1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Abbas kutogombea tena urais

Ramadhan Ali6 Novemba 2009

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Wapalestina ,Mahmud Abbas, ameutosa utaratibu wa amani ya Mashariki ya Kati katika hali isiojulikana alipotangaza kwamba, hatagombea tena urais na hivyo kufungua mlango kwa Hamas kunufaika

https://p.dw.com/p/KPw0
Rais wa Mamlaka ya wapalestina Mahmoud AbbasPicha: AP

Wakati Israel imeitikia tangazo hilo kimya kimya,Marekani, yanaonesha imesharidhia  kuondoka  kwa  Mahmud Abbas ingawa itakua tayari kushirikiananae katika wadhifa mwengine wowote.

Rais huyo wa Mamlaka ya Ndani ya wapalestina,Mahmud Abbas, alisema uamuzi wake umechangiwa na  kuzorota kwa juhudi za amani na Israel.Matamshi yake aliotoa kwa njia ya TV jana usiku yamezusha uvumi kwamba, hakutoa kauli ya mwisho na yamkini, ikawa ni mbinu tu  kuihimiza Israel na mshirika wake Marekani  kuwaridhia zaidi wapalestina wanayotaka. Abbas,ameelezea ni yake ya kutogombea tena uchaguzi uliopangwa Januari, mwakani na ambao unaweza lakini, kuahirishwa  na hivyo, kurefusha kipindi chake cha sasa kwa muda usiojulikana.

Israel leo, imenyamaa kimya  juu ya uamuzi wa bw.Abbas,lakini maafisa wa Israel, wamenon`gona kuwa, wangependa kumuona Bw.Abbas anaendelea madarakani.

Gazeti la mrengo wa shoto la Israel "HAARETZ", limearifu kwamba,rais Shimon Peres  wa Israel, alimpigia simu rais  wa Mamlaka ya Ndani ya Wapalestina ,siku moja kabla kutoa tangazo lake hilo ili kumshawishi asiondoke.

"Ukiondoka, wapalestina  watapoteza fursa yao ya kujipatia dola huru....Hali ya mambo katika  eneo hili itachafuka zaidi."-gazeti  lilimnukulu rais Perez kumwambia Abbas.

Nae mjumbe wa wapalestina katika mazungumzo ya amani Saeb Erikat ,akitafsiri hatua aliochukua  rais Mahmud Abbas alisema,

"Sio suali la urais, bali hii inatokana na serikali ya Israel kuendelea na ujenzi wa maskani za walowezi wa kiyahudi,kujiamulia kabisa  mambo  na kuamrisha nini la kufanywa.Na hata miaka 19 tangu  kujaribu kusaka  suluhisho la dola 2 ,yamkini rais amefadhahika  na kuutambua ukweli wa mambo ulivyo."

Taarifa kutoka Washington, Marekani, zinasema waziri wa nje bibi Hillary Clinton, alietembelea hivi punde Mashariki ya Kati  adhihirika kuridhia hatua alioitangaza Bw.Abbas kutogombea uchaguzi hapo Januari.Alisema kuwa, atakuwa tayari kufanya kazi nae katika wadhifa wowote ule mpya atakaochukua.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) Amr Mussa,amemtaka Bw.Mahmud Abbas,  kuufikiria tena uamuzi wake wa kun'gatuka .

 Viongozi wa Palestina  wamesema kuwa,  uamuzi wa Bw.Abbas kutogombea uchaguzi hapo Januari,mwakani, unatokana na  kuvunjika kwake moyo na juhudi za Marekani  kuzuwia  ujenzi wa maskani za wayahudi -hatua ambayo wanataka ichukuliwe kwanza kabla  kuanza tena mazungumzo ya amani.

Mwandishi: Ramadhan Ali/ APE/AFPE

Uhariri:Aboubakary Liongo