Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 27.12.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yamechapisha taarifa na yameandika maoni juu ya mgogoro wa Sudan ya Kusini.Pia yameandika juu ya Jamhuri ya Afrika ya Kati

Marais Salva Kirr wa Sudan ya Kusini na Uhuru Kenyatta wa Kenya

Marais Salva Kirr wa Sudan ya Kusini na Uhuru Kenyatta wa Kenya

Gazeti la "Süddeutsche" limechapisha taarifa juu ya mgogoro wa Sudan ya Kusini.

Taarifa hiyo imeanza kwa kichwa cha habari "kusambaratika kwa taifa changa" Taarifa hiyo inasema vita vya kupigania mamlaka vinasababisha vifo vya maalfu ya watu katika Sudan ya Kusini nchi iliyojipatia uhuru hivi karibuni tu.

Gazeti la "Süddeutsche" linasema katika taarifa yake kwamba hapo awali, aliekuwa makamu wa Rais wa Sudan ya Kusini Riek Machar alikanusha habari kwamba anakusuduia kuuangusha utawala wa Rais Salva Kirr lakini sasa anatoa mwito wa wazi kabisa juu ya kumwangusha Rais Salva Kirr.

Gazeti la "Süddeutsche " limemnukuu Riek Machar akisema katika mahojiano na Radio moja ya Ufaransa kwamba yupo tayari kusimamisha mapigano lakini kwanza lazima Rais Salva Kirr ajiuzulu.

Mtoto mchanga aingia mchanga

Gazeti la "die tageszeitung" linasema ndoto ya watu wa Sudan ya Kusini imetoweka. Katika maoni yake juu ya mgogoro wa nchi hiyo gazeti hilo linasema "Jumuiya ya kimataifa inakubaliana kwamba mauaji lazima yaepushwe katika Sudan ya Kusini. Lakini jumuiya ya kimataifa imesimama tu na kuona jinsi mauaji yanavyoendelea nchini humo." Gazeti la "die tageszeitung" linasema katika maoni yake kwamba licha ya mjadala juu ya wajibu wa kuwalinda raia, baada ya kutokea maafa ya Rwanda, mnamo mwaka wa 1994,jumuiya ya kimataifa bado haina mikakati thabiti ya kuyazuia mauaji halaiki. Hata hivyo gazeti hilo linasema jumuiya ya kimataifa bado haijachelewa kabisa kuyaepusha maafa katika Sudan ya Kusini.

Damu yavuja Jamhuri ya Afrika ya Kati

Gazeti la "Berliner Zeitung" limechapisha taarifa juu ya mgogoro wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.Katika taarifa hiyo gazeti hilo linasema majeshi yanayojaribu kuingilia kati yamekalia kuti kavu .Gazeti hilo linaarifu zaid kwamba nchi za Umoja wa Ulaya bado zimesimama mbalimbali juu ya kuchukua hatua za kijeshi katika sehemu nyingine za dunia. Wakati Ufaransa inasonga mbele katika kuyapeleka majeshi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, Ujerumani inakanyaga breki.

Gazeti la "Berliner Zeitung "linaeleza kwamba wakati Ufaransa ilipoingilia kati nchini Mali mwanzoni mwa mwaka huu, ilifanikiwa haraka. Lakini katika Jamhuri ya Afrika Kati,mafanikio bado yapo mbali. Gazeti hilo limemnukuu Waziri wa ulinzi wa Ufaransa Jean -Yves Le Drian akisema kwamba walipoingilia kati nchini Mali, walimjua adui wa kupambana naye.

Udugu wa kiislamu waitwa magaidi

Gazeti la "die tageszeitung" wiki hii pia limeyatupia macho matukio ya nchini Misri.Linasema katika taarifa yake kwamba baada ya kutokea shambulio la bomu, nchini humo utawala unaoshikiliwa na jeshi umeitangaza jumuiya ya Udugu wa kiislamu kuwa kundi la kigaidi ingawa ni kundi lingine lililosema kuwa lilihusika na shambulio hilo.


Umoja ni nguvu kwa wakulima wa Msumbiji

Gazeti la "Neues Deutschland" limeutumia msemo huo kuhusiana na mafalahi ,wakulima wadogo wadogo nchini Msumbiji.

Gazeti linaarifu katika makala yake kwamba wakulima hao wameungana ili kuzitetea haki zao.Umoja wa wakulima hao unasaidia katika kujenga mshikamano.Gazeti la "Neues Deutschland" limearifu kwamba kutokana na kuungana,wakulima hao wameweza kufungua akiba ya benki na hivyo kuwawezesha wakulima kuchukua mikopo.

Gazeti la "Neues Deutschland" linafahamisha kwamba ushirika wa wakulima hao wa Msumbiji ni muhimu katika kulijibu swali iwapo ustawi wa uchumi nchini humo utachangia katika juhudi za kupambana na umasikini.Ustawi mzuri wa uchumi pamoja na vitega uchumi katika miradi mikubwa ya wawekaji kutoka nje mpaka sasa havijaleta maendeleo ya kijamii. Gazeti hilo,linasema watu wa Msumbiji-sasa wanajaribu kutumia njia nyingine ili ,kuleta maendeleo ya kijamii na kuzilinda haki zao.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman