1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afghanistan haitoachwa mkono na Marekani

12 Mei 2010

Marekani itawajibika kwa mustakabali wa Afghanistan hata baada ya vikosi vyake kuondoka Afghanistan. Hiyo amehakikishiwa Rais wa Afghanistan Hamid Karzai anaefanya ziara ya siku nne nchini Marekani.

https://p.dw.com/p/NM08
Afghanistan's President Hamid Karzai, left, and Secretary of State Hillary Clinton hold opening discussions to repair relations following public criticisms from both sides, at the State Department in Washington, Tuesday, May 11, 2010. Karzai's four-day trip to the U.S. comes as Nato prepares for an assault in southern Kandahar province. (AP Photo/J. Scott Applewhite)
Rais wa Afghanistan,Hamid Karzai (kushoto) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton.Picha: AP

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton, alipokutana na Rais Karzai na ujumbe mkubwa wa mawaziri waliofuatana nae mjini Washington, alisema:

"Wacha niseme wazi kabisa. Katika wakati ambapo tunajiandaa ipasavyo kuelekea kipindi cha mpito katika mapambano ya kimataifa nchini Afghanistan, jukumu la Marekani kuelekea umma wa Afghanistan litaendelea kwa muda mrefu."

Kwa mujibu wa waziri Clinton,wajibu huo utaendelea hata baada ya vikosi vya Marekani kurejea nyumbani, kwani kutozingatiwa kwa Afghanistan kwa miongo kadhaa ndio sababu ya kukosekana utulivu nchini humo na kuwa maficho ya wafuasi wa Al Qaeda. Hilo ni somo lililopatikana.

Tangu siku ya Jumatatu, Karzai amekuwa na mikutano ya kujadili masuala mbali mbali kuanzia usalama,uchumi hadi uongozi bora mjini Kabul. Na hii leo Karzai atakaribishwa na Rais Barack Obama katika Ikulu mjini Washington. Mkutano huo unatazamiwa kufungua ukurasa mpya katika uhusiano wa viongozi hao wawili na kuonyesha umoja wakati huu wa vita.

Miezi ya hivi karibuni, Karzai alikuwa akikosolewa wazi wazi na Marekani kwa kuvumilia rushwa katika serikali yake - na kiongozi huyo wa Afghanistan akajibu kwa kuzikosoa vikali nchi za Magharibi. Khofu za Marekani kuhusu rushwa nchini Afghanistan hazikutoweka, lakini serikali ya Obama sasa inajitahidi kushughulikia masuala kama hayo faraghani na kutomkosoa Karzai hadharani.

Washington, inafahamu vizuri kuwa kumtenganisha Karzai, kutahatarisha uungaji mkono unaohitajiwa kutoka Waafghanistan ili mkakati wa vita wa Marekani uweze kufanikiwa. Ziara ya Karzai inafanywa wakati majeshi ya Marekani yakijiimarisha kuwashinda waasi wa Taliban nchini Afghanistan na kuleta utulivu nchini humo na hatimae kutimiza ahadi ya Rais Obama kuanza kuvirejesha nyumbani vikosi vya Marekani katika mwezi wa Julai mwaka 2011.

President Barack Obama makes a statement to the nation Sunday night following the final vote in the House of Representatives for comprehensive health care legislation, in the East Room of the White House in Washington, March 21, 2010. Obama and Democratic House leaders resolved a dispute over abortion Sunday, securing crucial support from a handful of lawmakers. (AP Photo/Gerald Herbert)
Rais wa Marekani,Barack Obama.Picha: AP

Rais Obama, katika jitahada ya kutuliza khofu za Karzai kuhusu ratiba hiyo, atasisitiza ahadi ya kuendelea kuiunga mkono Afghanistan kwa miaka mingi ijayo. Bila shaka wengi wa Waafghanistan watakuwa na shaka, hasa wakikumbuka jinsi Marekani ilivyowaacha mkono, pale vikosi vya Soviet Union ya zamani vilipoondoka Afghanistan mwaka 1989.

Mwandishi: Martin,Prema/DPA/RTRE

Imepitiwa: M.Abdul-Rahman