Adhabu ya kifo yatekelezwa Marekani. | Masuala ya Jamii | DW | 24.09.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Adhabu ya kifo yatekelezwa Marekani.

Kutekelezwa kwa adhabu ya kifo katika jimbo la Virginia, nchini Marekani, kumechochea hasira kali kutoka kwa watu wanaoipinga adhabu ya kifo.

Teresa Lewis.

Teresa Lewis.

Jimbo hilo limetoa adhabu kwa mwanamke mmoja nchini humo, ambaye amekuwa wa kwanza kwa takriban karne moja kuhukumiwa adhabu hiyo kwa kuchomwa sindano ya sumu.

Afisa wa gereza la Greensville katika jimbo hilo la Virginia, nchini Marekani, Larry Traylor, aliarifu juu ya kutekelezwa kwa adhabu ya kifo dhidi ya mama huyo, Teresa Lewis, mwenye umri wa miaka 41, jana jioni, ambapo alipatikana na hatia ya kuhusika na mpango wa kumuua mumewe na mtoto wake wa kambo.

Afisa huyo amesema kwamba Lewis, ambaye alipatikana na hatia mwaka 2003, alikuwa mtulivu wakati akielekea katika chumba cha kifo, na kwamba alikuwa akionekana kama mtu aliyedhamiria kufa.

Lakini, hata hivyo, waandishi wa habari wanasema mama huyo alikuwa akionekana ana hofu na kutetemeka.

Hukumu hiyo imetolewa baada ya mahakama kuu nchini Marekani kutengua rufani ya Lewis.

Wakati hukumu hiyo ikitekelezwa, nje ya gereza hilo la Greensville kulikusanyika takriban watu 30 wanayoipinga adhabu hiyo ya kifo, wakisali na kupiga kengele wakati mwanamke huyo akienda kuuawa.

Watu wanaotaka kufutwa kwa adhabu hiyo ya kifo walisisitiza kuwa mama huyo alikuwa na matazizo ya akili na kwamba watu waliokwenda kumuua mumewe walikuwa wajanja zaidi na kuutumia udhaifu wa mama huyo.

Akizungumzia juu ya kutekelezwa kwa adhabu hiyo, wakili wa Bibi Lewis alisema kwa inaamaanisha kuwa mfumo wa sheria umekiukwa.

Kwa upande wa mwanachama katika shirikisho la taifa la kukomesha adhabu ya kifo, Jack Payden-Travers, ameelezea kutekelezwa kwa adhabu hiyo sawa na kile alichokiita ''mauaji ya binadamu yaliyo halali''.

Teresa Lewis ni mfungwa wa kwanza mwanamke kutekelezewa adhabu yake ya kifo katika jimbo hilo la kusini tangu mwaka 1912, baada ya msichana mweusi aliyekuwa na umri wa miaka 17, kuuawa baada ya kuwekwa kwenye kiti cha umeme.

Aidha mwanamke huyo pia ni wa 12 kuuawa nchini humo tangu adhabu hiyo ya kifo ilipoanza tena mwaka 1976.

Licha ya kuwa na uwezo mdogo wa akili, Teresa Lewis alizingatiwa kama ni mwenye afya nzuri kwa ajili ya hukumu hiyo.

Alikiri kosa la kukodi watu wawili mwaka 2002 kwa ajili ya kumuua mumewe na mtoto wake wa kambo ili kuweza kupokea malipo ya bima ya mumewe.

Alikiri kuacha mlango wazi ili kuwawezesha wauaji hao kuingia na kumuua mumewe na mtoto wake wa kambo aliyekuwa na miaka 25.

Wauaji wote watatu walikiri makosa, wakihukumiwa kifungo cha maisha gerezani, na Lewis adhabu ya kifo.

Hata hivyo, watu wanaomuunga mkono mama huyo wamehoji kwanini ahukumiwe kunyongwa wakati waliofanya mauaji wamehukumiwa kifungo cha maisha gerezani.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp)

Mhariri: Miraji Othman

 • Tarehe 24.09.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PLcs
 • Tarehe 24.09.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PLcs
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com