Afghanistan:Taliban kuendeleza mapambano hadi Ramadhan | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.05.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Afghanistan

Afghanistan:Taliban kuendeleza mapambano hadi Ramadhan

Mkutano wa viongozi kutoka matabaka mbalimbali nchini Afghanistan uliofanyika kwa lengo la kutafuta uwezekano wa kuanzisha mazungumzo ya amani na kundi la Taliban, huku kundi hilo likisema litaendeleza mapambano.

Mkutano huo wa siku nne, ambao ulihudhduriwa na wajumbe wapatao 3,200 kutoka nchini kote umekamilika siku moja kabla ya ratiba iliyopangwa hapo awali. Mapendekezo 23 ya kusitisha mapigano mara moja utakapoanza mwezi mtukufu wa Ramadha yalitolewa.

Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani, aliyehudhuria sherehe ya kufunga mkutano huo, amesema serikali yake itautii mwito huo, lakini amesema kundi laTaliban pia linatakiwa kukubaliana na mwito huo na vilevile  kuutekeleza.

Ghani aliongeza kusema katika kuonyesha ishara ya nia njema, serikali yake itawafungua wafungwa 157 wa Taliban. Amelitaka kundi hilo la wanamgambo kupeleka wawakilishi kwa ajili ya kuwapokea wafungwa hao watakaoachiwa kutoka gerezani.

Madai mengine yaliyotolewa na wajumbe yalijumuisha kuongeza kasi ya mchakato wa amani, mazungumzo ya moja kwa moja kati ya serikali ya Afghanistan na kundi la Taliban, na uteuzi wa kikosi cha wawakilishi watakaoendesha mazungumzo yote ya Amani pamoja na Taliban.

Walioshiriki kwenye halmashauri ya upatanishi ni pamoja na wawakilishi wa serikali za mitaa, wazee wa kikabila, wasomi wa dini, mashirika ya kiraia na wawakilishi wengine. Kulingana na waandaaji wa mkutano huo, kati ya asilimia 30 na 35 ya washiriki walikuwa ni wanawake.

Hata hivyo Taliban bado hawajajibu kuhusiana na wito wa kusitisha mapigano na hapo awali walionyesha kuupinga mkutano huo, wakiuita kuwa ni sehemu ya majigambo ya vibaraka wa Marekani katika juhudi za kuuendeleza mchakato wa kulidanganya taifa.

Wajumbe wa Afghanistan walioshiriki kwenye mkutano wa Kabul (picture-alliance/AP Photo/R. Gul)

Wajumbe wa Afghanistan walioshiriki kwenye mkutano wa Kabul

Msemaji waTaliban Zabihullah Mujahid amesema badala yake mjumbe wa Marekani anayeshughulikia Afghanistan Zalmay Khalilzad anapaswa kutoa ujumbe kwa Marekani kwamba inapaswa kuacha matumizi ya nguvu.

Katika taarifa ya Ijumaa, Wataliban wameukataa mwito wa kukomesha mapigano, wakisema

mashambulizi yataendelea wakati wa Ramadan lakini kundi hilo limesema wapiganaji wake wataweka

tahadhari kubwa ili raia wasidhurike wakati wa operesheni yoyote watakaayoendesha. Kundi hilo limesema linawataka askari wa Marekani na wa washirika wao wa NATO lazima kwanza waondoke kutoka nchi Afghanistan.

Baadhi ya wanasiasa muhimu wa Afghanistan hawakuhudhuria mkutano huo, ikiwa ni pamoja na Mtendaji Mkuu Abdullah Abdullah na Rais wa zamani Hamid Karzai miongoni mwa wengine. Abdullah ambaye ni mshirika wa Rais Ghani katika Serikali ya Umoja wa kitaifa amesema hakuhudhuria kwa sababu hakushauriwa kabla ya kufanyika uamuzi wa kufanya mkutano huo.

Kwa upande wake Rais wa zamani Hamid Karzai, amesema mkutano huo haukuzingatia maslahi ya Waafghan, amesema mkutano huo ulipasa kuwasaidia Waafghan kujenga hali ya kuaminiana na kuzingatia misingi ya amani, na sio vinginevyo.

Serikali imefanya jitihada katika miaka ya hivi karibuni kukaa chini naTaliban ili kupata suluhisho la amani katika mgogoro wa muda mrefu nchini Afghanistan. Watalibaan hadi sasa wamekataa kuingia kwenye mazungumzo rasmi ya amani na serikali ya Afghanistan, ingawa kundi hilo la waasi limekutana na wawakilishi wa Marekani tangu kipindi cha majira ya joto cha mwaka uliopita.

Mazungumzo kati ya Marekani na Taliban yanalenga kutafuta ufumbuzi wa kisiasa kwa mgogoro wa Afghanistan na kujaribu kuumaliza mgogoro mrefu zaidi katika historia ya Marekani.

Vyanzo:/AP/DPAE

 

 

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com