Afrika katika magazeti ya Ujerumani. | Magazetini | DW | 27.08.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani.

Magazeti ya Ujerumani yatoa maoni juu ya matukio ya nchini Misri,kuapishwa kwa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe na pia yanazingatia mjadala juu ya maendeleo ya barani Afrika. Jee wakoloni warudi tena Afrika?

Husni Mubarak aachiwa

Husni Mubarak aachiwa


Gazeti la "Frankfurter Allegmeine" limechapisha makala juu ya kuachiwa kwa aliekuwa Rais wa Misri Hosni Mubarak.Gazeti hilo linasema mgogoro wa kisiasa nchini Misri unatishia kuwa mkubwa zaidi baada ya mahakama ya mjini Cairo kuamuru kuachiwa kwa Mubarak alieangushwa na jeshi mnamo mwaka wa 2011 kutokana na shinikizo la waandamanaji. Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linasema kwamba kuachiwa kwa Mubarak kunaweza kusababisha wimbi lingine kubwa la upinzani nchini Misri.

Gazeti hilo linatilia maanani kwamba uamuzi wa kumwachia Mubarak umepitishwa wakati ambapo tayari pana mvutano mkubwa baina ya wafuasi wa chama cha Udugu wa kiislamu na serikali ya mpito iliyopachikwa na jeshi lililomwondoa madarakani Rais aliechaguliwa kwa njia za kidemokrasia,Mohammed Mursi.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine pia limeandika juu ya Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe . Rais Mugabe ameapishwa kwa mara ya saba kuwa Rais wa Zimbabwe ,wakati kukiwa na mashaka juu ya uwezo wake, kutokana na umri wake mkubwa. Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linatilia maanani kwamba sherehe za kuapishwa kwa Mugabe zilifanyika kwenye uwanja wa soka wa Harare, ili kuwavutia wananchi wengi.

Viongozi wa nchi na Wakuu wa serikali zaidi ya 40 walialikwa kwenye sherehe hizo, lakini ni wachache tu waliohudhuria,ikiwa pamoja na marais wa Tanzania, Jakaya Kikwete waJamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Joseph Kabila na Hifikipunye Pohamba wa Namibia. Mpinzani mkuu wa Mugabe,Morgan Tvsangarai aliisusia ghafla ya kuapishwa kwa Mugabe.

Gazeti la"Frankfuret Allgemeine" pia linazitilia maananni shutuma zilizotolewa na nchi za magharibi juu ya uchaguzi wa Rais nchini Zimbabwe.Lakini gazeti hilo limemkariri Rais Mugabe akijibu kwa kusema kuwa shutuma hizo ni fedheha.

Jee bara la Afrika linaweza kuendelea bila ya misaada kutoka nje? Jee wakoloni watarudi tena barani Afrika.

Hicho ni kichwa habari cha makala iliyochapishwa na gazeti la "Die Welt" Makala ya gazeti hilo inatokana na kauli iliyotolewa na mtengenazaji filamu kutoka Camerun Jean Pierre Bekolo. Akizungumza katika mahojiano na jarida la wasomi linaloitwa "Chimurenga," Bekolo amesema kuwa viongozi wa Afrika wameshindwa kuleta maendeleo na amesema kwamba itapasa wakoloni warudi tena barani Afrika.

Gazeti la "Die Welt" linauliza jee maoni hayo ni mtengenezaji filamu huyo peke yake,au yanawakilisha ya wasomi wa barani Afrika kwa jumla? Katika makala yake gazeti la "Die Welt" linakumbusha juu ya kitabu cha mtaalamu mmoja wa uchumi kutoka Camerun. Mtaalamu huyo wa uchumi Axelle Kabou anasema viongozi wa Afrika waliamini kwa makosa kwamba dunia nzima inapaswa kutoa fidia kwa nchi za Afrika kwa udhalimu uliotendwa na wakoloni.

Mtaalamu huyo wa uchumi anadai kwamba Waafrika wenyewe ndiyo wanaopaswa kulaumiwa kwa hali duni ya maendeleo katika bara lao. Hata hivyo gazeti la "Die Welt" linatilia maanani kwamba kitabu hicho kiliandikwa mnamo miaka ya 90.

Wakati gazeti "Die Welt" linakumbusha juu ya riwaya maarufu ya Ayi Kwei Armah-inayoitwa "wema bado hawajazaliwa", iyaozungumzia juu ya kutamauka kwa Waafrika baada ya kupatikana kwa uhuru,gazeti hilo pia limemkariri aliekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan akishutumu rushwa,ukabila na upendeleo-yaani mambo yanayokwamisha maendeleo barani Afrika.

Gazeti la "Die Welt" pia limewakariri baadhi ya wasomi barani Afrika wakisema kuwa kauli ya Jean Pierre Bekolo kwamba ,wakoloni wapaswa kurudi barani Afrika ili kuleta maendeleo, ina mapungufu mengi.


Mwandishi: Mtullya Abdu

Mhariri: Mohammed Khelef