1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ADB kuzisaidia Cote d'lvoire, Tunisia na Misri

10 Juni 2011

Katika Mkutano wa mwaka mjini Lisbon, Benki ya Maendeleo ya Afrika, ADB, yaahadi kuisaidia, Cote d'l voire na nchi za Afrika Kaskazini baada ya mageuzi. Suala la ukosefu wa ajira na kupanda kwa maisha bado changamoto.

https://p.dw.com/p/11Y4i
Benki ya Maendeleo ya Afrika, ADBPicha: ADB

Rais wa Benki hiyo ya Maendeleo ya Afrika, Donald Kaberuka, amesema benki hiyo itaungana na wabia wengine katika kuendeleza mpango wa baadae wa Afrika Kaskazini kutokana na mabadiliko yaliotokea Tunisia, Misri, na kujenga upya uchumi wa Libya wakati utakapofika.

Akihutubia mkutano huo wa siku mbili ulioanza jana katika mji wa Lisbon, Ureno, Kaberuka amesema shabaha iwe ukuaji wa pamoja utakaolenga kuondoa changamoto zinazozikabili nchi hizo.

Mageuzi katika nchi hizo yalilkuja kufuatia kutoridhika kwa wananchi na hali ya mambo, ikiwemo ukosefu wa ajira na ukosefu wa demokrasia ya kweli.

Hali pia ilichangiwa na ongezeko la bei ya vyakula, ambazo zilienda juu kwa asilimia mbili, ikilinganishwa na ile ya kuporomoka kwa uchumi mwaka 2008.

Waziri wa Fedha nchini Ureno, Fernando Teixeira do Santos, amesema hali ya kuyumbayumba ya hivi karibuni Afrika Kaskazini, inatishia sio tu ukuaji wa uchumi katika eneo hilo, bali pia shughuli za taasisi hiyo ya kifedha.

Rais wa Benki hiyo ya Maendeleo ya Afrika, Kaberuka, ametangaza bajeti ya dharurua ya dola za kimarekani milioni 130 kuisaidia Cote d'l voire kufuatia vurugu zilizotokea nchini humo baada ya uchuguzi.

Azimio hilo la kuisaidi nchi hiyo limefungua milango kwa taasisi hiyo ya fedha kurudi kwenye makao makuu yake, katika mji wa Abidjan, baada ya kuondoka miaka nane iliyopita na kwenda Tunisia.

Kaberuka amasema ni kazi kubwa iliyo mbele ya nchi ya Cote d'l voire, lakini benki hiyo iko tayari kutimiza wajibu wake, sambamba na jumuiya za kimataifa.

Mkutano huo pia umetumiwa kama jukwaa la wagombea wa wadhifa wa mwenyekiti wa Shirika la fedha la Kimataifa, IMF.

Frankreich Finanzministerin Christine Lagarde kandidiert für IWF
Waziri wa Fedha wa Ufaransa, Christine LagardePicha: dapd

Waziri wa Fedha wa Ufaransa, Christine Lagarde, amelitumia jukwaa hilo kuwashawiishi waafrika wamuunge mkoni katika juhudi zake za kuwania wadhifa huo.

Hata hivyo, Umoja wa Afrika, unaowakilishwa katika mkutano huo, umezungumza kwa mara ya kwanza, umuhimu wa kubadilishwa makubaliano yaliyofikiwa ya kugawa nyadhifa za taasisi kuu za fedha za kimataifa kati ya Ulaya na Marekani.

Umoja huo umesema wakati umewadia sasa wa kukabidhiwa wadhifa huo mwana uchumi kutoka nchi zinazoinukia, na hasa barani Afrika.

Habari zinasema Afrika kusini itamtangaza waziri wake wa fedha, Trevor Manuel, kugombea wadhifa huo.

Mkutano huu unaofanyika mjini Lisbon umezileta pamoja nchi 77, yakiwemo mashirika ya kimataifa.

Benki ya Maendeleo ya Afrika, ADB, ina nchi 53 za Afrika kama wabia wake, na inalenga kupunguza umasikini na kuboresha hali ya maisha kwa wakazi wa Bara la Afrika.

Mwandishi: Rose Athumani/AFP

Mhariri: Miraji Othman