1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afisa wa ngazi ya juu wa kanali Gaddafi atiwa mbaroni

20 Septemba 2011

Afisa wa ngazi ya juu wa jeshi la aliyekuwa kiongozi wa Libya, kanali Muammar Gaddafi, amekamatwa kusini mwa nchi hiyo, huku viongozi wa baraza la mpito wakiendelea kuvutana kuhusu kuunda serikali mpya.

https://p.dw.com/p/12cgP
Aliyekuwa kiongozi wa Libya, Muammar GadhafiPicha: AP

Jenerali Belgacem Al-Abaaj, mkuu wa idara ya ujasusi ya kanali Gaddafi amekamatwa katika eneo la Al Khofra hapo jana, yapata kilometa 100 kutoka mji wa kusini wa Sabha. Kwa mujibu wa msemaji wa wapiganaji wa baraza la mpito la Libya mjini Benghazi, Mohamed Wardugu, jenerali Al-Abaaj, ambaye amekuwa akisakwa, alitiwa mbaroni pamoja na familia yake walipokuwa wakisafiri kutumia magari makubwa ya kifahari.

Jenerali huyo anashutumiwa kwa kufanya uhalifu wa kivita huko Al Khofra na wakati mji wake ulipodhibitiwa na waasi, alikimbilia Al Joufra, ambako aliendeleza harakati dhidi ya vikosi vya utawala mpya wa Libya.

Mapigano makali yameripotiwa mjini Bani Walid wakati wapiganaji wa baraza la mpito walipoushambulia mji huo ambako mtoto wa kiume wa Gaddafi, Seif al Islam, anaaminiwa amenasa, pengine pamoja na babake.

Libyen Seif al-Islam Gadhafi im Fernsehen in Tripolis
Mtoto wa Gaddafi, Seif al-IslamPicha: dapd

Serikali ya mpito ya Libya imesema vikosi vyake vimeuteka uwanja wa ndege mjini Sabha pamoja na ngome. Mji huo unadhibiti njia kubwa muhimu kutoka nje ya Libya kupitia kusini kwenda Niger, njia ambayo imekuwa ikitumiwa na wapambe wa Gaddafi kuikimbia Libya.

Msemaji wa jeshi la baraza la mpito, Ahmed Bani amewaambia waandishi wa habari mjini Tripoli hapo jana kuwa vikosi vyao viko katika uwanja huo wa ndege na kwenye ngome iliyojengwa na mkoloni wa zamani wa Libya, Italia. Msemaji huyo aidha amekanusha madai kwamba vikosi vya Gaddafi vimewakamata mamluki 17, baadhi yao wakiwa raia wa Uingereza na Ufaransa, katika mapigano huko Bani Walid.

Waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Ufaransa, Alain Juppe, amesema hakuna mamluki wowote wa Ufaransa nchini Libya, huku wizara ya kigeni ya Uingereza kwa upande wake ikisema haina taarifa kuhusu ukweli wa madai hayo.

Frankreich Außenminister Alain Juppe
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa, Alain JuppePicha: dapd

Yote haya yanajiri wakati viongozi wa baraza la mpito wakiendelea kuvutana kuhusu kuunda serikali mpya. Waziri mkuu wa mpito, Mahmoud Jibril, alishindwa kutangaza serikali mpya Jumapili iliyopita na duru zinasema jukumu lake yeye mwenyewe limekuwa kikwazo. Kuna mvutano pia kama ni sawa kutangaza serikali ya mpito kabla kuitangaza Libya kuwa huru, jambo ambalo maafisa wa baraza la mpito wanasema linawezekana tu wakati wafuasi wote wa Gaddafi watakaposhindwa kabisa.

Nepal Wahlen
Ian Martin, mumbe wa Umoja wa Mataifa nchini LibyaPicha: AP

Kwa upande mwingine katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amemteua mjumbe maalumu kwa ajili ya Libya, Ian Martin. Martin amekuwa akiratibu shughuli za mashirika ya umoja huo nchini Libya na miradi ya benki ya dunia na amekuwa akishirikiana kwa karibu na baraza la mpito la Libya. Martin amewahi kufanya kazi Timor Mashariki, Nepal, Ukanda wa Gaza, Ethiopia na Eritrea.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/RTRE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman