1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afghanistan: Loya Jirga yataka pande zote zisitishe mapigano

2 Mei 2019

Maelfu ya Waafghanistan wanaoshiriki katika Baraza la Kijadi kujadili uwezekano wa amani kati ya serikali ya nchi hiyo na Wataliban, wamezitaka pande hizo mbili kusitisha mapigano kama hatua ya kwanza kuelekea muafaka.

https://p.dw.com/p/3HpJb
Afghanistan Kabul - Friedensgespräche
Picha: picture-alliance/AP Photo/R. Gul

Lengo kuu la mkutano wa baraza hilo la kijadi lijulikanalio kama ''Loya Jirga'', ambao ulianza Jumatatu wiki hii ni kuyapa msukumo mazungumzo kati ya Marekani na kundi la waasi la Taliban, yanayoazimia kumaliza vita vya Afghanistan ambavyo vimekuwepo tangu mwaka 2001. Wajumbe wapatao 3,200 wanashiriki katika baraza hilo linalokutana katika hema kubwa katika mji mkuu Kabul.

Kundi la Taliban linalopigana kurejesha utawala wa Kiislamu limekataa katakata kuzungumza na serikali ya mjini Kabul inayoongozwa na Rais Ashraf Ghani, likisema serikali hiyo ni kibaraka wa Marekani. Vile vile kundi hilo limepuuza mwaliko wa kushiriki katika Baraza la Loya Jirga.

Afghanistan Peace Talks Afghanistan Loya Jirga Kabul Ashraf Ghani
Rais wa Afghanistan, Ashraf GhaniPicha: Reuters/O. Sobhani

Sayed Abdul-rahman, msemaji wa kamati mojawapo katika baraza hilo, amesema wanachokitaka raia wa Afghanistan ni amani inayoshirikisha pande zote.

''Pande zote zinapaswa kutangaza usitishwaji wa mapigano, mara moja. Vyama vyote vya kisiasa vinapaswa kusuluhisha tofauti zao na serikali, ili tuweze kuwa na sauti moja kuelekea amani. Amani inayoshirikisha wote ndio matarajio ya Waafghanistan.'' Amesema.

Mtazamo sawia

Wito huo umeungwa mkono na mjumbe anayewakilisha sehemu ya Kusini mwa nchi Abdul Hannan, ambaye amesema vita nchini humo vitamalizika tu, ikiwa pande zinazohasimiana zitaweka silaha chini kabla ya kusaini makubaliano ya amani.

Afghanistan Herat Taliban Kämpfer
Kundi la Taliban linataka vikosi vya kigeni viondoke kwanza kabla ya kusitisha mapiganoPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Khan

Wataliban wamekataa uwezekano wa kusitisha mapigano, hadi pale wanajeshi wa NATO wapatao 17,000, miongoni mwa 14,000 wakiwa Wamarekani, watakapokuwa wameondoka kwenye ardhi ya Afghanistan.

Soma zaidi: Kongamano la "Loya Jirga" lafunguliwa Afghanistan

Wanawake wanaoshiriki wametaka hakikisho kuwa haki za wanawake zitaendelea kuheshimiwa hata baada ya kuondoka vikosi vya kigeni kutoka Afghanistan.

Wanasiasa mashuhuri wasusia

Hata hivyo, baraza hili limepata pigo kwa kususiwa na wanasiasa mashuhuri, akiwemo rais wa zamani Hamid Kharzai, wanaolitazama kama jukwaa la rais Ashraf Ghani kuimarisha nafasi yake ya kuchaguliwa tena katika uchaguzi utakaofanyika mwaka huu.

Baraza la Loya Jirga ambalo hukutana kwa nadra, mara hii linafanyika kukiwa na mazungumzo baina ya Marekani na Wataliban nchini Qatar. Mazungumzo hayo ambayo ni sehemu ya mkakati wa Rais Donald Trump wa kuondoa wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan, yanataka ahadi ya Wataliban kwamba nchi hiyo haitageuzwa kituo cha makundi ya kigaidi, baada ya wanajeshi wa Marekani kufungasha virago na kuondoka.

Ingawa maazimio rasmi ya baraza hilo yatatangazwa mwishoni mwa kikao chake kesho Ijumaa, tayari idadi kubwa ya wajumbe wanaunga mkono mazungumzo kati ya serikali na Wataliban.

rtre,ape