwao wakimbizi 34,500 kutoka Eritrea.

Gazeti la "die tageszeitung"limearifu kuwa Waziri wa mambo ya ndani wa Uejrumani,Thomas de Maiziere ameshauri kujengwa kituo barani Afrika kitakachowashughulikia wakimbizi wanaoelekea barani Ulaya.

Jee Oscar Pistorius atasimamishwa tena kizimbani?

Gazeti la "Berliner Zeitung " linatueleza kwamba kwa mara nyingine Oscar Pistorius yumo katika hali ya wasi wasi Mwanamichezo huyo wa Afrika Kusini aliekatwa miguu yote miwili anaweza kupewa adhabu kali zaidi ya kifungo cha zaidi ya miaka 15 jela.

Hakimu Thokozile Masipa aliehukumu kesi ya Pistorius amemruhusu mwendesha mashtaka wa serikali awasilishe rufani kuipinga hukumu iliyotolewa hapo awali ambapo Pistorius alipatikana na hatia ya kumwuua mpenzi wake lakini siyo kwa kudhamiria.Na hivyo alipewa adhabu ya kifungo kifupi cha miaka mitano jela. Na angeliweza kutoka jela baada ya miezi 10 tu. Lakini gazeti la"Berliner Zeitung" linatufahamisha kwamba Oscar Pistorius atawekwa ndani hadi hapo uamuzi juu ya rufani utakapotolewa.

Waendesha mashtaka wanataka Pistorius ahukumiwe kwa mauaji ya kudhamiria. Hata hivyo kwa sasa mwanamicheo huyo yupo kwenye hospitali ya jela ya Kgosi Mampuru ambako mazingira ni mazuri kwake.

Mafanikio yapatikana katika harakati za kupambana na malaria

Gazeti la "die tageszeitung" wiki hii pia limendika juu ya harakati za kupambana na maradhi ya Malaria. Gazeti hilo linasema mafanikio yamepatikana, lakini bado watu 1500 wanakufa kila siku kutokana na maradhi hayo, idadi kubwa ikiwa ile ya watoto.

Gazeti la "die tageszeitung" limeikariri ripoti ya shirika la afya duniani WHO ikisema kuwa idadi ya watu wanaoyapata maradhi hayo na wale wanaokufa imeendelea kupungua. Kwa mujibu wa ripoti hiyo watu Milioni 198 waliugua malaria mwaka jana na 584,000 walikufa. Kwa usemi mwingine idadi ya wagonjwa ilipungua kwa 9,000,000


Hata hivyo gazeti la "die tageszeitung" linatilia maanani katika taarifa yake kwamba asilimia 90 ya vifo vinavyotokana na maradhi ya Malaria vinatokea barani Afrika. Gazeti hilo limearifu kwamba mafanikio makubwa yamefikiwa katika utaratibu wa kuugundua mapema ugonjwa huo. Mnamo mwaka 2008 ni vipimo milioni 46 tu vilivyofanyika lakini mwaka jana vipimo milioni 319 vilifanywa na madaktari kwa mafanikio.

Mwandishi:Mtullya Abdu.Deutsche Zeitung.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman