Adhabu ya kifo yathibitishwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.07.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Adhabu ya kifo yathibitishwa

Eti kweli bahshishi itawaokoa wauguzi watano wa Bulgaria na daktari wa kipalastina?

Jeshi lailinda mahakama kabla ya adhabu ya kifo kuthibitishwa mjini Tripoli

Jeshi lailinda mahakama kabla ya adhabu ya kifo kuthibitishwa mjini Tripoli

Korti kuu ya Libya jana imethibitisha hukmu ya kifo dhidi ya wauguzi watano wakike kutoka Bulgaria na daktari mmoja wa kipalastina.Walikutikana na hatia mwaka 2004 ya kuwaambukiza virusi vya maradhi ya UKIMWI zaidi ya watoto mia nne wa Libya.Wahukumiwa wote sita wamekua daima wakidai hawana hatia.Wanasiasa wa Ulaya wameelezea wasi wasi wao na kuikosoa vikali hukmu hiyo.Hawajakosea.

Kuthibitishwa kwa mara nyengine tena hukmu hiyo ya kifo kunadhihirisha wazi kabisa:kiongozi wa mapinduzi ya Libya Muammar Al Gaddafi bado hajakivua kikamilifu kilemba cha jangili na kujigeuza “mshirika” wa nchi za magharibi. Hata kama Gaddafi hawatumi tena magaidi na silaha nzito nzito katika kila pembe ya dunia,ameachana na mradi wa kinuklia na kukubali eti kuwalipa fidia nono kabisa familia za wahanga wa mashambulio ya Lockerbie,bado lakini Gaddafi anasalia kua muimla asiyekadirika na asiyeaminika katika masuala ya ushirikiano.Hasa kama hakuna ule mtindo wa nipe nikupe.

Sawa kabisa kwamba hukumu hii mpya haikumridhisha Gaddafi.Lakini itakua ujinga kuamini kwamba mfumo wa sheria wa Libya ni huru na haushawishiwi na mtawala wa kimabavu.

Ingawa Libya chini ya uongozi “wa mkuu wa mapinduzi mwenye kupenda makubwa” inajivunia sifa ya uongozi miongoni mwa mataifa ya eneo hilo,hata hivyo haijafikia daraja ya kuitwa nchi inayofuata sheria.

Hali hiyo imedhihirika katika kesi hii ya usumbufu dhidi ya matabibu wa kigeni, inayoendelea kwa muda mrefu hivi sasa.Wamehukumiwa adhabu ya kifo eti kwasababu ya kuwaambukiza maksudi watoto 400 wa Libya virusi vya UKIMWI,japo kama wenyewe wanashikilia hawana hatia na kwamba walilazimika kukiri kwasababu waliteswa.

Jengine lenye uzito mkubwa zaidi ni ile hali kwamba ripoti ya wataalam inayowatakasa na kuwatoa hatiani watuhumiwa hao haijazingatiwa hata kidogo hukumu ilipotangazwa.Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya wataalam,matabibu hao sio chanzo cha kuambukizwa watoto hao,bali uchafu ulioenea katika hospitali hiyo.

Si hasha kwa hivyo kuwaona majaji wakitoa hukmu isiyo ya haki:kinyume chake ingekua sawa na kuukosoa mfumo wa afya wa taifa, kwa maneno mengine kuukosoa utawala wa Muammar Gaddafi.Ghadhabu zinazoeleweka za familia za wahanga wa UKIMWI zingeelekezwa wakati huo moja kwa moja dhidi ya mwenye kudhibiti madaraka mjini Tripoli.

Matumaini ya mwisho walio nayo matabibu hao hivi sasa ni hongo,kutokana na kiu cha utawala wa Libya cha kutaka kuzidi kutambuliwa kimataifa.Jumatatu ijayo baraza la mahakimu wakuu wa Libya linakutana kuzungumzia kadhia hiyo.Baraza hilo linaweza ama kuthibitisha adhabu hiyo ya kifo,kuibatilisha au kuibadilisha.Itategemea pengine na fedha ambazo wazungu wamesema wako tayari kuwalipa familia za wahanga.Yuro milioni 10 kwa kila familia ndizo zinazotajikana.Uvumi ulizagaa hata kabla hukmu mpya kutangazwa,eti makubaliano yamefikiwa.

Ikiwa kweli basi hali hiyo itamaanisha Ulaya inakubali kushiriki katika mchezo wa kamari wa Gaddafi-itamaanisha inakubali kuridhia kiini macho cha kisheria kitakacho mfanya Gaddafi anaonekane kama karimu mkubwa nchi za nje na ndani uangaliwe kama ushindi uliopatikana kwa njia ya mazungumzo kwa masilahi ya watoto walioambukizwa virusi vya UKIMWI.Kwa waliohukumiwa ufumbuzi kama huo ni baraka.

 • Tarehe 12.07.2007
 • Mwandishi Sollich / Oummilkheir Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHB2
 • Tarehe 12.07.2007
 • Mwandishi Sollich / Oummilkheir Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHB2

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com