Afisa wa Jeshi la Marekani nchini Iraq akiri kuwa jeshi lake bado lina kazi kubwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.12.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Afisa wa Jeshi la Marekani nchini Iraq akiri kuwa jeshi lake bado lina kazi kubwa

Afisa wa Juu wa Jeshi la Marekani nchini Iraq, Jenerali David Petraeus ameelezea kuridhishwa kwake na maendeleo yaliyopatikana nchini humo, lakini amekiri kuwa jeshi lake bado liko mbali na ushindi unaotarajiwa.

default

Afisa wa Jeshi la Marekani nchini Iraq, David Petraeus

Jenerali Petraeus aliyasema hayo wakati alipokuwa akizungumzia ziara ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani Robert Gates nchini Iraq.

Petraeus ambaye mwezi Septemba alitangaza uwezekano wa kupunguza wanajeshi wa Marekani nchini Iraq, alisema kwa tahadhari kwamba wanafanya kazi kubwa kuhakikisha kuwa wanajenga mafanikio waliyoyapata.

Amefahamisha kuwa katika siku za karibu wamekuwa wakijisikia vizuri na hali iliyokuwapo ya mafanikio licha ya kuwepo na mashambulizi ya hapa na pale.

Hata hivyo Petraeus alikiri kuwa, bado kuna kazi kubwa ya kufanya katika masuala ya usalama nchini Iraq.

Aidha amekiri kuwa mtandao wa Al-qaida wa wapiganaji wa kisunni nchini Iraq bado wamekuwa ni hatari licha ya taarifa za kupungua kwa ghasia nchini humo.

Jenerali Petraeus amesema kutokana na hali hiyo inabidi wachukue tahadhari kubwa na sio tu kujipa matumaini mengi ya mafanikio.

Amefafanua kuwa kuna uwezekano wa mtandao huo wa Al-qaeda kufanya mashambulizi mengine wakati wowote.

Kwa upande wake Waziri wa Ulinzi wa Marekani Robert Gates amesema ghasia nchini Iraq zimepungua na kwamba hali hiyo inaonesha mafanikio ama ushindi katika masuala ya kiusalama, utulivu na uimara pamoja na uwezekano wa kuwepo kwa demokrasia nchini humo.

Akizungumzia zaidi kuhusu ziara yake nchini Iraq Waziri Gates alikuwa na haya ya kusema;

’’Moja ya sababu kubwa ya ziara yangu nchini Iraq, ni kutafuta njia nzuri ya kuwezesha jinsi gani tunaweza tukafanya kazi pamoja sio tu kwa ajili ya kutoa msukumo wa hali ya miezi ya hivi karibuni lakini pia kuijenga hali hiyo, nafahamu kuwa watu wa Iraq ni zaidi katika changamoto hii’’.

Akiwa ziarani nchi Iraq , Waziri wa Ulinzi wa Marekani Robert Gate ametarajiwa pia kukutana na viongozi wa ngazi za juu wa nchi hiyo akiwemo Waziri Mkuu wa nchi hiyo Nuri Al Malik.

Baadaye Waziri Gates ataelekea Bahrain kuhudhuria mkutano wa kikanda unaohusu masuala ya usalama utakaofanyika mwishoni mwa wiki.

Imeelezwa kuwa watu 23 waliuawa jana kufuatia mashambulio manne tofauti ya bomu lililotegwa katika gari kwenye miji minne ya nchi hiyo.

Bomu moja lililipuka karibu na msikiti wa Washia mjini Baghdad, eneo ambalo ni jirani na ambako Waziri Gate alikutana na viongozi wa Iraq, ambako watu 15 waliuawa na wengine 35 kujeruhiwa . idadi ambayo ni kubwa toka kutokea kwa shambulio kubwa mwezi Septemba mwaka huu.

 • Tarehe 06.12.2007
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CY40
 • Tarehe 06.12.2007
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CY40

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com