1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afisa wa Umoja wa Mataifa awasili Guinea.

Halima Nyanza19 Oktoba 2009

Afisa mwandamizi wa Umoja wa Mataifa amewasili Guinea, kuanza majadiliano, kuhusu uchunguzi wa mauaji ya watu wengi yaliyofanywa na jeshi nchini humo, huku shinikizo la kimataifa likiongezeka dhidi ya utawala wa kijeshi.

https://p.dw.com/p/K9hh
Kiongozi wa Kijeshi wa Guinea Conakry, kapteni Moussa "Dadis" Camara(kati). Majadiliano ya kimataifa yameanza kuchunguza mauaji ya watu wengi yaliyofanywa na wanajeshi wake.Picha: AP

Wakati Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, anayeshughulikia utatuzi wa migogoro, Haile Menkerious amewasili jana mjini Conakry na kufanya mazungumzo na kiongozi huyo wa kijeshi nchini humo Kapteni Moussa Dadis Camara na kutarajia pia kukutana na viongozi wa kanda hiyo ya Afrika magharibi, kiongozi huyo wa utawala wa kijeshi, ameahirisha kutoa uamuzi kama atashiriki katika uchaguzi ujao, kuwania nafasi ya kuwa Rais wa nchi hiyo.Halima Nyanza na taarifa zaidi..

Menkerious ambaye yupo katika kitengo cha masuala ya siasa, amewaambia waandishi wa habari mjini Conakry, kwamba amekwenda nchini humo kufikisha ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ambaye yuko tayari kutuma Tume ya Uchunguzi kutokana na kwamba nchi zote jirani za Afrika magharibi zimeshtushwa na tukio hilo la mauaji.

Kiongozi wa Kijeshi wa Guinea, anakabiliwa na shinikizo la kimataifa kumtaka ajiuzulu kufuatia mauaji ya watu 157, waliokuwa wakikutana kwenye uwanja wa mpira mjini Conakry, kupinga utawala wake wa kijeshi mwezi uliopita.#B#

Watu walioshuhudia tukio hilo wanasema wanajeshi pia waliwadhalilisha kijinsia wanawake waliohudhuria mkutano huo wa upinzani.

Serikali ya nchi hiyo inasema watu waliouawa katika shambulio hilo ni 57 tu.

Kapteni Camara ameomba radhi kutokana na mauaji hayo na kulaumu kwamba waliofanya kitendo hicho ni wanajeshi wasio na nidhamu.

Siku ya Jumamosi, Umoja wa Afrika ulimpa Kapteni Camara muda wa hadi usiku wa Jumamosi kuamkia jana kuahidi kwa maandishi kwamba hatogombea katika uchaguzi wa rais utakaofanyika nchini humo Januari mwakani kama alivyoahidi wakati alipochukua madaraka katika mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika Desemba mwaka uliopita.

Umoja wa Afrika umetishia kuuwekea vikwazo kiongozi huyo wa kijeshi iwapo ataendelea na msimamo wake.

Siku ya Jumamosi nchi 15 za Jumuia ya kiuchumi ya nchi za Afrika magharibi -ECOWAS-, ambayo tayari imeisimamisha Guinea uanachama, iliiwekea nchi hiyo vikwazo vya silaha baada ya utawala huo wa kijeshi kujaribu kununua silaha zaidi.

Katibu Mtendaji wa ECOWAS Dokta Mohammed Ibn Chambas amesema wamechukua hatua hiyo kutokana na ukatili huo uliofanywa nchini humo wa mauaji ya watu wengi.

Akizungumzia kuhusiana na vikwazo hivyo, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Guinea, Alexandre Cece Loua, amesema vikwazo havitatatua matatizo yaliyopo, na kusema kwamba Camara bado hana nia ya kutekeleza maombi hayo ya kumtaka kukaa pembeni na badala yake kutaka upatanishi wa kimataifa.

Viongozi wa nchi za Afrika magharibi wamekuwa na wasiwasi kwamba ghasia nchini humo zinaweza kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuvuruga amani katika kanda hiyo.

Mwandishi: Halima Nyanza(dpa,afp)

Mhariri: Josephat Charo