1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya14 Desemba 2013

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Kenya. Pia yameandika juu ya Madiba na juu ya mgogoro wa Jamhuri ya Afrika Kati

https://p.dw.com/p/1AZoE
Wakenya washerehekea miaka 50 ya uhuru
Wakenya washerehekea miaka 50 ya uhuruPicha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Gazeti la die "tageszeitung" limeandika juu ya miaka 50 ya Kenya kwa kusema kwamba watu wa Kenya wamesherehekea miaka 50 tokea nchi yao ijipatie uhuru kutoka kwa wakoloni wa Uingereza kwa furaha kubwa ,matumaini lakini pia ulikuwa wasaa wa kujisahihisha.


Gazeti la die "tageszeitung" limemnukuu Rais Uhuru Kenyatta akisema watu wa Kenya wanaudhimisha mwaka wa 50 wa uhuru wao kwa fahari na furaha kubwa.Lakini gazeti la die "tageszeitung" pia limemnukuu mwanaharakati Boniface Mwangi akisema kwamba hakuna cha kusherehekea.

Gazeti hilo limemkariri Mwangi akisema wakati alipoingia madarakani Rais Uhuru Kenyatta aliahidi kupambana na umasikini na magonjwa..Lakini mpaka leo maadui hao bado wapo, na baya zaidi ni kwamba umeongezeka uovu wa ufisadi.

Horst Köhler amuenzi Madiba

Gazeti la "Die Zeit" limechapisha makala juu ya Nelson Mandela anaetarajiwa kuzikwa leo katika mji wa Qunu. Makala hiyo imeandikwa na aliekuwa Rais wa Ujerumani Horst Köhler aliekutana na Mandela mnamo mwaka wa 2006 mjini Maputo.

Katika makala hiyo Rais wa zamani wa Ujerumani Horst Köhler amesema kwamba Mandela alikuwa shujaa lakini hakuwa mtakatifu. Hata hivyo badala ya kulipiza kisasi baada ya kutoka jela Mandela alihubiri maridhiano. Bwana Köhler amesema juu ya Mandela kwamba alikutana na kiongozi alieyaweka kando maslahi yake ya kibinafsi. "Mandela amatuonyesha jinsi ya kuleta mabadiliko kwa njia ya amani". Rais huyo wa zamani wa Ujerumani amesema ni wajibu wetu kuuiga mfano wa Mandela.

Jamhuri ya Afrika ya Kati

Gazeti la" Frankfurter Allgemeine" limeandika juu ya mgogoro wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na dhima ya Ufaransa.

Gazeti hilo linakumbusha katika makala yake kwamba Ufaransa imekuwa inayalinda maslahi yake barani Afrika kwa zaidi ya nusu karne.Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linaeleza kwamba sera ya Ufaransa ya kujiingiza kijeshi barani Afrika ni ya muda mrefu sawa na kipindi cha tokea nchi za Afrika zijipatie uhuru. Lakini aghalabu Ufaransa imekuwa inaingilia kati katika msingi wa mikataba ya siri iliyotiwa saini baina yake na viongozi wa nchi za Afrika.

Gazeti linakumbusha kwamba Ufaransa iliingilia kati kijeshi nchini Gabon kumrudisha madarakani Rais Leon M'ba mnamo mwaka wa 1964.Hata hivyo gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linasema ujiingizaji wa Ufaransa wakati huo ulienda sambamba na maslahi yake ya kiuchumi. Lakini safari hii Ufarasna imesema imepeleka majeshi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ili kuepusha mauaji kama yale yaliyotokea Rwanda.

Wananchi waporwa ardhi Msumbiji

Gazeti la "Neues Deutschland" wiki hii linalizingtia suala nyeti la ardhi nchini Msumbiji.Gazeti hiloli nasema katika makala yake kwamba sera ya uporaji wa ardhi inakiuka haki za binadamu. Gazeti hilo linaeleza kuwa ardhi inapokuwa bidhaa ya kuuzwa na kununuliwa basi ,kukiukwa kwa haki za binadamu kunasogea karibu. Licha ya kuyatambua madhara yake sera hiyo bado inaendelea barani Afrika, na haionyeshi dalili ya kupungua.

Gazeti hilo linasema kaskazini mwa Msumbiji kuna mpango mkubwa wa kuwahamisha watu.Gazeti la "Neues Deutschaland" linafahamisha kwamba chini ya mradi unaoitwa "Pro Savannah," hekta kati ya milioni sita na 14 zitakodishwa kwa watu wa nje kutoka Japan na Brazil.Majimbo yatakayohusika kaskazini mwa Msumbiji ni pamoja na Nampula, Niassa na Zambezi.

Mwandishi: Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Mohammed Khelef