1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Adhabu aliyopewa Habre ni mfano wa kwanza

31 Mei 2016

Aliekuwa dikteta wa Chad Habre amehukumiwa kifungo cha maisha kwa kutenda uhalifu. Katika maoni yake mwandishi wetu Dirke Köpp, anasema hiyo ni ishara thabiti ,kwamba bara hilo linao uwezo wa kuwahukumu madikteta

https://p.dw.com/p/1Ixe1
Aliekuwa dikteta wa Chad Hissene Habre
Aliekuwa dikteta wa Chad Hissene HabrePicha: Getty Images/AFP

Watu walioathirika na uhalifu uliotendwa na Hissene Habre alietawala nchini Chad kuanzia mwaka wa 1982 hadi 1990 walisubiri muda mrefu kuona haki ikitendeka. Kwa muda wa robo karne hapakuwapo ishara ya kuonyesha kutambuliwa kwa maumivu yaliyowasibu.

Na jambo baya zaidi ni kwamba dikteta Habre aliewatendea uhalifu maalfu ya watu, aliweza kuishi maisha mazuri katika jumba la kifahari kwa muda miaka mingi, katika hifadhi ya kisiasa nchini Senegal, bila ya wasi wasi wowote.

Rais wa Senegal wa wakati huo Abdoulaye Wade alimlinda mhalifu huyo.Wade hakuchua hatua yoyote ili Habre awajibishwe kwa uhalifu wake ingawa mnamo mwaka wa 2006 Umoja wa Afrika uliipa Senegal jukumu la kuichukua hatua hiyo.

Mfano mbaya

Kwa muda mrefu suala la Habre lililonekana kuwa ni mfano mwingine mbaya jinsi viongozi wa Afrika wanavyoweza kufanya uhalifu bila ya kuwajibishwa. Polisi ya siri ya Habre iliwaweka watu roho juu na kuwaandama kwa muda wa miaka minane, mfano mwingine mbaya jinsi serikali inavyoweza kuyatumia vibaya madaraka.Maalfu kwa maalfu ya watu waliteswa na wengine wapatao 40,000 waliuliwa.

Ni kutokana na msimamo thabiti wa watu waliofanyiwa unyama pamoja na ukakamavu wa mashira ya kutetea haki za binadamu kwamba iliwezekana kumfikisha Habre mahakamani. Mahakimu wa baraza maalumu la nchi za Afrika, waliotoa adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa Habre pia wanastahili pongezi.

Hukumu hiyo iliyotolewa na baraza hilo maalumu la Umoja wa Afrika ni ishara ya nguvu barani Afrika, kutokea ndani ya bara hilo.Habre ni dikteta wa kwanza kuhukumiwa kwa niaba ya bara la Afrika . Ni mfano wa kwanza.

Hukumu hiyo inathibitisha juhudi za mahakimu wa Afrika za kuujenga mfumo huria wa haki kwa Afrika, na jambo muhimu zaidi ni kuziimarisha asasi za kiraia.Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba ulipita muda mrefu kuichukua hatua hiyo.

Lakini utepetevu wa aliekuwa Rais wa Senegal Abdoulaye Wade unaonyesha kwamba njia bado ni ndefu. Barani Afrika viongozi hawatoani boriti.Kila mmoja anahofia kutolewa yake siku moja.

Mahakama ya mjini Dakar
Mahakama ya mjini DakarPicha: Getty Images/AFP/Seyllou

Hata Rais wa Senegal aliemo madaakani sasa, Macky Sall alichelea kumwita Habre dikteta. Hata hivyo Sall ametimiza ahadi yake ya kuhakikisha kwamba Habre anafikishwa mahakamani. Lakini viongozi wengi wa Afrika wana hofu kubwa ya kufikishwa mahakamani siku moja.

Na ndiyo sababu kwamba adhabu iliyotolewa kwa Habre ni muhimu ; inatoa ujumbe kwa viongozi wote kwamba ikiwa watatenda uhalifu, wataadhibiwa.

Mwandishi: Köpp,Dirke

Mfasiri: Mtullya abdu.

Mhariri: Mohammed Khelef