1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afghanistan: Matokeo ya uchaguzi yazusha mzozo mpya

Daniel Gakuba
19 Februari 2020

Baada ya tume ya uchaguzi ya Afghanistan kumtangaza Ashraf Ghani kuwa mshindi wa uchaguzi uliofanyika Septemba 28, mpinzani mkuu wa rais huyo, Abdullah Abdullah ameyakataa matokeo hayo, na kujitangaza kuwa ndiye mshindi.

https://p.dw.com/p/3XzLc
Abdullah lehnt Ghanis Wiederwahl ab und kündigt eine Parallelregierung in Afghanistan an
Abdullah Abdullah, mpinzani mkuu wa Rais Ashraf Ghani wa AfghanistanPicha: AFP/W. Kohsar

 

Matokeo hayo yaliyotangazwa Jumanne alasiri, yalionyesha kuwa Rais Ashraf Ghani alipata asilimia 50.64 katika uchaguzi wa Septemba 28, huku mpinzani wake wa karibu Abdullah Abdullah akipata asilimia 39.52. Kwa matokeo hayo, alisema mkuu wa tume hiyo Hawa Alam Nuristani, Ghani alishinda muhula wa pili madarakani bila kuhitaji duru ya pili ya uchaguzi.

Abdullah Abdullah ambaye alikuwa pia mshirika wa Rais Ashraf Ghani katika serikali ya umoja wa kitaifa, bila kuchelewa aliyapinga matokeo hayo, akisema yeye na washirika wake ndio washindi, na kwamba wangeanza mchakato wa kuunda serikali.

''Matokeo yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi yalikuwa ni wizi wa uchaguzi, mapinduzi dhidi ya demokrasia, na usaliti kwa maamuzi ya umma, na tunayachukulia kuwa haramu,'' alisema Abdullah mbele ya mashabiki wake, na kuongeza kuwa historia ya Afghanistan itawahukumu wadanganyifu, na ''sisi tutaunda serikali inayowakilisha kila mtu.''

Changamoto juu ya changamoto

Marekani ambayo inao maelfu ya wanajeshi nchini Afghanistan, haijatoa tangazo la kumtambua Rais Ashraf Ghani kama mshindi halali, lakini wanadiplomasia mjini Washington wamesema kuwa mjumbe wa nchi hiyo katika mazungumzo na Wataliban, Zalmay Khalilzad, alikuwa amewasili mjini Kabul, tayari akifanya mazungumzo na viongozi wa kisiasa.

Weltwirtschaftsforum 2020 in Davos | Aschraf Ghani, Präsident Afghanistan
Ashraf Ghani, Rais wa AfghanistanPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Schreiber

Msemaji wa Khalilzad, Molly Phee, amesema mvutano kati ya Ashraf Ghani na Abdullah Abdullah unaleta changamoto nyingine katika siasa za Afghanistan, ukiwemo ule wa unaohusu mchakato wa amani.

Mafahali wawili

Uhasama baina ya wanasiasa hao wawili una mzizi mrefu, kwani hata matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2014 yalibishaniwa, huku Abdullah akidai ulikumbwa na mizengwe lukuki. Marekani ililazimika kuingila kati, na kufanikiwa kuunda serikali ya pamoja iliyoongozwa na Ashraf Ghani kama rais, na Abdullah Abdullah kama mtendaji mkuu.

Haya yanajiri wakati Marekani ikikaribia kupata makubaliano na kundi lenye silaha la Taliban katika mazungumzo yanayofanyika mjini Doha. Pande mbili hizo zinasema kuna uwezekano wa kuyasaini makubaliano hayo mwishoni mwa mwezi huu wa Februari, ikiwa siku saba za usitishaji wa mapigano walizowekeana zitamalizika bila matatizo.

Lakini hata Wataliban waliyatupilia mbali matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa jana, wakisema kuchaguliwa tena kwa Ashraf Ghani kunakwenda kinyume na mchakato wa kutafuta amani.

rtre, dpae