AFRIKA KATIKA MAGAZETI YA UJERUMANI. | Magazetini | DW | 23.07.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

AFRIKA KATIKA MAGAZETI YA UJERUMANI.

Magazeti ya Ujerumani yasema hali katika eneo la Pembe ya Afrika ni mbaya sana

default

Wakimbizi wa Somalia kwenye kambi ya Dadaab ,Kenya

Mamilioni ya watu wamo katika hatari ya kufa njaa kutokana na ukame wa kiwango kisichokuwa na mithili katika kipindi cha miaka 60 iliyopita. Magazeti karibu yote ya Ujerumani yameandika juu ya maafa hayo.

Gazeti la Die Welt linasema watu wapatao milioni 15 kwenye eneo la pembe ya Afrika wamo katika hatari ya kufa njaa. Wasomali wenye uwezo wanakimbilia Kenya. Lakini siyo wote wanaofanikiwa kufika kwenye kambi ya wakimbizi nchini humo. Na wanaokufa kwanza ni watoto.

Gazeti la Die Welt linaeleza katika makala yake kwamba hali nchini Somalia ni mbaya zaidi kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Gazeti hilo pia linatilia maanani kwamba kwa muda wa miezi kadhaa wataalamu na mashirika muhimu pamoja na Umoja wa Mataifa yamekuwa yakiyaona maafa ya njaa yakinyemelea hadi, jumatano iliyopita ambapo Umoja wa Mataifa uliitangaza hali ya Pembe ya Afrika kuwa ya maafa ya njaa.

Katika taarifa yake gazeti la Süddeutsche Zeitung limeandika kuwa Umoja wa Mataifa umelitangaza eneo la Pembe ya Afrika kuwa ni sehemu ya maafa ya njaa.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine limeripoti katika taarifa yake kuwa Umoja wa Mataifa ulianza kuwapelekea watu wa Somalia misaada jumamosi ya wiki iliyopita.Ndege ya kwanza ya Shirika la Umoja huo la misaada kwa watoto UNICEF ikiwa na shehena ya chakula na dawa ilitua katika mji wa Baidoa sehemu inayodhibitiwa na kundi la waislamu wenye itikadi kali al Shabaab

Gazeti la Frankfurter Allgemeine limemkariri msemaji wa shirika la UNICEF akieleza kuwa hakuna ushuru uliolipwa kwa kwa al -Shaabab. Gazeti la Der Spiegel pia limeandika juu ya maafa ya njaa katika eneo la pembe ya Afrika. Gazeti hilo linaeleza kuwa maafa hayo yanatokea kana kwamba yamepangwa. Wataalamu wameyaona maafa yakinyemelea kwa muda wa miezi kadhaa kwenye eneo la pembe ya Afrika. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba kutokana na mabadiliko ya tabia nchi ,mvua hazikunyesha, lakini wakati huo huo idadi ya watu imeongezeka mara nne katika eneo hilo.

Gazeti hilo pia limeeleza kuwa mashirika ya misaada yanatumia sehemu ya fedha kwa ajili ya kukabiliana na hali za dharura.Kwa hiyo aghalabu ni kiasi kidogo cha fedha kinachobakia ambacho hakitoshelezi kwa ajili ya kujenga visima au kununua mbegu.

Wiki hii magazeti ya Ujerumani pia yameandika juu matukio ya kisiasa magharibi na kaskazini mwa Afrika.

Rais Alpha Conde wa Guinea amenusurika kifo baada ya shambulio lililofanywa na askari waasi kwenye makaazi yake. Hizo ni habari zilizoandikwa katika gazeti la Frankfurter Allgemeine. Gazeti hilo limeandika katika makala yake kwamba katika usiku wa kuamkia jumanne iliyopita askari waasi waliyashambulia kwa mizinga ya vifaru, makaazi ya Rais huyo katika mji mkuu wa Guinea ,Konakry. Gazeti hilo limezikariri taarifa zilizothibitisha kuwa askari mmoja aliuawa katika shambulio hilo.

Gazeti hilo limeendelea kueleza, kwamba sababu ya askari waasi kujaribu kumuua Rais Conde haijulikani,lakini yumkini shambulio walilolifanya linahusiana na kukamatwa kwa kanali maaruf Moussa Keita, wiki mbili zilizopita. Kanali Keita alikuwamo katika utawala wa hapo awali wa dikteta Lansana Konte aliefariki dunia mnamo mwaka wa 2008. Kanali huyo alikamatwa baada ya kutoa madai kwamba Jenerali Sekouba Konate aliiba dola milioni 22. Jenerali huyo ndiye aliezitayarisha hatua za kuirejesha Guinea kwenye utawala wa kiraia.

Magazeti ya Süddeutsche Zeitung na Frankfurter Zeitung yameandika juu ya matukio ya kisasa nchini Misri. Süddeutsche limearifu juu ya mabadiliko yaliyofanywa katika baraza la mawaziri wakati hali ya kutoridhika miongoni mwa wananchi inazidi kuwa kubwa. Gazeti la Frankfurter limearifu juu ya kujiuzulu kwa Waziri wa mambo ya nje Muhhammad al Orabi baada ya siku 20 tu katika wadhifa huo.

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri/-Othman Miraj

 • Tarehe 23.07.2011
 • Mwandishi Abdu Said Mtullya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/122IS
 • Tarehe 23.07.2011
 • Mwandishi Abdu Said Mtullya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/122IS